Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sababu 8 za matumaini kwa mwaka mpya 2023

Pichani, Isatou, Mariama na Fatoumatta hawalazimiki tena kutoenda shule wakati wa hedhi baada ya UNFPA kusaidia uzalishaji na mgao wa bure wa taulo za kike zitumikazo tena na tena wa ajili ya shule ikiwemo shule yao ya viziwi mjini Banjul, Gambia.
UNFPA Gambia
Pichani, Isatou, Mariama na Fatoumatta hawalazimiki tena kutoenda shule wakati wa hedhi baada ya UNFPA kusaidia uzalishaji na mgao wa bure wa taulo za kike zitumikazo tena na tena wa ajili ya shule ikiwemo shule yao ya viziwi mjini Banjul, Gambia.

Sababu 8 za matumaini kwa mwaka mpya 2023

Masuala ya UM

 “Kama kuna vifo, hiyo ndio itakuwa habari ya juu,” ni msemo wa siku nyingi katika vyumba vya habari, ukiangazia vile ambavyo vyombo vya habari vinapatia kipaumbele habari za majanga. Ukitazama nyuma mwaka 2022, uligubikwa na vichwa vya habari vyenye kiza, matangazo ya kutia hofu na tabiri chungu za siku zijazo. Si kila mtu ameweza kuona maendeleo yaliyopatikana, ikiwemo kusongesha ubunifu, haki, uwiano na usawa duniani kote.

Ni kwa kuzingatia hilo, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA kupitia chapisho kwenye wavuti wake, limeona ni bora kukupatia angalau mambo manane, ambayo ni sababu tosha za matumaini kwa mwaka mpya 2023 licha vyombo vya habari kugubikwa na taarifa za machungu na kukatisha tamaa.

Mariel mwenye umri wa miaka 30 (kushoto) akimtambulisha mtoto wake kwa Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem wakati wa ziara yake Ufilipino. Mariel aliweza kujifungua salama wakati wa kimbunga kutokana na mradi wa UNFPA wa kupeleka gari lenye h…
UNFPA Ufilipino/Ezra Acayan
Mariel mwenye umri wa miaka 30 (kushoto) akimtambulisha mtoto wake kwa Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem wakati wa ziara yake Ufilipino. Mariel aliweza kujifungua salama wakati wa kimbunga kutokana na mradi wa UNFPA wa kupeleka gari lenye huduma za kujifungua kwenye maeneo yenye majanga.

1. Mwelekeo wa dunia wa kusongesha mbele haki za afya ya uzazi

Ni dhahiri kuwa kwenye kuimarisha haki na upatikanaji wa huduma za afya za uzazi kuna changamoto, na bila shaka janga la COVID-19 lilirudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana kwa kuongeza mzigo kwenye mifumo ya afya, kuvuruga mnyororo wa utoaji huduma na kupunguza fursa ya kupata taarifa na huduma za afya ya uzazi. Changamoto hizi zinatia shaka lakini kwa ujumla mwelekeo unatia matumaini.

Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu duniani mwaka 2022 iliyotolewa na UNFPA inataka suala la mimba zisizopangwa litambuliwe kuwa ni janga la kimataifa. Tayari viongozi wa kisiasa na kiraia wameitikia wito, wakitambua janga na suala lisilokubalika kuwa takribani nusu ya ujauzito wote duniani haujapangwa.

Nchi nyingi zaidi zinapitisha sheria kutetea na kulinda haki za afya ya uzazi. “Tunatambua kuhusu maendeleo haya kwa sababu kwa mara ya kwanza kidunia tunaweza kupima suala hilo kwa kutumia vigezo vya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs,” amesema Natalia Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA.

UNFPA ilifanya utafiti katika nchi 153 zenye asilimia takribani 90 ya watu wote duniani na kubaini kuwa asilimia 76 ya nchi hizo zinasheria za kulinda na kutetea haki ya masuala ya ngono na uzazi.

Wanaharakati vijana wakitoa ujumbe wao kwa washiriki wa COP27 wakidai fidia kwa hasara na uharibifu kwa nchi maskini kutokana na jinsi zinaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Kiara Worth
Wanaharakati vijana wakitoa ujumbe wao kwa washiriki wa COP27 wakidai fidia kwa hasara na uharibifu kwa nchi maskini kutokana na jinsi zinaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

2. Kauli za usawa na kusongesha haki zinapazwa zaidi

Mwaka uliopita uligubikwa na ukosefu wa uhakika wa chakula, janga la bei ya nishati ya mafuta na majanga mengine mengi ya dharura ambamo kwayo waathirika wengi walikuwa wakazi wa nchi maskini zaidi.

Inaweza kuwa ilipita bila kubainika wakati huo, wito wa kubadili mifumo ya haki – kubadili makosa ya kihistoria, kutoa wito kwa mifumo kandamizi kurekebishwa na kupatia kipaumbele wale walioachwa nyuma zaidi – kauli hizi zilitumika zaidi kwenye utatuzi wa changamoto za kimataifa.

