Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvunjaji wa sheria umetapakaa duniani, tuchukue hatua sasa- Katibu Mkuu UN

Ukosefu wa usalama unazidi kushamiri nchini Haiti
JOA/Yes Communication Design
Ukosefu wa usalama unazidi kushamiri nchini Haiti

Uvunjaji wa sheria umetapakaa duniani, tuchukue hatua sasa- Katibu Mkuu UN

Amani na Usalama

Hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu utawala wa sheria ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa Antonio Guterres amesema ingawa nchi wanachama, mashirika ya kikanda, ya kiraia na sekta binafsi wana wajibu wa kuchangia katika kujenga na kulinda utawala wa sheria, hali ilivyo hivi sasa ni tofauti na kinachoonekana bado kuna safari ndefu ya kufikia lengo la utawala wa sheria.  

Akihutubia Baraza hilo jijini New York, Marekani, Guterres amesema uvunjivu wa sheria ni dhahiri duniani kote kuanzia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, hadi mizozo iliyojikita maeneo mbalimbali, kama Mashariki ya Kati na  Afghanistan, na kusema kuwa katika kila ukanda wa dunia, raia wanataabika kutokana na madhara ya majanga, mauaji, ongezeko la njaa na umaskini. 

Solange, mtoto mwenye umri wa miaka 11 (aliyevalia nguo ya rangi ya chungwa) alitenganishwa na famili yake alipokimbia mapigano. Sasa anaishi na familia enyeji lakini mchana anakuweko kwenye  kituo cha  malezi cha  UPDEDO kinachosaidiwa na UNICEF. Anapat…
UNICEF/Arlette Bashizi
Solange, mtoto mwenye umri wa miaka 11 (aliyevalia nguo ya rangi ya chungwa) alitenganishwa na famili yake alipokimbia mapigano. Sasa anaishi na familia enyeji lakini mchana anakuweko kwenye kituo cha malezi cha UPDEDO kinachosaidiwa na UNICEF. Anapatia stadi za kufuma vikapu.

Mifano ya uvunjifu wa sheria 

Kupitia uendelezaji wa silaha za nyuklia kinyume cha sheria, hadi matumizi ya nguvu kiholela, nchi zimeendelea kuvunja sheria ya kimataifa na kukwepwa uwajibikaji. 

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeibua janga kubwa la kibinadamu na haki za binadamu, kizazi cha watoto wenye kiwewe, na kuchochea janga la uhaba wa chakula na nishati. 

“Kitendo chochote cha nchi kujimegea eneo la nchi nyingine kutokana na tishio au kutumia nguvu ni ukiukwaji wa Chata ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa,” amesema Katibu Mkuu akikumbusha kuwa Chata ya Umoja wa Mataifa inasema “sisi watu wa Umoja wa Mataifa tumeazimia kuanzisha mazingira ambamo kwayo haki na heshima vitokanavyo na mikataba na vyanzo vingine vya sheria za kimataifa vinalindwa.” 

Huko Mashariki ya Kati, mwaka 2022 ulikuwa  mwaka mchungu zaidi kwa wapalestina na waisrael, “tunalaani mauaji yote ya kinyume chas heria na vitendo vya misimamo mikali. Hakuna chochote kile kinachohalalisha ugaidi.” 

Zaidi ya nusu ya wananchi wa Afghanistan wanategemea misaada ya kibinadamu.
IOM 2021/Paula Bonstein
Zaidi ya nusu ya wananchi wa Afghanistan wanategemea misaada ya kibinadamu.

Na wakati huo huo, kupanuliwa kwa makazi ya walowezi wa Israel na ubomoaji wa makazi na kufurushwa kwenye makazi vyote vinachochea hasira na kukata tamaa. 

Katibu Mkuu amesema pia ana wasiwasi juu ya maaamuzi ya hivi karibuni ya upande mmoja huko MAshariki ya Kati akisema, “utawala wa sheria ni kitovu cha kufanikisha amani yenye haki na ya kina kwa kuzingatia jawabu la mataifa mawili kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria ya kimataifa na makubaliano ya awali.” 

Amegusia pia uondoaji wa serikali madarakani kinyume cha katiba, akitaja mapinduzi ya kijeshi ambayo inasikitisha kuwa sasa yamerejea kuwa ndio mtindo. 

Guterres amesema mapinduzi ya kijeshi yanatia hofu zaidi hasa pale yanapofanyika kwenye maeneo ambayo tayari yana mizozo iliyojikita,  uhaba wa chakula  na ugaidi, akitolea mfano Ukanda wa Sahel. 

“Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi za kikanda za kuimarisha utawala wa kidemokrasia, amani,usalama na maendeleo endelevu,” amesema Katibu Mkuu. 

Korea Kaskazini nako mpango wa nyuklia ni tishio 

Guterres ametaja pia mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK, au Korea Kaskazini akisema mpango huo ulioko kinyume cha sheria ni hatari iliyo dhahiri, kichocheo cha mvutano kwenye eneo la Asia. “Jawabu ni DPRK ikubaliane na wajibu wa kimataifa na irejee kwenye meza ya mazungumzo.” 

