Mbegu za mimea zapandwa nje na ndani ya kituo cha anga za juu
Mbegu za mimea zapandwa nje na ndani ya kituo cha anga za juu
Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA limesema mbegu za mazao zilizopelekwa kituo cha anga za juu mwezi Novemba mwaka jana tayari zimepandwa eneo la ndani na nje ya kituo hicho na hivyo zinapata miali kamilifu ya anga za juu pamoja na viwango vya juu zaidi vya joto kwenye eneo hilo.
Kwa mujibu wa chapisho la IAEA yenye makao yake makuu, Vienna, Austria, mbegu hizo zilipelekwa na shirika hilo pamoja na lile la chakula na kilimo, FAO kwa lengo la kuchunguza athari za miali ya anga za juu kwenye mbegu kama sehemu ya utafiti wa kuimarisha aina mbalimbali za mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuongeza uhakika wa chakula.
“Lengo ni kubaini iwapo mazingira magumu ya hali ya hewa anga za juu kama vile joto kali kupindukia, miale kutoka anga za juu vinaweza kuchochea mabadiliko kwenye mbegu na hatimaye mabadiliko hayo ya hali ya hewa yanaweza kusaidia mimea kuwa na mnepo zaidi pindi inapokabiliwa na changamoto za ukuaji au kumea duniani,” imesema taarifa hiyo.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IAEA na pia Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Nyuklia na Matumizi yake, Najat Mokhtar amesema wana wajibu wa kuchunguza teknolojia za kinyuklia ambazo zinaweza kuleta tofauti chanya kwa afya ya binadamu na chakula anachokula.
“Jinsi dunia inahaha kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji kuongeza kasi ya tafiti za kuboresha mimea na kupata majawabu yanayotesheleza na fanisi,” amesema Bi. Mokthar.
Mbegu zilizopelekwa anga za juu ni pamoja na mtama.