WFP na wakfu wa Rockefeller wazindua mradi wa kuimarisha mlo shuleni

Mpishi wa shule
© WFP/Emily Fredenberg and Fredrik Lerneryd
Mpishi wa shule

WFP na wakfu wa Rockefeller wazindua mradi wa kuimarisha mlo shuleni

Utamaduni na Elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, linakaribisha msaada wa dola milioni 10.7 kutoka kwa wakfu wa Rockefeller ili kuwasaidia mamilioni ya watoto walio katika mazingira magumu kupata fursa ya chakula chenye lishe bora kupitia programu za mlo shuleni nchini Benin, Ghana, Honduras na India. Mradi huo wa miaka miwili na nusu unalenga katika kujumuisha vyakula vilivyoimarishwa kwenye milo ya shuleni pamoja na kuchagiza chakula chenye lishe zaidi katika programu zote. 

Nchini Benin, Ghana na Honduras, mradi unatarajiwa kusaidia moja kwa moja maisha ya zaidi ya watoto milioni moja wa shule.  

Mradi huo pia utakuza uzalishaji wa chakula wa ndani, kunufaisha wakulima wadogo na kuwapa wapishi wa shule taarifa kuhusu lishe bora kwa watoto.  

Nchini India, mradi huo utasaidia msaada wa kiufundi unaotolewa na WFP kwa mpango wa serikali wa mlo shuleni, kunufaisha moja kwa moja watoto 325,000, na unataka kuwafikia zaidi ya watoto milioni 110 wa shule kupitia kampeni za  chakula bora na mawasiliano zinazohimiza ulaji bora. 

Kadiri watoto wanavyokula vyakula vyenye virutubisho vingi, ndivyo wanavyochangamka zaidi, na wanafanya vizuri zaidi shuleni pia," anasema Faustin, baba yake Julienne (kushoto).
© WFP/Emily Fredenberg
Kadiri watoto wanavyokula vyakula vyenye virutubisho vingi, ndivyo wanavyochangamka zaidi, na wanafanya vizuri zaidi shuleni pia," anasema Faustin, baba yake Julienne (kushoto).

Umuhimu wa mradi huo 

Roy Steiner, makamu Rais wa mradi wa chakula wa wakfu wa Rockefeller amesema. "Mlo shuleni huwapa makumi ya mamilioni ya watoto katika nchi hizi mlo wao pekee wa kutegemewa wa siku. Kupanua wigo wa programu za mlo mashuleni kwa njia zinazohimiza ununuzi wa chakula chenye lishe bora kutawafanya watoto hao kuwa na afya njema hata kama kunachochea mabadiliko makubwa katika mfumo wa chakula. Hatimaye, mifumo ya chakula ambayo ni ya lishe, yenye kuzaliwa upya na yenye usawa itakuwa na athari kubwa nzuri katika kukomesha njaa na utapiamlo duniani.” 

WFP inasema programu za kulisha watoto shuleni ndio mtandao mpana zaidi wa hifadhi ya jamii ulimwenguni, unaofaidi moja kwa moja watoto milioni 388 ulimwenguni.  

Uchunguzi umeonyesha kuwa mara kwa mara programu hizi zinaweza kusaidia kilimo cha ndani, masoko na lishe bora huku ikiboresha afya, lishe na elimu katika jamii zilizo hatarini.  

Hata hivyo shirika hilo linasema , nchi mara nyingi zinatatizika kutoa vyakula vya kutosha vyenye afya ili kuzuia utapiamlo kwa watoto wenye umri wa kwenda shule.  

Hivi majuzi, programu za kulisha watoto shuleni pia zimelazimika kukabiliana na ongezeko la gharama za ngano na mahindi kutokana na athari za pamoja za janga la COVID-19 na vita nchini Ukraine. 

Naye Carmen Burbano, mkurugenzi wa WFP wa idara ya program za mlo shuleni amesema "WFP na wakfu wa Rockefeller wanashirikiiana kutimiza ahadi ya kutokomeza njaa, kuimarisha mifumo ya chakula na kuhakikisha ustawi wa maisha kwa wote. Mradi huu unakuza msaada wa miaka 60 wa WFP wa programu za kitaifa za mlo mashuleni lakini unafika mbali zaidi, ukilenga kubadilisha mifumo inayoleta chakula kwa watoto wa shule na familia zao."  

Julienne akiwa na wenzake wakila chakula cha mchana shuleni
© WFP/Emily Fredenberg
Julienne akiwa na wenzake wakila chakula cha mchana shuleni

Hii si mara ya kwanza wakfu wa Rockefeller kusaidia 

Mradi huu mpya uliotangazwa unatokana na ruzuku ya awali kwa WFP kutoka wakfu wa Rockefeller ili kukabiliana na utapiamlo miongoni mwa watoto nchini Burundi, Kenya na Rwanda kwa kuleta maharagwe yaliyoimarishwa na unga wa mahindi ulioirutubishwa katika milo ya shule.  

Ili kuunga mkono mabadiliko haya katika nchi hizo, WFP inafanya kazi na watendaji wa mnyororo wa thamani na wasagisaji wa kiwango cha kati katika kubadilisha nafaka nzima, ambayo ina virutubisho mara tano zaidi ya nafaka iliyosafishwa. 

Msaada huo ni sehemu ya mkakati wa chakula bora wa wakfu wa Rockefeller, ambao unalenga katika kuongeza upatikanaji wa chakula cha bei nafuu na chenye afya, kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi katika mfumo wa chakula, na kupanua wifo wa fursa za kiuchumi kwa wazalishaji wadogo na wa kati wa chakula. 

Mpango huu mpya wa unaogharimu dola milioni 10.7 pia utachangia muungano wa mlo shuleni, ambao unaleta pamoja nchi 73 zilizojitolea kuhakikisha kwamba kufikia mwaka 2030 kila mtoto duniani kote anapata mlo wa kila siku wenye afya na lishe bora shuleni.