Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN kuunda mfumo wa kukabiliana na majanga

Wasichana wadogo wakiwa nyumbani kwao huko grand Turk, ambayo iliharibiwa vibaya wakati kimbunga Irma kilipopiga Visiwa vya Turks na Caicos.
© UNICEF/Manuel Moreno Gonzalez
Wasichana wadogo wakiwa nyumbani kwao huko grand Turk, ambayo iliharibiwa vibaya wakati kimbunga Irma kilipopiga Visiwa vya Turks na Caicos.

Mashirika ya UN kuunda mfumo wa kukabiliana na majanga

Tabianchi na mazingira

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Mpango wa maendeleo duniani, UNDP, Hali ya hewa Duniani WMO pamoja na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya upunguzaji hatari za majanga UNDRR yanashirikiana kutengeneza mfumo mpya wa ufuatiliaji, kurekodi na kuchambua majanga hatari pamoja na hasara na uharibifu unaosababishwa na matukio hayo.

Kwa ushirikiano mkubwa kati ya mashirika hayo matatu, mfumo huo mpya unatarajiwa kutumika mwakani 2023.

Mfumo huo utatengenezwa huku wakishirikisha maoni ya wadau mara kwa mara na kufanya mashauriano na serikali pamoja na washirika wengine husika.

Kama sehemu ya ushirikiano huu, mashirika hayo matatu kwa pamoja yaliandaa Kongamano la Kiufundi huko Bonn, Ujerumani tarehe 29 mpaka 30 Novemba 2022 ambalo lilishirikisha wawakilishi wapatao 175 wa usimamizi wa hatari za maafa, huduma za hali ya hewa na maji, na taasisi nyingine za kisekta kutoka karibu serikali 50 na mashirika ya kimataifa 60.

Mfumo wa kidigitali

Mfumo huu mpya utaundwa kwa kurejelea mfumo wa DesInventar ambao umekuwa ukitumika katika nchi 110 za Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1994.

Jukwaa hilo lililoketi mwezi uliopita limependekeza kuunda mfumo shirikishi wa kizazi kipya unaolingana na viwango vya takwimu na ukomavu wa kidijitali katika nchi na ambao utaweza kutoa taarifa tofauti tofauti na zenye uwiano, zenye kuweza kufuatilia Matukio ya hataru na hasara pamoja na uharibifu mara kwa mara. 

Mfumo mpya utaendana kikamilifu kwakuzingatia mfumo wa Sendai na kuweka viashiria vinavyolenga kutimiza malengo 17 ya Maendeleo Endelevu SDG, na pia utashirikiana na mwongozo wa WMO kuhusu Matukio ya hatari ambao utatoa rekodi kwa mamlaka za hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi, na matukio yahusianayo na maji ambayo yanasababisha madhara kwa viwango vya kitaifa na kikanda.

Mataifa kujengewa uwezo

Mashirika hayo matatu yatashirikiana kutengeneza sera kuhusu msururu wa thamani wa takwimu na mfumo wa matukio ya hatari na hasara na uharibifu.

Sera hizi nazo zinatarajiwa kuwa tayari mwakani 2023 na kuanza kusambazwa katika mataifa ili kutumika.

Kulikuwa na wito wa ushirikiano kati ya mashirika hayo matatu, imeonekana ni vyema kuimarisha uwezo wa Ofisi za Kitaifa za Kudhibiti Maafa (NDMOs), na kuwezesha uhusiano wa kiutendaji na Huduma ya Kitaifa ya Utabiri wa Hali ya Hewa na Uhai (NMHS) pamoja na taasisi zingine za kisayansi ili kufuatilia vyema matukio ya hatari na hasara na uharibifu.

Mfumo mpya utaruhusu nchi kutoa uchanganuzi bora na taswira ya takwimu ili kusaidia maendeleo yenye taarifa za hatari, kujiandaa na hatua za kibinadamu kwa viwango vya kimataifa.