Nilichoka maisha ya kuwa ngariba, hata jela nilifika: Paulina Robi
Nilichoka maisha ya kuwa ngariba, hata jela nilifika: Paulina Robi
Kwa muda sasa, Umoja wa Mataifa kupitia mashirika na wadau wengine, wameendelea kutafuta namna nzuri ya kutokomeza mila ya ukeketaji ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka elfu moja katika jamii mbalimbali duniani.
Hatua kadhaa zimepigwa katika mapambano haya na Umoja wa Mataifa unaamini kwamba mila hii iliyopitwa na wakati inaweza kutokomezwa katika kizazi kimoja ikiwezekana kufikia mwaka 2030.
Moja ya viashiria vya kufanikiwa kutokomeza ukeketaji ni kuona kuwa baadhi ya waliokuwa wanaushikilia utamaduni huu wanaanza kuelewa kuwa ni utamaduni wenye madhara na hivyo wanaanza kuiacha tabia hiyo ya kuwakeketa watoto wa kike katika jamii zao.
Ngariba Paulina Robi
Nchini Kenya, Paulina Robi aliifanya kazi ya kuwakeketa wasichana kila msimu ulipowadia kama mila zilivyodai. Kwa mujibu wake, mikono yake ina mengi ya kuelezea laiti ingeweza kusema kwani ilitumika kwa muda mrefu kuwakata wasichana. Hata hivyo Paulina Robi hatimaye busara zake zilimsukuma kuitii amri ya serikali ya kupiga marufuku ukeketaji wa wari.
Mwandishi wa habari, Thelma Mwadzaya alipokutana na mwanamke huyu aliyeacha ungariba mjini Kehancha alisisitiza kuwa sasa anajihusisha na shughuli ndogo ndogo ili aweze kupata mkate wa siku na ameacha ukeketaji. Alinisimulia maisha yake akisema, “niliacha ukeketaji kwani nilikuwa nasumbuliwa kila wakati. Polisi wakiingia nakamatwa na kupelekwa kituoni ninakozuiliwa.Hata jela nilifungwa. Nilichoka na maisha hayo na nikataka niweze kuwa na familia yangu kila wakati badala ya kusumbuliwa.”
Wakati wa likizo ni wakati wa machungu
Kulingana na mila na tamaduni za Wakurya, wari hukeketwa pindi wanapovunja ungo. Aghalabu hilo hufanyika katika msimu wa likizo ndefu ya shule mwishoni mwa mwaka. Kwa ujumla, ukeketaji umekuwa ukipungua katika miongo mitatu iliyopita zinaelezea takwimu za shirika la Umoja wa mataifa la watoto-UNICEF na UNFPA yaliyozindua mpango wa pamoja mwaka 2020 wa kuutokomeza ukeketaji kwa ushirikiano na serikali na mashirika ya kijamii.
Katika mataifa 31 kote ulimwenguni, utamaduni huu umewekwa pembeni na msichana mmoja kati ya watatu walio na umri wa miaka kati ya 15 na 19 wamekeketwa. Hayo ni mafanikio kwani katika miaka ya 90 msichana mmoja kati ya wawili alikeketwa. Hata hivyo kasi ya kupambana na ukeketaji imechukua sura mpya na wanaume sasa wanashirikishwa kwa karibu zaidi. Kwa sasa wanaume nao pia wako mstari wa mbele kuupiga vita ukeketaji baada ya serikali kuupiga marufuku. Simon Nchama ni mwenyekiti wa baraza la wazee wa Kikuria na kwa mtazamo wao elimu imewasaidia na anasema, “tumefundishwa kuhusu madhara ya tohara ya kike na tumekuja kuona kuwa mwanamke anateseka sana.Madaktari wametuonesha kinachotokea kwenye mwili wa mwanamke anapokeketwa hasa wakati wa kujifungua au kwenye mahusiano na mume wake.Sasa tunawahimiza wanaume kutowaruhusu mabinti zao kukeketwa.”