Familia zilizofurushwa kutokana na machafuko Myanmar zikiwa katika jumba la watawa jimboni Rakhine nchini Myanmar.
© UNICEF Myanmar
Familia zilizofurushwa kutokana na machafuko Myanmar zikiwa katika jumba la watawa jimboni Rakhine nchini Myanmar.

Afghanistan nako maendeleo yamerudishwa nyuma 

Nchini Afghanistan, amesema Katibu Mkuu, “mashambulizi ya kimfumo dhidi ya haki za wanawake na wasichana na ukwepaji uwajibikajiwa kimataifa vinajenga ubaguzi wa kijinsia.” 

Amesema hatua hiyo inakandamiza maendeleo ya taifa hilo ambalo linahitaji mchango wa watu wote ili liweze kurejea katika amani endelevu. 

Myanmar rejesheni mpito wa kidemokrasia 

Ametaja nayo Myanmar akitaka uvunjaji wa sheria tangu mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021 umechangia kuweko kwa ghasia, ukandamizaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. 

Nasihi mamlaka zisikilize matakwa ya wananchi wao na zirejee kwenye mpito wa kidemokrasia.” 

Haiti utawala wa sheria ni dhaifu, uhalifu umefurutu ada 

Haiti nako hali si shwari, ambako Katibu Mkuu amesema hali ya taifa hilo inadhihirishwa na janga kubwa la kitaasisi na utawala dhaifu wa kisheria, bila kusahau unyanyasaji wa haki za binadamu na ongezeko la kiwango cha uhalifu, rushwa na uhalifu wa kuvuka mipaka. 

Amesihi wadau wa Haiti washirikiane kurejesha taasisi jumuishi za kidemokrasia na utawala wa sheria. 

Muonekano wa Jumba la Amani, makao ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague, Uholanzi, 2005
ICJ/Jeroen Bouman
Muonekano wa Jumba la Amani, makao ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague, Uholanzi, 2005

Mwelekeo unaotakiwa 

Katibu Mkuu amesema mifano yote hiyo inaonesha kuwa uzingatiaji wa sheria ni muhimu hivi sasa kuliko wakati wowote ule. Nchi zote zina wajibu wa kuzingatia kila wakati. 

Utawala wa sheria ni msingi wa juhudi za Umoja wa Mataifa za kusaka majawabu ya amani katika mizozo yote, majanga na mambo mengine mengi na kusaidia watu walio hatarini zaidi na jamii nyinginezo duniani kote. 

Guterres amesema kutokomeza ukwepaji sheria ni jambo la msingi na hilo linafanyika kupitia Mahakama ya Kimataifa ya haki, ICJ, Baraza la Umoja wa Mataifa la  haki za binadamu, kamisheni za kusaka ukweli na mifumo ya Umoja wa Mataifa ya kuendeleza na kusongesha utawala wa kisheria. 

“ICJ yenye majukumu yake ya kipekee, ina nafasi muhimu. Natambua umuhimu wa kukubali mamlaka ya Mahakama hii kushughulikia masuala kwenye eneo na hivyo natoa wito kwa nchi wanachama kufanya hivyo bila kuacha jambo lolote. Wajumbe wa Baraza la Usalama wana wajibu hapa na wachukue dhima ongozi,” amesema Katibu Mkuu. 

Utawala sheria kupitia kusaidia manusura 

Katibu Mkuu amesema utawala wa sheria pia unaimarishwa kwa kusaidia manusura na waathirika na kuwapatia fursa ya kupata haki yao pamoja na fidia. Amesema Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC nayo hapa ina nafasi yake ili kufikisha wakiukaji wa haki mbele ya sheria. 

Mfuko wa kusaidia manusura wa ukatili na unyanyasaji wa kingono umesaidia wanawake huko DR Congo kujifunza kilimo cha uyoga (Oktoba 2018)
MONUSCO/Michael Ali
Mfuko wa kusaidia manusura wa ukatili na unyanyasaji wa kingono umesaidia wanawake huko DR Congo kujifunza kilimo cha uyoga (Oktoba 2018)

Nchi wanachama ziimarishe taasisi za UN 

Guterres amegeukia pia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa akisema nazo zina wajibu wao kwenye kuimarisha utawala wa kisheria, “kwa kuimarisha taasisi za Umoja wa Mataifa kwa lengo la kusongesha utawala wa sheria.” 

Mosi, ametaka zifanye hivyo kwa kuzingatia Chata ya Umoja wa Mataifa na Tamko la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu. 

Pili, “nazisihi zitumie utawala wa sheria kama mbinu za kuzuia uvunjifu wa sheria, kupitia mashauriano na majadialino.” 

Tatu, ziimarishe utawala wa sheria kama kiwezeshaji cha kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs au Ajenda 2030.