Mathalani makubaliano ya kihistoria mwezi Novemba wakati wa COP27 huko Sharm el- Sheik nchini Misri ya kutaka nchi zilizo hatarini zaidi zilipwe fidia kwa hasara na uharibifu kwa kutambua zinavyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi, janga ambalo mchango wao ni kidogo mno.

3. Wanawake wanataka usawa kwenye majukwaa ya kidijitali

Ni ukweli wa kusikitisha kwenye dunia ya kwamba majukwaa ya kidijitali si salama kwa wanawake na wasichana. Matukio 8 kati ya 10 ya ukatili yamechochewa na teknolojia ikiwemo kulaghaiwa kwa wasichana na wanawake kutuma picha za utupu kupitia mitandao. Lakini mwaka 2022, wanawake na wasichana wengi waliokumbwa na ukatili wa aina hiyo walisimama kidete na kusema sasa inatosha na UNFPA ikashikamana nao.

Kwa miaka miwili iliyopita, kampeni ya UNFPA ya Haki ya Mwili ambayo imeshinda tuzo imekuwa inatoa wito kwa ulinzi zaidi kwa wanawake na wasichana na jamii zilizo pembezoni dhidi ya ukatili wa kidijitali. Wanatumia alama kama vile @Hakimiliki @Hakiyamwili kuonesha kuwa mwili ni mali ya msichana au mwanamke mwenyewe.

Tangu uzinduzi wa kampeni hiyo mwaka 2021, zaidi ya watu 30,000 wametia saini barua ya UNFPA ya  kutaka watunga sera na kampuni za teknolojia zitambua ghasia au ukatili wa kimtandao pale unapofanyika na juhudi za kutokomeza. Kuungwa mkono kwa kampeni hii ni ishara tosha ya mshikamano na manusura, mshikamano ambao hautakoma hadi wasichana na wanawake wajihisi salama wanapokuwa mtandaoni na nje ya mtandao.

Manusura wa ukatili wa kingono Kadijatu Grace akisimulia kwa uchungu yaliyomfika wakati wa hafla ya uzinduzi wa maonesho ya "Ulikuwa umevaa nini?" kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani
Spotlight Iniative
Manusura wa ukatili wa kingono Kadijatu Grace akisimulia kwa uchungu yaliyomfika wakati wa hafla ya uzinduzi wa maonesho ya "Ulikuwa umevaa nini?" kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani

4. Ukatili wa kingono kwenye mizozo walaaniwa waziwazi

Wakati wa siku ya kimataifa ya kutokomeza aina zote za ukatili wa kingono kwenye mizozo, Dkt. Kanem, Mkuu wa UNFPA alitambua madhara haribifu ya ukatili wa kingono akisema unaharibu mwili, unaanza makovu kwenye fikra na hata unaua. Unanyamazisha na kuaibisha wanawake na kupanda mbegu ya uoga na ukosefu wa usalama.

Mwaka jana wanwake na wasichana walionasa katika dharura za kibinadamu duniani kote walikabiliwa na mwelekeo wa kutisha: hatari ya jamii zao kuona ukatili wa kingono kuwa jambo la kawaida kwenye mizozo ijapokuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu na uhalifu kwa mujibu wa sheria za kimataifa na lazima ukome.

Miradi ya kiutu ya UNFPA duniani kote imesaidia maelfu ya vituo ya afya kutoa huduma mahsusi kwa manusura na waathirika wa vitendo vya ubakari. Shirika hili linaendeleza kazi yake ya kupaza sauti za watu hao na kusaka haki. Manusura wanatambua kuwa ukatili wa kingono unapoenea #Sijambolakawaida, na ni wakati wa dunia kuhakikisha unatokomezwa.

Katika eneo la Tambakunda mfanyakazi wa IOM anamueleza chifu wa kijiji mchakato wa kuelezea mahitaji ya watu wenye matatizo ya afya ya akili wanaohitaji huduma zaidi za afya
IOM/Robert Kovacs
Katika eneo la Tambakunda mfanyakazi wa IOM anamueleza chifu wa kijiji mchakato wa kuelezea mahitaji ya watu wenye matatizo ya afya ya akili wanaohitaji huduma zaidi za afya

5. Wanawaharakati wanaleta mabadiliko na kutengua vitendo hatarishi

Kutekeleza matendo mapya na kubadili mila na desturi zilizozoeleka miaka nenda miaka rudi kunahitaji kujizatiti, lakini duniani kote watu wamekuwa wakianzisha mbinu mpya za kuchagiza mchakato huo kuanzia kusambaza vifaa vya huduma za kuokoa maisha kwa kutumia ndege zisizo na rubani, hadi magari yenye huduma za kujifungua ambazo hufuata wanawake katika maeneo yenye mizozo ili wajifungue salama. Bila kusahau harakati za kuhakikisha wanawake na wasichana wanakuwa salama nje na ndani ya majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Nchini Laos na Maldives, UNFPA inatumia mtandao wa Tik Tok kufundisha wakunga na kuibua mjadala kuhusu mamlaka ya mwanamke kwenye mwili wake ilhali Bangladesh apu moja inatumika kusambaza vifaa vya hedhi.

