Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada ya kibinadamu kuendelea kuingia Syria kupitia mpaka wa Bab al-Hawa

Familia moja inayoishi katika makazi yasiyo rasmi katika mji wa Raqqa, kaskazini mashariki mwa Syria.
© UNICEF/Delil Souleiman
Familia moja inayoishi katika makazi yasiyo rasmi katika mji wa Raqqa, kaskazini mashariki mwa Syria.

Misaada ya kibinadamu kuendelea kuingia Syria kupitia mpaka wa Bab al-Hawa

Msaada wa Kibinadamu

Malori yanayosafirisha kutoka Uturuki shehena za vyakula, dawa na misaada mingine muhimu inayohitajika nchini kaskazini-magharibi mwa Syria, yataendelea kutoa huduma hiyo baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza muda wa mpango huo. 

Azimio la awali lilikuwa limalizike kesho Jumanne na hivyo kulikuwa na wito wa kimataifa wa kutaka azimio hilo liongezwe muda bila kuchelewa kutokana na mahitaji. 

Punde baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alitoa taarifa kupitia msemaji wake akieleza kutambua uamuzi huo na kuelezea kuwa operesheni za kibinadamu ni hatua muhimu kwa watu milioni 4.1 kwenye eneo hilo la Syria. 

Azimio hilo namba 2672 linafanikisha usafirishaji wa bidhaa za misaada ya kibinadamu kupitia mpaka wa Bab al-Hawa, mpango ambao ulianza takribani miaka 9 iliyopita. 

Kupanua wigo wa kufikisha usaidizi wa kibinadamu 

“Uamuzi wa kuthibitisha kuongeza kwa miezi sita zaidi umekuja wakati mahitaji ya kibinadamu yamefikia viwango vya juu zaidi tangu mzozo nchini Syria uanze mwaka 2011, wakati ambapo pia wananchi wa Syria wanakabiliwa na majira baridi kali pamoja na mlipuko wa kipindupindu,” imesema taarifa hiyo ya Katibu Mkuu. 

Guterres amesema suala la kuwezesha misaada ya kibinadamu kufikia maeneo yote nchini Syria, ikiwemo kupitia mipakani na maeneo yenye mizozo lazima lipanuliwe na shughuli za kibinadamu wigo wake nao uongezwe kupitia uwekezaji kwenye miradi ya mapema ya kujikwamua. 

Kufikia wasyria wenye mahitaji 

Uswisi na Brazili ziliwasilisha rasimu ya azimio hilo, zikiendeleza kazi za watangulizi walioandika maazimio ya awali ambao ni Ireland na Norway ambao ziliwasilisha azimio  mwezi Julai mwaka jana, azimio ambao liliidhinisha operesheni kwa miezi sita au hadi tarehe  10 mwezi Januari mwaka 2023. Azimio hilo lilieleza kuwa kuongezwa muda lazima kufanyike kupitia azimio lingine. 

Mwakilishi wa kudumu wa Uswisi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Pascale Baeriswyl akizungumza  baada ya kupitishwa kwa azimio amesema “azimio hili linatoa fursa kwa wahudumu wa kibinadamu hasa Umoja wa Mataifa kuendelea kufikia wale wenye uhitaji zaidi kwa njia inayoratibika na kwa uangalifu.” 

Balozi Baeriswyl  amesema ufikishaji misaada bila kikwazo chochote ni muhimu na ametoa wito kwa pande zote kufanikisha ufikishaji wa misaada hiyo.