Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makaburi ya wayahudi mjini Fez nchini Morocco, ushahidi wa jamii tofauti kuishi pamoja kwa amani

Johanna, mfanyakazi wa kujitolea katika makaburi ya Wayahudi ya Fez, Morocco.
UN News
Johanna, mfanyakazi wa kujitolea katika makaburi ya Wayahudi ya Fez, Morocco.

Makaburi ya wayahudi mjini Fez nchini Morocco, ushahidi wa jamii tofauti kuishi pamoja kwa amani

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa unasema robo tatu ya migogoro mikuu ya ulimwengu ina uhusiano na masuala ya kitamaduni na kwa hivyo kuziba pengo kati ya tamaduni ni jambo la haraka na la lazima kwa ajili ya amani, utulivu na maendeleo. Makaburi ya Kiyahudi huko Fez, Morocco ni ushuhuda wa utamaduni tofauti kuishi pamoja kwa amani.

Wakiwa katika safari ya kikazi huko Fez, kuangazia Mkutano wa tisa wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la Muungano wa Ustaarabu, UNAOC, May Yacoub na Alban Mendes De Leon kutoka Timu ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa walikutana na Johanna Devico Ohana, mzaliwa wa Fez, ambaye anajitolea kutunza makaburi haya yenye umri wa miaka 200, akitaka kutunza jina la marehemu babake ambaye mwenyewe alikuwa msimamizi wa utunzaji wa makabuli haya hadi  alipoaga dunia miezi michache iliyopita. Anold Kayanda anasimulia makala hii kwa lugha ya Kiswahili.

Umoja wa Mataifa unasema robo tatu ya migogoro mikuu ya ulimwengu ina uhusiano na masuala ya kitamaduni na kwa hivyo kuziba pengo kati ya tamaduni ni jambo la haraka na la lazima kwa ajili ya amani, utulivu na maendeleo. Makaburi ya Kiyahudi huko Fez, Morocco ni ushuhuda wa utamaduni tofauti kuishi pamoja kwa amani. Wakiwa katika safari ya kikazi huko Fez, kuangazia Mkutano wa tisa wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la Muungano wa Ustaarabu, UNAOC, May Yacoub na Alban Mendes De Leon kutoka Timu ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa walikutana na Johanna Devico Ohana, mzaliwa wa Fez, ambaye anajitolea kutunza makaburi haya yenye umri wa miaka 200, akitaka kutunza jina la marehemu babake ambaye mwenyewe alikuwa msimamizi wa utunzaji wa makabuli haya hadi  alipoaga dunia miezi michache iliyopita. Anold Kayanda anasimulia makala hii kwa lugha ya Kiswahili.

Makaburi ya Wayahudi ya Fez, Moroko.
UN News
Makaburi ya Wayahudi ya Fez, Moroko.

Fez Medina mji nchini Morocco ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka 1000, umeorodheshwa kama Eneo la Urithi wa Dunia wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO na kwa hakika panafaa kupatazama kila wakati. Katika namna mbili za tofauti zake za kitamaduni zisizogusika na zinazoonekana, Fez ni eneo moja ambalo wanaishi kwa amani na kwa pamoja jamii ya Amazigh, Waarabu, Wayahudi na makundi mengine ya kijamii. Mathalani mtaa unaoitwa ‘Mellah’, ambayo ni makazi ya wayahudi hapa mjini Fez Morroco ni uthibitisho mmoja wa uwepo na jamii mbalimbali kuishi pamoja.

May Yacoub na Alban Mendes De Leon kutoka Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa na hasa kutoka UN News walikutana na Johanna ambaye aliwafafanulia kuhusu makaburi ya Wayahudi ya Fez lakini pia kuhusu maisha ya amani kati ya jamii mbalimbali za kidini katika jiji hili la Fez.

Johanna Devico Ohana anatunza makaburi ya Kiyahudi yenye umri wa miaka 200 kutokana na ombi la baba yake, Elie Devico, ambaye aliaga dunia miezi michache iliyopita.

Johanna akitembeatembea pemezoni mwa makaburi anayoyajali sana anasema, “jina langu ni Johanna. Nimekulia hapa Fez. Nimeishi hapa katika utoto wangu wote na ujana wangu kisha nikaondoka kwenda masomoni huko Meknes, kisha huko Ufaransa.”

Johanna akiokota uchafu kidogo uliodondoka kwenye bustani anasema, “tuliishi kwa amani. Hakukuwa na mvutano. Sote tulijua sisi ni Wayahudi, Waislamu au Wakatoliki, na hatukuwahi kuwa na matatizo yoyote upande huo.”

Jamii za Kiyahudi na za Kiislamu za Morocco zimeishi kwa amani kama majirani kwa zaidi ya milenia moja yaani kwa zaidi ya miaka elfu moja. Johanna anaeleza mapenzi ya baba yake kwa mji wa Fez na Morocco kwa ujumla, "baba yangu alikuwa mpenzi wa Morocco na mpenzi wa Fez. Alikuwa mgonjwa kwa miaka mingi. Alitibiwa Ufaransa na kila mara alipoona kwamba mambo hayaendi sawa, aliniambia hivi: ‘Niahidi jambo moja: kwamba nikifa nikiwa Ufaransa, uniletee Fez.’”

Fez hivi karibuni ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa tisa wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la Muungano wa Ustaarabu, UNAOC. Muungano wa Ustaarabu unakuza tofauti za kitamaduni, wingi wa kidini, na kuheshimiana kati ya jamii. Alipoulizwa kuhusu jinsi alivyohisi alipofahamu kwamba Fez imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo, Johanna Devico Ohana alisema alijisikia "fahari" “tunajivunia kwamba Fez ilichaguliwa. Na kwa Morocco, inaonesha hasa ukweli wa taswira yetu, utamaduni wetu. Ninafanya kwa hiari kile baba yangu aliniomba nifanye, ambayo ni utunzaji wa makaburi. Kwa hiyo hapa yuko Fez, yuko karibu nasi na natumai anapumzika kwa amani.”