Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upotevu wa bayoanuai unaweka rehani kizazi hiki na vijavyo: CBD Elizabeth Mrema

Elizabeth Maruma Mrema (kushoto) ambaye ni katibu mkuu wa CBD akihudhuria mkutano  wa COP15 huko Montreal nchini Canada
Picha: CBD
Elizabeth Maruma Mrema (kushoto) ambaye ni katibu mkuu wa CBD akihudhuria mkutano wa COP15 huko Montreal nchini Canada

Upotevu wa bayoanuai unaweka rehani kizazi hiki na vijavyo: CBD Elizabeth Mrema

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa 15 au COP 15 wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu bayoanuai, CBD unaendelea mjini Montreal Canada ukizikutanisha serikali kutoka kote duniani na wadau wengine muhimu kwa lengo la kuafikiana malengo mapya yatakayoiongoza dunia katika hatua za kubadili mwelekeo na kusitisha upotevu wa bayoanuai ambayo ni tegemeo la viumbe na mazingira ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa bayoanuai CBD upotevu huo wa bayoanuai unaongezeka kwa kasi ambayo inatishia mustakbali wa dunia kwani uhai wa viumbe vyote vilivyomo duniani unategemea bayoanuai na matendo ya wanadamu ndio chachu ya upotevu huo.  

Elizabeth Maruma Mrema ambaye ni katibu mtendaji wa CBD akizungumza na UN News akiwa mkutanoni mjini Montreal Canada na anaeleza ni kwa nini mkutano huu ambao ni wa kuchukua hatua ni muhimu “Ni mujibu kwa sababu has ani kutokana na ripoti zilizotolewa hivi karibuni na wanasayansi na wanabaolojia, ripoti zote zinasema matendo yetu sisi binadamu dhidi ya bayoanuai ndio yanasababisha hali mbaya ya dunia tuliyofikia wanasayansi wanatuambia tumeshasababisha bayoanuai kupotea kwa asilimia 97, tumechafua hali ya ardhi kwa asilimia 75, bahari majiasilimia 66 pia tumechafua maeneo oevu kwa asilimia 85 , matumbawe kwa asilimia 50 yote imepotea.” 

Bayoanuai  kwa ajili ya chakula na kilimo inapungua
Picha: FAO
Bayoanuai kwa ajili ya chakula na kilimo inapungua

Bila bayoanuai hakuna uhai 

Bi. Mrema akaenda mbali zaidi na kufafanua kwamba binadamu hawawezi kuishi bila bayoanuai “Kwa sababu bayoanuai ndio inayotupa chakula, ndio inayotupatia maji ya kunywa na kutumia na ndio inayotupa madawa. Pia bayoanuai ndio inayopatia watu sio tu chakula bali na maisha, kazi , makazi yanatokana pia na na hii asili.” 

Ameendelea kusema kwamba wanasayansi wameweka bayana kuwa wanadamu wmesababisha hali mbaya ya mazingira katika kiasi ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika Ulimwengu huu hivyo “Kama hakuna kitakachofanyika wakati huu na kwa haraka ina maana vizazi vijavyo, watoto wetu, wajukuu zetu watakuwa hawana mahali pa kuishi wakati sisi watu wazima tulioko sasa hivi ndio tuliochafua haya mazingira.” 

Uhifadhi wa bayoanuai kwa ajili ya chakula na kilimo pia unakwamishwa na upungufu wa maarifa, upungufu wa fedha na ushirikiano usioridhisha
Picha: FAO
Uhifadhi wa bayoanuai kwa ajili ya chakula na kilimo pia unakwamishwa na upungufu wa maarifa, upungufu wa fedha na ushirikiano usioridhisha

Nini kinapaswa kufanywa kuokoa bayoanuai 

Kwa mujibu wa Katibu mtendaji huyo wa CBD wanasayansi wanasema licha ya maafa yote yaliofanyika kuharibu bayoanuai bado asilimia 50 ya maendeleo ya nchi yanatokana na bayoanuai ambayo ni sawa na dola bilioni 44 kwa mwaka ambazo zinatokana na faida ya bayoanuai. 

Kwa mantiki hiyo amesema “Tunapoendelea kuharibu bayoanuai tunazikosesha fursa nchi za ajira ya kazi zote zinazotokana na bayoanuai.” 

Ili faida itokanayo na bayoanuai iweze kuendelea kuwepo kwa kizazi hiki na vijavyo Bi. Mrema amesisitiza kwamba”Ili bayoanuai iweze kusaidia wananchi ni lazima ilindwe, inahitaji iangaliwe vizuri, uhudumiwe na pale ilipoharibika iweze kurudishiwa na manufaa yanayotokana na bayoanuai yaweze kugawanywa bila upendeleo kwa watu wote hasa tukiangalia wale watu wa asili ambao maeneo wanayokaa ndiyo wanasayansi wamesema yana bayoanuai nzuri zaidi na endelevu kuliko sehemu zingine zote.” 

Kwa kutambua hilo CBD inasema ndio maana dunia nzima hivi sasa iko Montreal Canada wakijadiliana ili kuweza kuja na mfumo mpya wa bayoanuai utakaoweza kuisaidia dunia sio tu kupunguza upotevu wa bayoanuai bali kuukomesha kabisa kaba la mwaka 2030 ambao ndio ukomo wa kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDGs. 

Mkutano wa 15 au COP 15 wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu bayoanuai CBD unaendelea mjini Montreal Canada
Picha: CBD
Mkutano wa 15 au COP 15 wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu bayoanuai CBD unaendelea mjini Montreal Canada

Mfumo mpya kutia msukumo wa kulinda bayoanuai 

Bi. Mrema amefafanua kuwa mfumo huo mpya utahakikisha bayoanuai inalindwa 

“Huu mfumo mpya una malengo kamili ambayo yatatuwezesha kutufikisha hapo, malengo ambayo ndani yake yatakuwa na malengo yah atua ambazo kila nchi itapaswa kuzichukua, na kila nchi itatakiwa pia kutoa ripoti inafanya nini ili kuweza kuchangia katika kuhakikisha upotevu wa bayoanuai unakomeshwa.” 

Mkutano huu ni wa wiki mbili na Bi Mrema anaeleza matarajio yao “Tunategemea baada ya wiki mbili viongozi walioko hapa waweze kukubaliana na huo mfumo, mfumo ambao sasa utawezesha kuiongoza dunia nzima na umuhimu utakaofuata baada ya hapo ni kuhakikisha huo mfumo mpya au mkataba mpya tutakaokubaliana unatekelezwa katika nchi. Isipofanyika hivyo inamaana tutakuwa na mkataba kwenye karatasi ambao hautasaidia kurudisha maji tunayopoteza, kuchafua hewa, madawa tunayohitaji na pia kuhakikisha bayoanuai inaendelea kutupatia kazi.” 

Mkutano huo ulioanza Desemba 7 utafunga pazia Desemba 19.