Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2023 ni mwaka wa mtama duniani:FAO

Wanawake wakiwa wamebeba vikapu vya mtama aina ya lulu nchini Malai baada ya kuvuna
ICRISAT/AS Rao
Wanawake wakiwa wamebeba vikapu vya mtama aina ya lulu nchini Malai baada ya kuvuna

Mwaka 2023 ni mwaka wa mtama duniani:FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mwaka 2023 ni mwaka wa mtama, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO mwaka huu itakuwa ni fursa ya kuongeza ufahamu na kuelekeza umakini wa kisera kwa manufaa ya lishe na afya ya mtama na jinsi ulivyo endelevu katika kilimo chini ya hali mbaya na inayobadilika ya hewa.  

FAO inasema mwaka huu pia utachagiza uzalishaji endelevu wa mtama, huku ukiangazia uwezo wa zao hilo wa kutoa fursa mpya za soko endelevu kwa wazalishaji na watumiaji. 

FAO imeongeza kuwa “Huku mifumo ya kimataifa ya chakula cha kilimo ikikabiliwa na changamoto za kulisha idadi ya watu inayoongezeka duniani kote, nafaka zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi kama mtama hutoa chaguo la bei nafuu na lenye lishe bora, na juhudi zinahitaji kuongezwa ili kukuza kilimo cha zao hilo.” 

 Aina za mtama 

Katika ujumbe maalum wa mwaka wa kimataifa wa mtama FAO imesema kuna aina mbalimbali za mtama zikijumuisha lulu, seredo, mkia wa mbweha, uwele, ulezi, serena, macia, teff, pamoja na fonio au mtama mkubwa.  

Mtama ni chanzo muhimu cha lishe kwa mamilioni ya watu katika maeneo ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia.  

Na zao hilo limejikita sana katika tamaduni za watu asilia na kusaidia kuhakikisha uhakika wa chakula katika maeneo ambayo yana umuhimu wa kitamaduni. 

Mtama aina ya ulezi kabla na baada ya kukobolewa
UN India/Anadi Charan Behera of Studio Priya, Bhubaneswar
Mtama aina ya ulezi kabla na baada ya kukobolewa

Mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema "Mtama ni mazao ya ajabu ya kutoka kwa mababu zetu yenye thamani ya juu ya lishe. Mtama unaweza kuwa na jukumu muhimu na kuchangia katika juhudi zetu za pamoja za kuwawezesha wakulima wadogo, kufikia malengo ya maendeleo endelevu, kuondoa njaa, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kukuza bioanuwai, na kubadilisha mifumo ya chakula ya kilimo.” 

Mgurugenzi huyo mkuu ameongeza kuwa uzalishaji mkubwa wa mtama unaweza kusaidia maisha ya wakulima wadogo na unaweza kutoa ajira zenye staha kwa wanawake na vijana.  

Mapato yanayopatikana yanaweza kusaidia kukuza uchumi na pia zao hilo linauwezekano wa kuwa mbadala wa nafaka yenye lishe, na hatari zinazohusiana na changamoto za uzalishaji zinaweza kupunguzwa. 

“Mwaka huu wa kimataifa wa mtama ni ukumbusho wa umuhimu wa zao hili. Na inatoa fursa ya kipekee ya kuongeza ufahamu wa zao hilo” 

Mwaka 2023 kuwa mwaka wa mtama duniani ulipitishwa na kutangazwa katika kikao cha 75 cha Baraza Kuu mwezi Machi 2021 na FAO ndio inashoshika usukani wa mwaka huu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali