Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya waandishi wa habari mwaka 2022 yaliongezeka maradufu: UNESCO

UNESCO inapigania kwa kikamilifu usalama wa waandishi wa habari na wale wanaozalisha uandishi wa habari.
Unsplash/Engin Akyurt
UNESCO inapigania kwa kikamilifu usalama wa waandishi wa habari na wale wanaozalisha uandishi wa habari.

Mauaji ya waandishi wa habari mwaka 2022 yaliongezeka maradufu: UNESCO

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Waandishi wa habari 86 pamoja na watendaji wa vyombo vya habari waliuawa duniani kote mwaka 2022, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, ikichambua zaidi ya  kwamba takwimu  hizo ni sawa na mmoja katika kila siku 4. 

Taarifa ya UNESCO iliyotolewa leo Paris, Ufaransa inasema nusu ya watumishi hao waliuawa nje ya saa za kazi na hivyo “kuangazia hatari kubwa ambazo waandishi wa habari na watendaji kwenye vyombo vya habari wanakabiliwa kwa kufanya kazi yao.” 

UNESCO inasema ongezeko la mauaji ya watumishi hao mwaka 2022 limekuja na kubadili mwelekeo wa kupungua kwa mauaji katika miaka ya karibuni. 

Mathalani mwaka 2018 idadi ya vifo ilikuwa 99 na kisha kuanzia mwaka 2019 hadi 2021 idadi ikapungua hadi vifo 58 kila mwaka, kwa mujibu wa Kitengo cha UNESCO cha kufuatia mauaji ya waandishi wa habari. 

UNESCO inasema idadi hiyo ya vifo ni kumbusho juu ya pengo katika mifumo ya kisheria duniani kote na kushindwa kwa serikali kutekeleza wajibu wake wa kulinda wanahabari na kuwakinga dhidi ya uhalifu na wakati huo huo kufungulia mashtaka wale wanaotenda uhalifu dhidi ya watumishi hao. 

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay akizungumzia taarifa hii amesema “baada ya miaka kadhaa ya kupungua, sasa ongezeko la mauaji ya waandishi wa habari mwaka 2022 linatisha. Mamlaka lazima ziongeze juhudi kukomesha mauaji na kuhakikisha watekelezaji wanaadhibiwa kwa sababu kutosemea chochote ni sababu kuu ya tabia hii ya ghasia.” 

Amerika ya Kusini na Karibea imeongeza kwa mauaji mengi 

Ingawa kila ukanda umekuwa na vifo, Amerika ya Kusini na Karibea unaongoza kwa mauaji ya wanahabari mwaka 2022 na kuwa na vifo 44, zaidi ya nusu ya vifo vyote duniani, 

Asia na Pasifiki vifo 16, Ulaya Mashariki vifo 11. 

Nchi zilizokuwa na mauaji mengi zaidi ni Mexico, wanahabari 19 waliuawa, kisha Ukraine wanahabari 10 na Haiti 9. 

Nusu waliuawa wakiwa nje ya majukumu ya kikazi 

Takribani nusu yao waliuawa wakiwa nje ya majukumu yao ya kazi; mathalani wakiwa safarini, nyumbani au kwenye maegesho ya magari na maeneo mengine ya umma. 

Mauaji ya wanahabari na watendaji wa vyombo vya habari ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuripoti kuhusu uhalifu wa kupangwa, ongezeko la misimamo mikali, kuandika habari kuhusu rushwa, mazingira, matumizi mabaya ya madaraka na maandamano. 

Ukwepaji sheria umeshamiri 

UNESCO inasema ingawa kuna maendeleo katika kipindi cha miaka mitano katika kufungulia mashtaka watendaji wa mauaji ya wanahabari, bado kiwango cha ukwepaji sheria ni cha juu kikiwa ni asilimia 86. 

“Hii inathibitisha kuwa kukabili ukwepaji sheria bado ni jambo linalotaka ushirkiano wa kimataifa,” imesema UNESCO. 

Kando ya mauaji ,wanahabari bado wanaendelea kukumbwa na vitisho lukuki na ghasia kama vile kutoweshwa, kutekwa nyara, kuswekwa rumande kiholela, unyanyasaji wa kisheria, ghasia mtandaoni hasa dhidi ya wanahabari wanawake.