Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna wa Haki za Binadamu apongeza makubaliano ya amani nchini Sudan

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk akikutana na viongozi wa mashirika ya kiraia nchini Sudan.
OHCHR/Anthony Headley
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk akikutana na viongozi wa mashirika ya kiraia nchini Sudan.

Kamishna wa Haki za Binadamu apongeza makubaliano ya amani nchini Sudan

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amekaribisha makubaliani kati ya viongozi wa kiraia na wanajeshi nchini Sudan.

Taarifa iliyotolewa leo kutoka jijini Geneva Uswisi na ofisi ya Kamishna Turk imesema amekaribisha kutiwa saini kwa makubaliano hayo na kueleza ni hatua muhimu ya kwanza kuelekea makubaliano ya kisiasa na kurejeshwa kwa serikali inayoongozwa na raia.

“Itakuwa muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono awamu inayofuata ya mpito.” Amesema Kamishna Turk na kuongeza kuwa “Wakati wa ziara yangu nchini Sudan mwezi uliopita, niliguswa na nia ya watu wa Sudan ya kutafakari mustakabali wa nchi hiyo inayozingatia haki za binadamu na haki. Kusainiwa kwa makubaliano ya mfumo ni fursa kubwa ya kuhakikisha kuwa dira hii inakuwa ukweli.”

Kamishna Turk pia amefurahishwa na hatua ya hapo jana kuachiliwa kwa maafisa wawili Wagdi Saleh na Abdullah Suleiman, waliokuwa wanafanya kazi kwenye Kamati iliyovunjwa na Utawala wa Juni 30, 1989 ambayo ilikuwa ikihusika na Kupambana na Ufisadi na Urejeshaji wa Fedha za Umma akieleza tukio hilo ni hatua muhimu ya kujenga imani.

Kamishna huyo wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amehitimisha taarifa yake kwa kutoa ahadi ofisi yake kuendelea kuunga mkono watu wa Sudan katika matarajio yao ya amani, haki, demokrasia na utawala wa sheria, na kuhakikisha kwamba haki za binadamu na uwajibikaji vinasalia kuwa muhimu katika mchakato wa mpito.