Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhara ya tabianchi yasomba makaburi, nyumba na uwanja wa mpira Belize

Nyumba katika Mto Monkey, ilisombwa baharini kutokana na mmomonyoko wa udongo.
UN Video/ Andrea Ocampo
Nyumba katika Mto Monkey, ilisombwa baharini kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Madhara ya tabianchi yasomba makaburi, nyumba na uwanja wa mpira Belize

Tabianchi na mazingira

Fikiria unashuhudia nyumba yako ikisombwa na maji hadi baharini; uwanja wa mpira na hata wapendwa wako makaburi yao yanasombwa hadi baharini. Huu ni uhalisia kwa wakazi wa Kijiji cha Monkey River kilichoko nchini Belize, wakazi ambao licha ya changamoto hii bado wana nia ya kuendelea kuishi kwenye eneo hili. 

Soundcloud

Video iliyoandaliwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa inaonesha mawimbi ya bahari yakipiga kwenye fukwe ya bahari, ya Karibea katika bonde la mto Monkey ulioko Belize, taifa ambalo kaskazini linapakana na Mexico, Kusini na Magharibi Guatemala na mashariki bahari ya Karibea. 

Mawimbi haya yakipiga yanajenga hofu na machungu kwa wakazi wa kijiji cha Monkey River kwenye fukwe hii kwani kile wanachokienzi na kutunza zaidi kinamezwa na maji. Mkazi wa eneo hili anasimulia akiwa kwenye eneo lenye makaburi.  Mario Muschamp mkazi wa eneo hili anasema hali ilivyoanza. 

Makaburi katika Mto Monkey, Belize, yamesombwa na maji baharini.
UN Video, Andrea Ocampo
Makaburi katika Mto Monkey, Belize, yamesombwa na maji baharini.

Sitaki kuona makaburi zaidi yakisombwa na maji 

“Tulianza kuona tatizo kutokana na mmomonyoko wa ukanda wa pwani. Kinachoniumiza zaidi , licha ya kupoteza vitu kadhaa, ikiwemo mali zetu, na uwanja mzima wa mpira wa soka, ni kule kumomonyolewa kwa eneo letu la makaburi. Bibi na Babu yangu makaburi yao yameoshwa na mawimbi ya baharí. Unajua makaburi yao yamesombwa. Inauma sana,” anasema Bwana Muschamp akiongeza kuwa wamejitahidi kulinda makaburi yaliyosalia, “kwa sababu sitaki kuona mengine nayo yakisombwa na maji. Kwani familia yangu bado iko hapa. Dada yangu, shangazi na wajomba. Binamu na marafiki wengi makaburi yao yako hatarini kumezwa na bahari.”  

Bwana Muschamp ni Rais wa Chama cha kuhifadhi eneo la mto Monkey ambako ndiko walikozaliwa na kukulia akifafanua ya kwamba, “hapa ndio nyumbani kwetu. Hapa ndipo nilipozaliwa. Hapa ndio tumekulia. Hakuna sehemu nyingine kama hii kwa ajili yetu na kama jamii hatuko tayari kuhama. Jamii ya Mto Monkey siku zote imekuwa jamii ya wavuvi na nilianza kama mvuvi, na ulikuwa wakati wa furaha.”  

Kazerine Garbot ambaye ni mwanakijiji akiwa amebarizi na mjukuu wake kwenye veranda ya nyumba yake anakumbuka siku za zamani akisema, “tulikuwa tunaishi hapo eneo ambako sasa kuna maji. Nyumba yetu ilisombwa na maji. Sasa hatuna tena ufukwe, lakini enzi hizo ilikuwa fukwe nzuri sana ambako tuliweza kutembea na kufurahia taswira ya machweo ya  jua.”  

Monkey River, Belize
UN Video/ Andrea Ocampo
Monkey River, Belize

Uchimbaji mchanga ni adui wa fukwe Belize 

Watalaamu wanaonya kuwa uchimbaji mchanga na ubadilishaji wa mkondo wa maji ya Mto Monkey ni vichocheo vya mmomonyoko wa fukwe za kijiji hiki cha Monkey River. Ili kukabiliana na hali hiyo, Chama cha kulinda eneo la Monkey River kilianzishwa. Bwana Muschamp anasema kama jamii tayari wameanza kuona mabadiliko kwenye mto. Hawakuona tena aina ya mchanga ambao ulikuwa unaonekana kwenye mto kabla ya kuanza harakati za kuhifadhi eneo hilo.  

