Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yajenga makazi mapya 3,000 kusaidia wakimbizi wa ndani Nyiragongo DRC

Makazi mapya yaliyojengwa na UNHCR Nyiragongo kwa ajili ya wakimbizi wa ndani
UN News Video/Byobe Malenga
Makazi mapya yaliyojengwa na UNHCR Nyiragongo kwa ajili ya wakimbizi wa ndani

UNHCR yajenga makazi mapya 3,000 kusaidia wakimbizi wa ndani Nyiragongo DRC

Msaada wa Kibinadamu

Takriban watu 233,000, wamelazimika kuyahama makazi yao katika wilaya ya Nyiragongo jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kutokana na vita vinavyochochewa na kundi la wapiganaji waasi la M23 na zaidi ya asilimia 95% ya watu hawa wanaripotiwa kuishi katika makanisa, shule, viwanja vya michezo na wakati wengine wanaishi na familia zinazowapokea.  

Kwa kutambua changamoto yao shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeamua kuwanusuru kwa kuwapatia msaada wa nyumba au makazi ya dharura na limeanza na zaidi ya familia 45 ambazo ni sehemu ya wakimbizi hao wa ndani walioahama makazi yao kutoka eneo la Kanyaruchinya, na sasa wamewaka kwenye makazi mapya katika eneo la Bushagara.  

Wakiwa na furaha isio kifani wakimbizi hao sasa wanataka vita ikomeshwe kwenye vijiji vyao ili ikiwezekana warejee nyumbani. Mwandishi wetu wa Kinshasa Byobe Malenga ameenda kushuhudia makazi hayo mapaya na kutundalia makala hii. 

Takriban nyumba 3,000 zimejengwa Bushagara katika eneo hilo la Nyiragongo kaskazini mwa mji wa Goma ili kuwapokea wakimbizi wa wandani wanaoishi katika hali ya ngumu huko Kanyaruchinywa.  

Mradi huu unaotekelezwa na shirika la AIDES unafadhiliwa na kusimamiwa shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR).  

Maniraguha Feza, mkimbizi ambaye  anaishi na familia yake katika makazi ya Nyiragongo.
UN News Video/Byobe Malenga
Maniraguha Feza, mkimbizi ambaye anaishi na familia yake katika makazi ya Nyiragongo.

Kwa walengwa, hii ni furaha kama asemabvyo Maniraguha Feza ambaye aliishi katika hali mbaya katika shule moja ya msingi na sasa anaona afueni baada ya kuletwa hapa na akinuia kuhakikisha amerejesha maisha ya familia yake katika biashara ndogondogo. 

Kwa muda yeye na familia yake yote walilazimika kulala darasani pamoja na wakimbizi wengine kadhaa waliokimbia makazi yao. 

" Kabla tufike hapa tulikuwa kwenye mabarabara, shuleni. Sasa shirika la UNHCR liliona kama sio vizuri waliona tusiteseke na watoto kunyeshewa na nvua nakadhalika ndo waliamua kutujengea nyumba na kutuleta hapa. Tunashukuru UNHCR kwa msaada huu licha ya kwamba ni ndogo sababu mimi nina watoto saba ukiongeza mimi na mume wangu ndo tunafanya watu 9. Nyumba ni ndogo lakini tunashukuru maana atunyeshewi tena. Kitu tuchokikosa sasa ni shida ya njaa". 

Espérance Badakunda, mkimbizi ambaye anaishi na familia yake katika makazi ya Nyiragongo.
UN News/Byobe Malenga
Espérance Badakunda, mkimbizi ambaye anaishi na familia yake katika makazi ya Nyiragongo.

Mateso ya nenda rudi kutokana na vita yamekuwa mengi na yenye kuchosha na kusikitisha katika eneo hilo lakini kwa Espérance Badakunda, sasa kwake yamekuwa historia kwani anasema amefurahishwa na hatua hii ya UNHCR. 

