Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka Tanzania hadi Makamba nchini Burundi- Asante UNHCR na wadau

Kelly Clements, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR akizungumza na  Helena Ndakiritumara, mmoja wa wakimbizi wa Burundi waliorejea nyumbani kutoka Tanzania.
UNHCR Video
Kelly Clements, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR akizungumza na Helena Ndakiritumara, mmoja wa wakimbizi wa Burundi waliorejea nyumbani kutoka Tanzania.

Kutoka Tanzania hadi Makamba nchini Burundi- Asante UNHCR na wadau

Wahamiaji na Wakimbizi

Akiwa katika ziara yake ya kwanza nchini Burundi hivi karibuni, Naibu Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHFR Kelly Clements ameisihi jamii ya kimataifa iongeze msaada kwa maeneo na jamii ambako wakimbizi wa Burundi wameamua kurejea nyumbani kwa hiari. 

Tangu mwaka 2017, zaidi ya wakimbizi 200,000 wa Burundi wamerejea nyumbani kutoka nchi jirani kama vile Tanzania. 

Tayari UNHCR imekuwa ikisihi hatua zaidi zifanyike ili kuboresha mazingira kwenye maeneo ambako wakimbizi wanarejea Burundi ili urejeaji wao uwe endelevu. 

Ni katika ziara yake Bi.Clements ameshuhudia wakimbizi zaidi wakirejea kutoka Tanzania na kuzungumza nao, huku wale waliorejea siku nyingi nao wakitoa wito wao na wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC nao wakipaza sauti zao.  

Safari ya kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wakiishi ukimbizini nchini Tanzania. Wamo ndani  ya basi, sura ni za matumaini ya kule waendako. Lango la mpakani na Tanzania, jimboni Makamba upande wa Burundi linafunguliwa, mwisho wa safari na wakimbizi wamefika nyumbani. 

Warundi rejeeni nyumbani tujenge nchi: Ramadhani Chongera 

Ni kwenye kituo cha mapokezi cha mpito cha Gitari na wamelakiwa na Naibu Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Kelly Clements. Kituo hiki cha mapokezi kiko takribani kilometa 10 kutoka mpaka wa Tanzania na Burundi. 

Watumishi wa UNHCR hapa wanasajili raia hawa wa Burundi takribani 400 walioamua kureja nyumbani baada ya kuishi miaka mingi nchini Tanzania, na miongoni mwao ni Ramadhani Chongera akitoa wito kwa waliosalia Tanzania akisema, “Napenda kuwahamasisha wale ambao wamesalia kambini Tanzania warejee nyumbani tujenge nchi yetu kwa sababu maisha kama mkimbizi mara nyingi si mazuri.” 

Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR Bi. Clements baada ya kuzungumza na baadhi ya wakimbizi anafunguka.“wanasubiri kwa hamu kuelekea majumbani mwao. Hapa wanapatiwa vifaa visivyo vya mlo, wanapatiwa fedha, na mbinu za kuanza upya maisha yao. Tunashukuru mamlaka za eneo hili kwa msaada waliotoa kuwezesha kurejea kwa wakimbizi hawa. Hali ilivyo kwenye makazi yao halisi hawafahamu watakuta kuko vipi.” 

Hata hivyo Bi. Clements anasema. “UNHCR tuko hapa pamoja na wadau kadhaa. Tuna mipango ya maendeleo  na uwekezaji vinaelekezwa eneo hili tukitumai kuwa kurejea kwao kuwe endelevu, watoto waweze kwenda shuleni, watu wazima waweze kupata kazi ili maisha yaanze upya. Tunashukuru kwa msaada wenu na tunahitaji zaidi.” 

Nilirejea nyumbani baada ya kuambiwa kuna amani 

Kando mwa waliorejea, wako  wakimbizi kama Helena Ndakiritumara, waliorejea siku nyingi na yuko nyumbani na wajukuu zake, mgeni kawatembelea naye si mwingine bali ni Naibu Kamishna wa UNHCR Bi. Clements. Wamezungumza akielezea hali ya chakula kuwa hakitoshi na ndipo akapatiwa ahadi kuwa atapatiwa msaada na hakusita kutoa shukrani akisema, “Kwa kweli nitashukuru mtakuwa mmeniongezea siku za kuishi. 

Na kisha anasema Bi. Ndakiritumara akaelezea sababu ya kuamua kurejea nyumbani Burundi ni kwamba, “niliona na wakimbizi wengnine wakirejea. Tulisikia kuwa wakifika Burundi wanapatiwa msaada, kwa hiyo nikaamua kurejea nchini mwangu kwa sababu nyumbani ni nyumbani.” 

Wakimbizi wa DRC nchini Burundi wapazia sauti umuhimu wa usalama 

Burundi pia ni nyumbani kwa wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwemo Pascaline Sangongena, ambaye naye alipata ugeni wa Bi. Clements. Hodi ikabishwa.. na hakusita kuwakaribisha.na kisha mazungumzo akiwaelezea safari yake ya kukimbia kutoka DRC hadi kufika Burundi, changamoto alizopitia njiani na sasa yuko na watoto wake, wa kwanza akiwa ni wa kike. 

Baada ya mazungumzo anatoa wito akisema“Wanapaswa kufikiria kuhusu wakimbizi ili wakimbizi wapate msaada zaidi. Wanapaswa kufikiria zaidi nini kifanyike ili wakimbizi wajihisi wako salama.” 

Pamoja na kuweko ukimbizi, wanawake wakimbizi wanaendelea kutiana moyo kwa nyimbo wakiwa na matumaini ya siku zijazo.