Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia zaongezeka jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini

Wakimbizi wakisubiri kushukishwa katika eneo moja katika jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini.
Picha: UNHCR/Jake Dinneen
Wakimbizi wakisubiri kushukishwa katika eneo moja katika jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini.

Ghasia zaongezeka jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk ameeleza kushangazwa na mashambulizi dhidi ya raia yanayofanywa na watu wenye silaha huku kukiwa na ongezeko la ghasia katika Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini na kuzitaka mamlaka pamoja na viongozi wa jamii kuchukua hatua za haraka kukomesha umwagaji damu.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo jijini Geneva Uswisi Kamishna Turk amesema ripoti aliyopokea kutoka nchini humo imeeleza raia wamekuwa wakipigwa.

Ripoti huyo pia imeeleza takriban raia 166 wameuawa na 237 kujeruhiwa katika kipindi cha miezi minne iliyopita huku mapigano yakizidi kati ya waasi wenye silaha, na kati ya wanamgambo hasimu wa jamii katika eneo hilo. Zaidi ya watu 20,000 wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia hizo tangu mwezi Agosti 2022.

“Mauaji haya, pamoja na ripoti za unyanyasaji wa kijinsia, utekaji nyara, uharibifu wa mali na uporaji, ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na lazima ukomeshwe," amesema KamishnaTürk na kuongeza kuwa “Ni muhimu Serikali ya Sudan Kusini ifanye uchunguzi wa haraka, wa kina na usiopendelea upande wowote kuhusu ghasia hizo na kuwawajibisha wale wote waliohusika kwa mujibu wa sheria za kimataifa.”

Hakikisheni kuna amani

Ripoti imetanabaisha kuwa raia wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na tishio la ghasia, na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumepunguza utoaji wa msaada wa dharura wa kuokoa maisha wa kibinadamu.

Kamishna huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuhakikisha kuna amani na kusema kuwa “Ninawasihi wale wanaoendeleza vurugu hizi zisizo na maana kuweka silaha zao chini na kufanya mazungumzo ili kushughulikia malalamiko yoyote kwa amani.”

Hata hivyo Kamishna Türk ameelezea wasiwasi kuwa kwamba ghasia hizo zilihatarisha kuenea zaidi ya eneo hilo na akahimiza mamlaka kuchukua hatua za haraka ili kupunguza mvutano na kutoa ulinzi kwa jamii zilizoathirika.

Aidha amewataka viongozi na wazee wa jamii kutumia ushawishi wao kwa makundi yanayohusika na vurugu hizo kukomesha umwagaji damu.