"Nilikuwa nalala pabaya sababu nilikuwa nalala katika shule huku nikilala kati ya watu wengi watoto, baba na mama yangu. wakati tulikuwa katika shule hiyo Tulishituka kuona UNHCR inakuja kutuorodhesha na kutujengea nyumba kisha kutuhamisha mmoja baada ya mwingine. Waliotujengea tunawaambia tunashukuru na tunawapigia asante wazidi kutusaidia na wale ambao hawajapata nyumba nao wawanjengee ili wahame.Tunaomba viongozi watusemee ili turudi kwetu". 

Licha ya wakimbizi kadhaa kupata msaada huu lakini bado kuna changamoto kubwa kwa wakimbizi wa ndani.  

Joseph Kamenge,mkimbizi anayeishi katika kambi hii ya wakimbizi DRC, kwenye nyumba iliyoezekwa kwa majani ya mgomba akiwa na familia yake yote
UN News Video/Byobe Malenga
Joseph Kamenge,mkimbizi anayeishi katika kambi hii ya wakimbizi DRC, kwenye nyumba iliyoezekwa kwa majani ya mgomba akiwa na familia yake yote

Katika eneo la kanyaruchinya waliosalia wanaendelea kupitia hali mbaya ya maisha. Hiki ndicho kisa cha Joseph Kamenge, anayeishi hapo, kwenye nyumba iliyoezekwa kwa majani ya mgomba na familia yake yote, watoto 8 na wazazi wawili akisema kuwa wakati wa mvua, nyumba hii hailaliki 

«Tazama jinsi kunavyolowana hapa na matope. Niko na watoto sita na mke na mimi ndio jumla ya idadi ya watu 8. Hii ni majani ya migomba ya ndizi ndio tunajihifadhi ndani sasbabu mtu ambaye hana uwezo wa kununua hema anajengea nyasi hizi». 

Shirika la UNHCR linatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa ya kibinadamu na wafadhili kuunga mkono Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kushughulikia ipasavyo mahitaji ya watu walio katika mazingira magumu. Umoja wa Mataifa unakaribisha kitendo hiki na unanuia kufanya vyema zaidi.  

Abdoulaye Barry ni mjumbe wa ofisi ya UNHCR huko Goma-DRC anasema "Kufikia leo, tumejkamilisha makazi zaidi ya 2000. Tulifanikiwa kufunga tanki la maji la zaidi ya lita za ujazo 70 na vyoo kadhaa na vituo vya maji vilijengwa. Na pia, nimeona majiko mengi ambayo yamejengwa. Tulihisi kwamba mahali walipokuwa, hasa Kanyaruchinywa, si mahali pazuri pa kuishi. Na kutokana na kwamba wanakabiliwa na hatari zote za ajali za barabarani, magonjwa ya kuambukiza, uasherati na pia hatari zingine za kila aina. Ni katika muktadha huu ndio tumeanzisha kambi hii mpya na tungependa kuiendeleza". 

Familia nyingi zimekimbia makazi yao mkoani Kivu Kaskazini kufuatia mapigano mashariki mwa DRC wakielekea eneo la Kanyaruchinya katika kambi za wakimbizi wa ndani.
© UNICEF/Jospin Benekire
Familia nyingi zimekimbia makazi yao mkoani Kivu Kaskazini kufuatia mapigano mashariki mwa DRC wakielekea eneo la Kanyaruchinya katika kambi za wakimbizi wa ndani.

26 Juni, 2022, kundi la kwanza la watu waliokimbia makazi yao waliwasili katika eneo la Nyiragongo, kaskazini mwa jiji la Goma, wakikimbia mapigano makali kati ya jeshi na waasi wa M23. Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA zinakadiria kwamba idadi ya watu waliokimbia makazi yao na waliotawanywa katika jimbo hilo kuwa ni watu 521,000 kutokana na ghasia zilizozuka upya, ambapo 233,000 kati yao wanapata hifadhi katika maeneo ya hapo hapo Nyiragongo.