Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Ukosefu wa usalama wafurusha takriban watu 530,000 jimboni Kivu Kaskazini - OCHA

Jamii nyingi zimekimbilia katika eneo la Kanyaruchinya kwa watu waliokimbia makazi yao katika mkoa wa Kivu Kaskazini kufuatia mapigano mashariki mwa DRC.
© UNICEF/Jospin Benekire
Jamii nyingi zimekimbilia katika eneo la Kanyaruchinya kwa watu waliokimbia makazi yao katika mkoa wa Kivu Kaskazini kufuatia mapigano mashariki mwa DRC.

DRC: Ukosefu wa usalama wafurusha takriban watu 530,000 jimboni Kivu Kaskazini - OCHA

Afya

Wakati zaidi ya Wananchi 7,000 raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC wamepata hifadhi katika nchi jirani ya Uganda, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura OCHA imesema takriban watu 521,000 wameyakimbia makazi yao tangu Machi 2022 kutokana na mapigano katika maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo, kaskazini mwa DRC.

Taarifa iliyotolewa leo na OCHA kutoka Geneva Uswisi imesema kuwa “Ongezeko hili la idadi ya watu waliokimbia makazi yao ikilinganishwa na wiki iliyopita (wahamiaji 510,000) linatokana na mapigano kati ya wanajeshi wa Kongo (FRDC) na washirika wao dhidi ya  waasi wa M23 katika eneo la Rutshuru.

Kutokana na kukosekana huko kwa hali ya usalama wanawake wanaokimbia kusaka hifadhi wanawakilisha 51% ya watu waliokimbia makazi na zaidi ya 58% ni watoto chini ya miaka 18.

Nyiranzaba na watoto wake tisa wanapata hifadhi kwenye hema baada ya kukimbia kijiji chake katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.
© UNICEF/Arlette Bashizi
Nyiranzaba na watoto wake tisa wanapata hifadhi kwenye hema baada ya kukimbia kijiji chake katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.

Wakimbizi hao wanaishi wapi?

Wengi wa watu waliokimbia makazi yao wako katika eneo la Nyiragongo (watu 233,000), ambao “zaidi ya 95% wanaishi katika makanisa, shule, viwanja vya michezo na maeneo yaliyoboreshwa, wakati wengine wanaishi na familia zinazowapokea”.

Lakini takwimu hizi zinaweza kubadilika kwani “mapigano yanaendelea kuripotiwa katika eneo la Rutshuru, na kusababisha watu kuzidi kuyakimbia makazi yao kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu”.

Aidha, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF na washirika wake wanaendelea kuhakikisha kuwa wanwatambua, kuwatunza na kuwaunganisha watoto wasio na walezi na waliotenganishwa na wale wanaohusishwa na vikosi vya jeshi na vikundi vyenye silaha.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kati ya tarehe 1 na 16 mwezi Desemba, 2022 angalau watoto 13 wasio na wasindikizaji walitambuliwa katika maeneo ya pamoja na vituo vya Nyiragongo. Pamoja na wimbi hilo kubwa la wakimbizi, watendaji wa kibinadamu wanafanya kazi ili kukidhi mahitaji ya wananchi hao na familia zinazowapokea. Zaidi ya watu 30,000 waliokimbia makazi yao wamepokea msaada wa chakula katika maeneo ya afya ya Kibirizi (Rutshuru) na Kayna (Lubero).

Kwa jumla, takriban watu 170,000 wamepatiwa msaada wa chakula tangu mwisho wa Oktoba 2022 na karibu watu 55,000 waliokimbia makazi wamepokea vifaa muhimu vya nyumbani.

Watoto wa familia za wakimbizi wa ndani wakipika katika kambi iliyoko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Watoto wa familia za wakimbizi wa ndani wakipika katika kambi iliyoko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

Mlipuko wa kipindupindu

Wakati watoa misaada ya kibinadamu wanashughulika kukidhi mahitaji, mwitikio umekuwa mgumu zaidi katika wiki za hivi karibuni na kuzuka kwa janga la kipindupindu. Kulingana na taarifa iliyotolewa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (Redio okapi), zaidi ya wagonjwa 1,000 wa kipindupindu vimetambuliwa katika muda wa wiki moja katika kambi ya Kanyaruchinya huko jimboni Kivu Kaskazini.

“Watu saba tayari wamekufa kutokana na janga hili katika kituo hiki cha wakimbizi” iliongeza Radio Okapi, ikitangaza taarifa iliyotolewa jana Alhamisi na mkuu wa Kitengo cha Afya cha jimbo laKivu Kaskazini, Dkt Janvier Kibuya. Afisa huyu wa afya amesema wanahakikisha wanatoa huduma za matibabu zinazofaa kwa wagonjwa hao, wakiwemo watoto walio chini ya umri wa miaka 5.

Takriban kaya 30,000 zisaidiwa kuondoa uchafu ili kukabiliana na janga la kipindupindu huko Nyiragongo.

Ikumbukwe kwamba hesabu iliyofanywa mnamo Desemba 11 iliripoti wagonjwa 824 wa kipindupindu katika eneo la Nyiragongo, ikiwa ni pamoja na 379 na vifo viwili vilivyorekodiwa katika kipindi cha kati ya Desemba 5 hadi 11.

Ni katika muktadha huu ambapo mamlaka ya jimbo la Kivu Kaskazini ilitangaza, mnamo Desemba 14, janga la kipindupindu katika jimbo hilo.

Kulingana na OCHA, wadau wa misaada ya kibinadamu wanajitahidi kudhibiti janga hili katika maeneo mengine ya kambi za wakimbizi ya Kanyaruchinya, Kibati, Munigi, Don Bosco, miongoni mwa wengine.