IFAD: Baada ya kujumuishwa kiuchumi, wenye ulemavu wadhihirisha ulemavu si kutokuwa na uwezo.
Inakadiriwa kuwa asilimia 20 ya watu maskini zaidi duniani wana aina fulani ya ulemavu. Watu wa vijijini wanaoishi na ulemavu wanakabiliwa na changamoto zaidi kuliko wenzao wa mijini ndio maana ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu ni lengo muhimu katika kutekeleza azma ya Mfuko wa umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD.
IFAD tayari ina uzoefu katika kufanya kazi na watu wenye ulemavu. Katika miaka ya hivi karibuni, IFAD imekuwa ikiongeza juhudi zake za kuwajumuisha watu wote wenye ulemavu.
Kwa sababu ya ulemavu nashindwa kugombania maji
Mathalani nchini Kenya, kupitia video ya IFAD anaonekana Leonard Murani, mkulima huyu mwenye ulemavu wa viungo akitembea katika shamba lake la kabichi, kwa msaada wa magongo.
Uhaba wa mvua, umekuwa mwiba kwa wakulima, kwani inabidi watembee mwendo mrefu kusaka maji ya kumwagilia, tena nyakati za usiku kwa kuwa maji yanakuwa ni mengi.
Kwa Bwana Murani, hiyo ni changamoto kwa kuwa ni mlemavu na anasema, “nyakati za mchana siwezi kumwagilia shamba langu kwa sababu kila mkulima anatumia maji, na wakati huo maji yanakuwa hayana nguvu nyingi. Kwa hiyo ni wale wenye nguvu au vijana ndio wanaweza kutumia maji usiku. Hata leo hii siwezi kupata maji usiku.”
IFAD yaweka mfumo wa umwagiliaji
Kilio cha Bwana Murani kilisikika kwani IFAD na serikali ya Kenya walifunga mfumo wa umwagiliaji ambapo pampu ya kusukuma maji inatoka mtoni na sasa mabomba yamefika kwenye mashamba yao.
Sasa bomba linamwagilia maji kwenye shamba la kabichi na hatua hii imekuwa maajabu kwa Bwana Murani akisema, “kwa miaka hiyo miwili ambayo IFAD imetupatia mabomba ya umwagiliaji, nimeona mabadiliko makubwa. Tumepanda mazao yanayoimarisha miili yetu na ziada tunauza.”
Pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwenye kilimo, wakulima wenye ulemavu wanakabiliwa pia na changamoto nyingine.
Steven Johnckeer ni Mtaalamu Mwandamizi wa kiufundi wa IFAD akijikita kwenye Jinsia na ujumuishaji anafafanua akisema, “wakulima wenye ulemavu mara nyingi wanakabiliwa na ubaguzi na unyanyapaa. Hawana pia huduma za mawasiliano, miundombinu na mara nyingi kwenye mikakati ya maendeleo vijiji huwa wanaenguliwa kwa sababu watu wanaona ni gharama kubwa kuwajumuisha au hawana tija.”
IFAD yawezesha watu wenye ulemavu kuinuka kiuchumi
Changamoto anayozungumzia Bwana Johnckeere alikumbana nayo Mariama Jalloh, mkulima nchini Sierra Leone akisema, “tunataka kulima, lakini kilimo cha kibiashara, yaani tunalima na kuuza. Lakini hatuna uwezo wa kulima wenyewe bila kulipa gharama za vibarua. vibarua.
IFAD nayo ikachukua hatua ilipatia Mariama na kikundi chake fedha za kuajiri vibarua wa kufanya kazi ambazo wenyewe hawawezi kuzifanya. Halikadhalika mafunzo kwa maafisa ugani juu ya ujumuishaji watu wenye ulemavu kwenye kilimo.
Sasa Mariamma anasema, “tunahitaij kusaidiwa, na tunataka kuonesha wafadhili wetu kuwa tunaweza kufanya vizuri kwa sababu kuwa na ulemavu, haina maana hauna uwezo. Tunataka kuonesha dunia tuna ulemavu lakini kuna kitu tunaweza kufanya.”
Video inatamatikia shambani kwa Bwana Murani nchini Kenya akisema, “ujumbe wangu kwa watu wote wenye ulemavu duniani, kuweni na matumaini. Hata kama utahisi kuwa huwezi kufanya kitu fulani, jaribu na utafanikiwa.”