Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UN lathibitisha uteuzi wa Bi. Inger Andersen kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP

Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), akizungumzia tukio la Ripoti ya Pengo la Uzalishaji katika mkutano wa COP27, huko Sharm El-Sheikh, Misri.
© UNFCCC/Kiara Worth
Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), akizungumzia tukio la Ripoti ya Pengo la Uzalishaji katika mkutano wa COP27, huko Sharm El-Sheikh, Misri.

Baraza Kuu la UN lathibitisha uteuzi wa Bi. Inger Andersen kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP

Masuala ya UM

Kufuatia pendekezo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, baada ya kushauriana na Nchi Wanachama, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limemthibitisha Inger Andersen raia wa Denmark kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) kwa muhula mwingine wa miaka minne kuanzia tarehe 15 Juni 2023 hadi 14 Juni 2027.

“Bi Andersen kwa sasa anatumikia muhula wake wa awali wa miaka minne.” Imeeleza taarifa aliyoitoa Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mchana wa leo Jumatano jijini New York, Marekani.

Tweet URL

Kabla ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji mnamo mwaka 2019, kwa zaidi ya miaka 30 Bi Andersen alikuwa akijishughulisha na uchumi wa maendeleo ya kimataifa, uendelevu wa mazingira na uundaji wa sera kwa zaidi ya miaka 30. Tangu mwaka 2015 hadi 2019 alihudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la IUCN (International Union for Conservation of Nature) ambalo linafanya kazi katika uga wa uhifadhi wa asili na matumizi endelevu ya maliasili. IUCN pia wanahusika katika kukusanya na kuchambua data, utafiti, miradi ya mashinani, utetezi, na elimu.

Kabla ya hapo, Bi Andersen alikuwa Makamu wa Rais wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika katika Benki ya Dunia (2011-2015) na Makamu wa Rais wa Maendeleo Endelevu na Mkuu wa Kundi la Ushauri la Baraza la Mfuko wa Kimataifa wa Utafiti wa Kilimo (2010-2011) ikifuatiwa na kazi ya muda mrefu na Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayolenga zaidi maendeleo endelevu barani Afrika na Mashariki ya Kati.

Muda mfupi baadaye Inger Anderson kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika kuwa ni heshima kubwa kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa UN na Baraza Kuu la UN kwa awamu ya pili kama Mkuu wa UNEP. Janga la mazingira linatishia maisha yote kwenye sayari. UNEP imejitolea kutengeneza suluhu za #ForPeopleForPlanet (Kwa ajili ya watu kwa ajili ya sayari) ili kufikia #SDGs.”

Makao makuu ya UNEP yako katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.