Katika mabara yote ubunivu na uvumbuzi unaongoza njia: kampeni kwa ajili ya mabadiliko, kuhoji imani na mila haribifu na kusaidia wanawake na wasichana kujilinda na kulinda wengine.

6. Afya ya akili sasa ni kipaumbele duniani

Dharura nyingi zilizogubika dunia mwaka jana ziliongeza kiwewe na msongo wa mawazo kwa wakazi wa dunia mathalani wakati wa janga la COVID-19 na baada ya mlipuko kupungua au kumalizika katika maeneo mengine.

Hali ilichochea ongezeko la matukio ya magonjwa ya afya ya akili.

Vijana na wanawake wanaathirika zaidi na afya ya akili, iwe ni kutokana na ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, ukeketaji, fistula, ujauzito usiotakiwa au ghasia za mtandaoni.

Katika miaka hii ya tafrani, UNFPA imeimarisha usaidizi wa kisaikolojia, kuelekeza manusura mahali pa kupata huduma za kisheria au kiafya, na kuongeza maeneo salama na rafiki kwa manusura.

UNFPA inasaidia wasichana walioathiriwa na ukatili wa kingono, ndoa za utotoni, wanawake walioshambuliwa kwa kupaza sauti za kudai au kutetea haki, au kusaka ajira, na mamilioni ya watu wanaobaguliwa kwa sababu ya walikozaliwa au ulemavu.

Duniani kote hali ya afya ya akili inaonekana kuwa ni janga; lakini ni janga ambalo UNFPA na kikosi chake kilicho mstari wa mbele, yaani wauguzi, madaktari, wakunga na wafanyakazi wa kibinadamu wameazimia kusalia imaria na kutoa huduma.

Janga la Corona limeathiri namna watu wanapitia hedhi salama.
©UNICEF/UNI328066/Nzenze
Janga la Corona limeathiri namna watu wanapitia hedhi salama.

7. Hedhi inatambuliwa kuwa suala la haki ya binadamu

Katika muongo mmoja uliopita, maendeleo makubwa yamepatikana kwenye kutambuliwa kwa hedhi kuwa si tu suala la afya, usafi na utu bali pia suala la usawa wa jinsia na haki za binadamu. Wachechemuzi wamebadili mawazo kuhusu hedhi katika ngazi mbalimbali ikiwemo kwenye Umoja wa Mataifa ambako Baraza la haki za binadamu lilipitisha azimio linalokemea unyanyapaa dhidi ya hedhi, uaibishaji na kutengwa kwa walio kwenye hedhi na kutangaza kuwa vitendo hivyo ni kinyume na haki za binadamu.

Sasa watunga será wa nchi wanabeba hoja hii ambako baadhi ya nchi zimetia saini sheria ya kuhakikisha bidhaa za hedhi zinatolewa bure. Nchi nyingin zaidi zinajadili suala la mzigo wa kifedha utokanao na bidhaa za hedhi pamoja na kuangazia umuhimu wa maeneo ya kazi na shule kutenga mazingira ya kuhudumia walio kwenye hedhi.

8. Idadi ya watu duniani yafikia bilioni 8

Tarehe 15 mwezi Novemba mwaka 2022, idadi ya watu duniani ilifikia bilioni 8. Mafanikio haya ya kihistoria yanaakisi dunia ambamo kwayo wanawake wengi zaidi wanajifungua salama, watoto wengi zaidi wanaepushwa na vifo vya utotoni, na watu wengi zaidi wanaishi muda mrefu na maisha yenye afya.

“Ni ushuhuda wa maendeleo ya miongo kadhaa kwenye afya ya umma na kupungua kwa umaskini, na ni simulizi ya mnepo zaidi na ufanisi zaidi wa mifumo ya afya,” amesema Dkt. Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA katika hotuba yake siku idadi ya watu ilipofikia bilioni 8.

Bila shaka mafanikio hayo lazima yalindwe kwa kuwa changamoto kama vile janga la COVID-19, mizozo, mabadiliko ya tabianchi yanatishia kurudisha nyuma.

UNFPA inasema, “kuna watu bilioni 8 sasa duniani, hivyo kuna sababu bilioni 8 za kuwa na matumaini kuwa kwa pamoja tunaweza kujenga dunia yoyote ile yenye jumuishi zaidi, yenye haki na mustakabli endelevu."