Na zaidi ya yote, “wito wangu sasa ni kujaribu na kuona kile tunachoweza kufanya. Kuboresha na kusimamia vema kile tulichonacho. Hii ni kwa sababu ni rahisi kusimamia kile ulichonacho kuliko kurejesha kile ulichopoteza. Kwa hiyo ilibidi nijishirikishe kupitia chama hiki cha Usimamizi wa eneo la Mto Monkey. Mwaka 2017 tuliweza kutekeleza mradi wetu wa kwanza wa majaribio ya kurejesha utulivu kwenye ufukwe kwa kutumia maboza ya mipira.”  

Maboza hayo ya mpira yanajazwa mchanga na kuwa kama bamba la kuzuia mawimbi ya maji na hutengenezwa kwa vitambaa vigumu vya mpira ili visimomonyolewe na maji. Maboza hayo ya mchanga yaliwekwa mbele ya kijiji ufukweni na hivyo kusaidia wanakijiji ambao walikuwa hatarini kupoteza nyumba zao.  

Kupitia mfuko wa mazingira duniani, GEF, wanakijiji wa Monkey River waliweza kutekeleza mradi huo. 

Leonel Requena, Mratibu wa kitaifa wa GEF katika shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP nchini Belize anasema, “mradi wa mikopo nafuu midogo katika GEF inatoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa mashirika ya kiraia ili kutekeleza hatua zinazoendeshwa na jamii na kuwa na mchango kimataifa. Niliweza kujenga uhusiano zaidi na wakazi wa Monkey River ikiwemo kuelewa madhila yao, hofu na shaka kuhusu mmomonyoko, kupoteza nyumba zao, kupoteza mbinu zao wa kujipatia kipato, halikadhalika kupoteza bayonuai. Mmomonyoko wa eneo hilo la mto kwa kweli unatisha na kwangu mimi unatia hofu kubwa.”  

Mawe makubwa yamepangwa kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa udongo katika pwani wa Monkey River.
UN Video/ Andrea Ocampo
Mawe makubwa yamepangwa kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa udongo katika pwani wa Monkey River.

Mawe makubwa yatasaidia kulinda eneo letu 

Kwa Kazerine, akiwa anacheza na mjukuu wake anasema kile kinachofanyika kinamtia moyo lakini anataka kuona hatua za dharura zaidi zinachukuliwa kabla ya hatua za kudumu akisema, “Kuhusu mmomonyoko, ninatumai wanaweza kudhibiti. Waweke mfano mawe makubwa, mchanga ili kutuliza ufukwe wetu. Pindi utakapokaa sawa, wanaweza kufanya basi miradi mingine kusaidia hilo.”  

Danet Young, kiongozi katika jamii hii ya Monkey River akiwa ufukweni ambako mawe makubwa yamepangwa kuzuia mmomonyoko anazungumza na afisa kutoka UNDP akimweleza ya kwamba, “mawimbi na mchanga vilikuwa vinaingia ngazi za ghorofa ya chini na kufika hadi nyuma ya nyumba. Sasa nini kilitokea? Watu walichukua mawe makubwa na madogo tuliyopatiwa na serikali na kuyaweka ndani ya tololi na mtumbwi na kisha mbele ya nyumba kusaidia kuinua mchanga na kwa hiyo tuna imani kuwa mawe yatasaidia.”  

Mario Muschamp, Chama cha uhifadhi wa pwani wa Monkey river, Belize
UN Video/ Andrea Ocampo
Mario Muschamp, Chama cha uhifadhi wa pwani wa Monkey river, Belize

UNDP na kipaumbele cha kulinda na kuhifadhi kijiji cha Monke River 

Kwa Leonel Raquena Kijiji hiki ni kipaumbele chao kwa kuwa “jamii hii ya wavuvi wa pwani iko kusini mashariki mwa Belize. Ni jamii ndogo inayoishi kwa amani na mazingira. Kijiji cha Monkey River hakijachangia janga la tabianchi lakini wao ndio wanaathirika zaidi kwa hasara na uharibifu. Tunachohitaji ni haki na usawa kwenye tabianchi.”  

Bwana Muschamp hakati tamaa akiamini kuwa kijiji chao kitadumu, na zaidi ya yote ni kwamba “maliasili ziko hapa kwa ajili yetu sisi tuzitumie vema badala ya kuzitumia hovyo na kiholela. Hii ni kwa sababu bila maliasili, sisi hatuwezi kuishi. Iwapo tunaweza kushughulikia hiki tunachokiona, basi kijiij cha Monkey River kinaweza kuweko hapa kwa miaka mingine 100.”