Mradi unaotekelezwa na UNICEF na wadau nchini Rwanda wapunguza vifo vya watoto wachanga

Muuguzi akimlisha mtoto mchanga chakula kwa njia ya mpira kwenye wadi ya watoto wachanga katika hospitali ya Muhima iliyoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
© UNICEF/Veronica Houser
Muuguzi akimlisha mtoto mchanga chakula kwa njia ya mpira kwenye wadi ya watoto wachanga katika hospitali ya Muhima iliyoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Mradi unaotekelezwa na UNICEF na wadau nchini Rwanda wapunguza vifo vya watoto wachanga

Afya

Nchini Rwanda Umoja wa Mataifa unashirikiana na serikali kuimairisha huduma za uzazi ili hatimaye kuhakikisha kila uzazi unakuwa salama si tu kwa mama bali pia mtoto anayezaliwa. Kupitia mradi uliofadhiliwa na TAKEDA, kampuni hii ya utafiti na dawa duniani, Rwanda imeweza kuimarisha huduma kwenye hospitali na vituo vya afya.

Mradi umeanza lini?

Mradi huo wa ubia ulianza mwaka 2017. Wakati huo, Rwanda ndio ilikuwa imekamilisha malengo ya milenia, ikimaanisha baadhi ya malengo yalitimizwa, lakini kulikuwa na kusuasua katika baadhi ya maeneo mengine.

Mathalani hadi leo vifo vya watoto wachanga ni 20 katika kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai na theluthi moja ya watoto nchini Rwanda wamedumaa. Sasa jawabu ni mradi wa kusaidia watoto kabla tu na baada ya kuzaliwa, au RPIP. Mradi huu ni ubia baina ya Wizara ya Afya ya Rwanda, Chama cha madaktari wa watoto Rwanda, na Chuo cha madaktari watoto na afya ya watoto nchini Uingereza.

Kituo cha afya cha Muhima kilichoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
Picha: Screenshot_UNICEF video
Kituo cha afya cha Muhima kilichoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Idadi ya vituo vya afya na hospitali zilizonufaika

Vituo 85 na hospitali 19 zimefikiwa na mradi huu ambapo ufuatiliaji unaanza kwa mjamzito hadi mtoto mchanga anapozaliwa. Hospitali ya Muhima kwenye mji mkuu Kigali ni miongoni mwa wanufaika.

Julia Battle, Mkuu wa kitengo cha afya na lishe UNICEF nchini Rwanda  amefika hospitalini Muhima na anasema “kwenye mradi tumelenga mwendelezo mzima wa huduma kwa mama na watoto wachanga. Ikimaanisha tangu mapokezi wanapofika hospitali, wanapokuwa kwenye uchungu, wanapoingia chumba cha kujifungua, baada ya kujifungua, na pia watoto wachanga waliozaliwa na huduma kwa watoto wachanga na wale wagonjwa kwenye wodi ya watoto wachanga. Ama hakika tumeshuhudia mabadiliko makubwa."

Sasa vifo vya watoto wachanga kwa watoto waliolazwa kwenye wodi ya watoto wachanga vimepungua kwa zaidi ya asilimia 30.

Josette Umucyo, mkunga na mwalimu wa mradi wa RPIP anasema awali eneo la mapokezi lilikuwa ni mlundikano wa wajawazito na kwamba daktari na mkunga wote walikaa pamoja kwenye chumba kimoja. Na ilichukua muda mrefu kubaini matatizo yanayowakabili na kuwatenganisha. Walisubiri kwa saa mbili hivi. “

Baada ya kutekeleza mradi, sasa daktari muda wote yuko wakati wote hapo na mchakato wa kubaini tatizo la mgonjwa na kuwapanga kwa mujibu wa mahitaji yao na uamuzi vinafanyika kwa haraka, jambo ambalo linatusaidia kutoa huduma bora kwa kwa mama mjamzito.

Mama akiwa na mtoto wake mchanga kwenye wadi ya watoto wachanga katika hospitali ya Muhima iliyoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
© UNICEF/UN0308931/N
Mama akiwa na mtoto wake mchanga kwenye wadi ya watoto wachanga katika hospitali ya Muhima iliyoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Wodi ya wajawazito

Katika wodi ya wajawazito kuna ubao ulioandikwa taarifa za kila mjamzito na kile cha kufuatilia hali inayowezesha mkunga kufuatilia wanawake wote kwa ufanisi zaidi.

Sasa vifo vya watoto wachanga kwa watoto waliolazwa kwenye wodi ya watoto wachanga vimepungua kwa zaidi ya asilimia 30- Julia Battle, Mkuu wa kitengo cha afya na lishe UNICEF, Rwanda

Josette anasema zamani huu haukuwepo! Yaani tuliwafuatilia bila mpango wowote ule, lakini sasa tuna ubao na jedwali ambalo tunaweza kufuatilia mwenendo wa uchungu wa mjamzito.

Chumba cha kujifungulia

Kutoka wodi ya wajawazito wanaelekea eneo la kujifungulia ambako kuna vyumba viwili kuna vitanda vine na vitanda viwili vya watoto vya kuwapatia joto. Na zaidi ya yote wana makasha ya dharura ambapo moja lina vifaa vya PPH vitumikavyo mjamzito anapovuja damu nyingi, na lingine ni Preeclampia, pale mjamzito anapokuwa na shinikizo la damu. Hayo ni magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo vya wajawazito.

Chumba cha kujifungulia kina vifaa vya dharura

Akifafanua maboresha ya chumba hicho, Josette anasema “zamani ilikuwa mtoto akizaliwa tu tukiona hayuko vizuri tunamchukua na kukimbia. Lakini sasa kwa sababu tuna mafunzo, tunamchukua mtoto, tunamsafisha na tunamweka kwenye kifaa cha joto na kupumua na kisha tunamwezesha arejee hali ya kawaida. Baada ya hapo tunapatia taarifa wahudumu wa wodi ya watoto wachanga wajiandae kwa mtoto aliyezaliwa.”

Mtoto  mchanga akiwa wadi ya watoto  katika hospitali ya Muhima iliyoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
© UNICEF/UN0308918/Houser
Mtoto mchanga akiwa wadi ya watoto katika hospitali ya Muhima iliyoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Je wodi ya watoto wa wachanga ina nini?

Usafi unaanzia mlango ambapo wananawa mikono na kuvaa viatu visafi na mwenyeji wa Julia hapa ni Valentine Mushikazi, muuguzi wa watoto wachanga. Kitengo kina vitanda vya watoto wachanga na mazingira ni masafi.

Valentine akilinganisha zamani na sasa anasema, “zamani tulichanganya watoto waliozaliwa nyumbani na waliozaliwa hapa hospitalini.”

Kwa hivi sasa watoto waliozaliwa nyumbani wako upande mmoja na waliozaliwa hospitali wako chumba kingine.

Halikadhalika kuna vifaa vya kusaidia watoto kupumua, jedwali la kuonesha ratiba ya chakula ya mtoto anayelishwa kwa mirija na pia chumba cha watoto njiti ambako mama anapatiwa fursa ya kubeba mtoto wake kwa njia ya kangaroo.