Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mpya ukijongea, wito watolewa kuwapa matumaini watu wa Syria

Watoto waliokimbia makazi yao kufuatia machafuko. Wanaishi katika kambi ya wakimbizi mipakani ya kusini magharibi mwa Syria.
© UNICEF/Alaa Al-Faqir
Watoto waliokimbia makazi yao kufuatia machafuko. Wanaishi katika kambi ya wakimbizi mipakani ya kusini magharibi mwa Syria.

Mwaka mpya ukijongea, wito watolewa kuwapa matumaini watu wa Syria

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao cha Baraza la Usalama leo Jumatano, kuhusu hali ya Syria, ambapo limesikiliza taarifa mbili fupi kuhusu hali ya kisiasa na usalama, iliyotolewa  kwa njia ya video na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kwa Syria Geir Pedersen na Martin Griffiths Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya  kuratibu misaada ya dharura, OCHA.

Wakati Mwaka Mpya unakaribia, maafisa wawili wakuu wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza haja ya kuwapa Wasyria matumaini ya siku zijazo na kusisitiza umuhimu wa suluhisho la kina la kisiasa ambalo linaendana na azimio nambari 2254 na Umoja wa Mataifa, linalokidhi matakwa halali ya Wasyria wote, na kurejesha mamlaka ya Syria, uhuru, umoja na nguvu ya himaya.

Katika kikao taarifa ya kwanza, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu kwa Syria, Geir Pedersen, amezungumzia ziara yake mjini Damascus wiki mbili zilizopita ili kuendelea na mazungumzo yake na serikali ya Syria juu ya kuendeleza mchakato wa kisiasa wa kutekeleza azimio nambari 2254, akibainisha kwamba hali ya mambo inaonesha mwelekeo wa wasiwasi:

"Wasyria wanakabiliwa na mzozo wa kibinadamu na kiuchumi unaozidi kuongezeka ndani na nje ya nchi na katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali na yasiyodhibitiwa  na serikali, hali bado ni mbaya zaidi, hasa katika kambi za waliofurushwa." Amesema Pedersen.

Mjumbe huyo wa wa Katibu Mkuu amesema tunakabiliana na hali inayokuja kwa sababu ya zaidi ya muongo mmoja wa vita na migogoro, rushwa na usimamizi mbovu, janga la kifedha la Lebanon, virusi vya Corona, vikwazo, na athari za vita nchini Ukraine.

Mienendo ya hasira

Ametaja kile alichokisema kuwa mienendo hatari inayowaathiri raia, ikiwa ni pamoja na ripoti za mashambulizi ya mara kwa mara ya anga ya serikali kaskazini-magharibi, mashambulizi ya anga ya kaskazini mwa Uturuki, na mashambulizi ya Damascus na kusini magharibi yanayohusishwa na Israel.

Vipaumbele sita ni muhimu

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza haja ya kubadili mienendo hii ya kutatanisha, akiangazia vipaumbele sita ambavyo amesema vinapaswa kuzingatiwa, akionesha kuwa amekuwa akiyafanyia kazi masuala haya yote wakati wa mikutano yake ya kidiplomasia na pande za Syria na wadau wa kimataifa.

Kipaumbele cha kwanza ni kupunguza na kurejesha utulivu.

Hatua ya pili ni kuhuisha upya mfumo wa kibinadamu wa baraza la usalama.

Tatu, haja ya kuanza tena na kufanya mikutano ya kamati ya katiba kuwa muhimu zaidi huko Geneva.

Amerejelea nia ya Umoja wa Mataifa ya kurejesha mikutano ya Kamati ya Katiba huko Geneva mara tu kunapokuwa na nia ya kufanya hivyo na wengine.

Nne, kulipa kipaumbele suala la wafungwa, waliotoweka na waliopotea. Mjumbe huyo wa Katibu Mkuu amesema kuwa alisisitiza huko Damascus umuhimu wa kubadilishana taarifa kuhusu wafungwa na kuachiliwa kwao.

Jambo la tano ni kuhamasisha mazungumzo ili kutambua na kutekeleza hatua za awali za kujenga imani hatua kwa hatua.

Mwaka wa 2022 umeshuhudia rekodi za mambo mabaya

Kwa upande wake, Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, alibainisha kuwa rekodi nyingi zilivunjwa mwaka wa 2022, lakini zilikuwa mbaya sana kama alivyosema kuwa "uhasama uliendelea kusumbua sana, hasa kwenye mstari wa mbele. Kaskazini Magharibi pekee, takriban raia 138 waliuawa na 249 kujeruhiwa kati ya Januari na Novemba na Novemba, kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa. Idadi ya watu wanaohitaji msada imeongezeka na kufikia watu milioni 14.6, ongezeko la watu milioni 1.2 ikilinganishwa na mwaka jana. Idadi hii inatarajiwa kufikia watu milioni 15.3 katika mwaka 2023.”

Griffiths ameongeza kusema “hatujaona idadi kama hiyo tangu kuanza kwa mzozo wa Syria mnamo mwaka 2011, akibainisha kuwa zaidi ya watu milioni 12 zaidi ya nusu ya idadi ya watu wanajitahidi kuweka chakula mezani, na ameonya kuhusu  uwezekano huo” na kwamba karibu watu milioni tatu wanaweza kutumbukia katika hali ya uhaba wa chakula.

Amesema kuzorota kijamii na kiuchumi ni mbaya zaidi tangu kuanza kwa mzozo huo, akielezea hofu yake kwamba mwaka wa 2023 hautatoa afueni kubwa kwa watu wa Syria.