Mwanamke 1 kati ya 5 Kenya amekeketwa
Tathmini zinaashiria kuwa ,mwanamke mmoja kati ya watano walio na umri wa kutokea miaka 15 hadi 49 wamekeketwa nchini Kenya. Ukeketaji ni shughuli inayoondoa sehemu au kufyeka sehemu za siri za mwanamke na madhara yake kiafya yanaweza kusababisha maafa. Margaret Nyamataga ni mama wa watoto kadhaa na alifanyiwa tohara ya kike iliyomuacha na makovu ya kimwili na kwenye nafsi yake. Akiwa na masikitiko anasimulia akisema “nilisikia uchungu sana. Kitendo kiliniathiri sana mithili ya kuwa sikutaka kuwa na mume wangu. Kila aliponijia niliona kama nateswa.Sikutaka mahusiano yoyote na mume wangu na ilipotokea sikutaka iwe safari ndefu. Hilo lilizua mivutano kwenye maisha yangu kwani hakuwa akinielewa kila nilipokataa tendo la ndoa. Si sawa kwa mwanamke kuishi kwenye mazingira ya malumbano nyumbani.”
Athari za ukeketaji kwa wanawake na wasichana
Utamaduni wa kuwakeketa wasichana unafanyika katika mataifa yasiyopungua 27 barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati. Aghalabu ngariba hutumia mbinu za kiasili na kuhatarisha maisha ya wari kwani hawafuatilii kanuni za usafi. Wakati mwengine, wasichana wanaweza kuvuja damu hadi kufa au kupata maambukizi yanayaoua. Kadhalika matatizo kama fistula au mengine yanaweza kutokea wakati wa kujifungua linatahadharisha shirika la Umoja wa Mataifa la afya,WHO.
Margaret Nyamataga anakiri kuwa msichana hupitia kipindi kigumu anapokeketwa na kwake yeye, “niliteseka kila wakati nilipooshwa.Walinifyeka sehemu yote ya siri nikasalia na maumivu tu.Sikuweza hata kulala kwa ubavu wangu.Nililala chali muda wote kabla ya kupona ndipo kidonda kisishikane na ngozi kurejea pamoja.Alikuwako bibi mmoja aliyekuja kutazama kidonda na kukiosha kila siku na hilo liliniacha na uchungu mwingi.Sioni haja ya msichana kukeketwa.Unaweza kuvuja damu hadi kufa au kuambukizwa magonjwa hatari na hakuna nafasi ya kupelekwa hospitali kwa matibabu.”
Ukeketaji ni haramu
Mwaka 2011 serikali ya Kenya ilipiga marufuku na kuharamisha ukeketaji mwaka na adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 3 jela na faini ya dola alfu 2. Mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa waliafikiana kuutokomeza ukeketaji ulimwenguni ifikapo 2030. Changamoto zinashuhudiwa zaidi katika kaunti za jamii za wafugaji kama Mandera na Wajir ambako uhaba wa nyenzo na usalama mbaya ni vikwazo. Paulina Robi aliyeacha kuwa ngariba anaishauri jamii kutilia mkazo masomo kwa wasichana badala ya mila zinazoirejesha jamii nyuma akisema,“masomo ndio muhimu zaidi.Siku hizi hata ukimlazimisha msichana afanyiwe tohara anakuchukulia hatua.Yupo msichana mmoja alimshtaki mama yake mzazi kwa kumtusi kuwa hana akili kwa sababu hajafanyiwa tohara.Mama huyo alifungwa kwa hilo.”
Takwimu za shirika la Umoja wa mataifa la watoto, UNICEF zinaashiria kuwa wasichana na wanawake wasiopungua milioni 200 wamekeketwa. Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linapinga aina zote za ukeketaji kwani hauna manufaa yoyote kiafya badala yake ni madhara ya muda mrefu.