Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP Rwanda yapokea dola milioni 7.2 kutoka USAID kuimarisha operesheni zake

Wakimbizi wa Burundi waliokimbilia kusaka hifadhi nchini Rwanda kufuatia ghasia nchini mwao.(MAKTABA)
UNHCr/Anthony Karumba
UNHCr/Anthony Karumba
Wakimbizi wa Burundi waliokimbilia kusaka hifadhi nchini Rwanda kufuatia ghasia nchini mwao.(MAKTABA)

WFP Rwanda yapokea dola milioni 7.2 kutoka USAID kuimarisha operesheni zake

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limekaribisha mchango wa dola milioni 7.2 uliotolewa na shirika la Marekani la maendeleo ya kimataifa USAID ili kusaidia kutoa msaada wa chakula kwa ajili ya kuokoa maisha ya wakimbizi walioko nchini Rwanda.

Katika taarifa yake aliyotoa leo huko mjini Kigali nchini Rwanda Kaimu Mkurugenzi wa WFP nchini humo Ahmareen Karim amesema fedha hizo zitatumika kusaidia wenye uhitaji kwa kuwapatia mgao wa fedha taslimu ili waweze kujikimu. Halikadhalika chakula tiba kwa wenye utapiamlo, kufadhili mipango ya kijamii inayoleta kubadili tabia kwa wakimbizi 113,500 wanaoishi katika kambi tano nchini humo. 

“Mchango huu kutoka Marekani umekuja wakati tunauhitaji zaidi. Kila siku tunapokea takriban wakimbizi wapya zaidi ya 100 Kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC na kupanda kwa gharama za chakula, nishati na usafiri, wakimbizi sasa wanahitaji msaada zaidi kuliko wakati mwingine wowote ili kuwawezesha kupiga hatua kuelekea kujitegemea,” anasema Karim.

Mchango huu ni nyongeza kwenye dola milioni 9.5 zilizopokelewa kutoka Marekani mwaka 2022 kwa ajili ya kusaidia operesheni za wakimbizi za WFP nchini Rwanda. WFP inatumia mgao wa fedha taslimu ili kuwajengea uwezo watu waweze kufanya machaguo katika kutatua changamoto wanazokabiliana nazo kwenye masoko ya ndani, wakati huo huo wakisaidia kuinua uchumi wa jamii zilizowakaribisha.

Licha ya ufadhili huu wa USAID, WFP bado haina uwezo wa kutoa mgao kamili kwa wakimbizi nchini Rwanda ili kukidhi angalau mahitaji ya kiwango cha chini ya chakula.

Mbinu mpya ya ugawaji wa misaada

Mwezi Mei mwaka 2022 WFP, kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR walianzisha mbinu ya kutoa msaada unaolenga mahitaji - mfumo ambao wakimbizi wanapewa mgao wa chakula kulingana na viwango vyao vya uhitaji.

Kutokana na upungufu wa fedha, wakimbizi walio hatarini zaidi kwa sasa wanapokea asilimia 92 ya mgao kamili na wale wanaoonekana kuwa katika mazingira magumu kiasi wanapokea asilimia 46 ya mgao kamili.

Hii inahakikisha kwamba wakimbizi walio hatarini zaidi wanapewa kipaumbele kwenye usaidizi wa chakula huku wakimbizi walio katika mazingira yasiyo magumu wanasaidiwa ili waweze kujitegemea zaidi.