Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitolee muda wako wako, Jitolee kipaji chako, Jitolee uzoefu wako: Katibu Mkuu UN

Mfanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania akipanda mti kama sehemu ya kutunza mazingira na kutekeleza ajenda 2030.
UN/Ahimidiwe Olotu
Mfanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania akipanda mti kama sehemu ya kutunza mazingira na kutekeleza ajenda 2030.

Jitolee muda wako wako, Jitolee kipaji chako, Jitolee uzoefu wako: Katibu Mkuu UN

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Kujitolea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa wanadamu kote duniani kutambua mchango wa wanaojitolea na pia kujifunza kutoka kwao ili kila mtu atoe mchango wa kutengeneza mstakabali mwema kwa watu wote.

Bwana Guterres kupitia ujumbe wake kwa sikuu ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Desemba, amesema, “katika Siku ya Kimataifa ya Kujitolea, tunaheshimu kujitolea na michango ya watu wa kujitolea katika kujenga jamii zenye haki na sayari yenye afya.” 

Ameongeza akisema kuwa kupitia huduma yao isiyo na ubinafsi, wanaojitolea huonesha ubinadamu bora. Wao ni mabingwa wa kweli “wa kazi yetu ya kuendeleza amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu. Na roho yao ya kutoa hutajirisha wote.” 

Kauli mbiu ya mwaka huu - "Mshikamano kupitia Kujitolea" - inaangazia umuhimu wa kuungana pamoja ili kujaliana. 

“Ni ukumbusho kwamba kila mtu ana jukumu lake. Popote unapoishi, ujuzi wako wowote, nakuomba uchukue hatua. Jitolee muda wako wako. Jitolee kipaji chako. Jitolea uzoefu wako.” Ametoa wito Katibu Mkuu Guterres.  

Akihitimisha ujumbe wake, Bwana Guterres amesisitiza akisema, “leo na kila siku, tuchukue ushawishi wa mfano kutoka kwa wale wote ambao, kwa matendo ya mshikamano wakubwa na wadogo, wanaboresha ulimwengu wetu. Na tuazimie kufanya sehemu yetu kutengeneza mustakabali mwema kwa wote.”