Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya vifo vya wakati wa kujifungua kuongezeka barani Afrika: WHO

Daktari akimchunguza mjamzito kwenye kituo cha afya cha Gbaleka, kaskazini mwa Côte d'Ivoire.
© UNICEF/UNI326749// Frank Dejongh
Daktari akimchunguza mjamzito kwenye kituo cha afya cha Gbaleka, kaskazini mwa Côte d'Ivoire.

Idadi ya vifo vya wakati wa kujifungua kuongezeka barani Afrika: WHO

Afya

Kupungua kwa maendeleo yaliyopatikana katika muongo mmoja uliopita dhidi ya vifo vya uzazi na watoto wachanga kunatabiriwa barani Afrika, kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO iliyotolewa leo. 

Ripoti hiyo “Ramani ya takwimu za afya Afrika kwa mwaka 2022” imetathmini maeneo tisa yanazohusiana na lengo la 3 maendeleo endelevu (SDG) kuhusu afya na kugundua kuwa kwa kasi ya sasa, uwekezaji zaidi unahitajika ili kuharakisha maendeleo kufikia malengo hayo na miongoni mwa magumu zaidi kufikiwa ni kupunguza vifo vya uzazi. 

Ripoti inasema Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa, inakadiria kuwa wanawake 390 watakufa wakati wa kujifungua kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030. Hii ni zaidi ya mara tano zaidi ya lengo la ajenda yam waka 2030 la vifo vya chini ya 70 vya uzazi kwa kila vizazi hai 100 000, na iko juu sana kuliko wastani wa vifo 13 kwa kila watoto 100 000 wanaozaliwa hai iliyoshuhudiwa barani Ulaya mwaka 2017 na pia ni zaidi ya kiwango cha kimataifa cha wastani wa vifo 2011. 

Mkunga mjini Addis Ababa akimhudumia mama na mtoto wake mchanga.
© Ethiopian Midwives Associatio
Mkunga mjini Addis Ababa akimhudumia mama na mtoto wake mchanga.

Afrika inahitaji punguzo la vifo kwa asilimia 86 

Ili kufikia lengo la SDG la afya ripoti inasema, Afrika itahitaji punguzo la asilimia 86% kutoka viwango vya 2017, ambapo ni mara ya mwisho takwimu ziliripotiwa, jambo lisilowezekana kwa kiwango cha sasa cha kupungua kwa hatua za kupunguza vifo. 

Kiwango cha vifo vya watoto wachanga katika eneo hilo la Afrika kwa mujibu wa ripoti ni 72 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa wakiwa hai.  

Katika kiwango cha sasa cha asilimia 3.1% cha kupungua kwa kila mwaka, kutakuwa na vifo 54 vinavyotarajiwa kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa hai ifikapo mwaka 2030, idadi ambayo iko juu ya lengo la chini la kupunguza vifo la watoto 25 kwa kila watoto 1000. 

"Afrika inashikilia baadhi ya viwango vya haraka zaidi vya kushuka kwa malengo muhimu ya afya duniani. Hii ina maana kwamba kwa wanawake wengi wa Kiafrika, kujifungua kunasalia kuwa hatari inayoendelea na mamilioni ya watoto hawaishi muda wa kutosha kusherehekea siku yao ya kuzaliwa ya miaka mitano. Ni muhimu kwa serikali kufanya marekebisho makubwa ya kubadili mwelekeo, kushinda changamoto na kuharakisha kasi kuelekea utimizaji wa malengo ya afya. Malengo haya sio hatua muhimu tu, lakini ni msingi wa maisha bora na ustawi kwa mamilioni ya watu.” amesema Dk Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika. 

Licha ya changamoto kuna hatua zilizopigwa 

Ripoti imeainisha kuwa ingawa eneo hilo la Afrika linashuhudia kasi ya kupungua kuelekea malengo muhimu ya afya kama vile chanjo, lakini pia imepiga hatua za maendeleo makubwa katika baadhi ya maeneo katika muongo wa kwanza wa karne ya 21.  

Vifo vya Watoto wa chini ya umri wa miaka 5 vilipungua kwa asilimia 35%, viwango vya vifo vya watoto wachanga vilipungua kwa asilimia 21% na vifo vya uzazi vilipungua kwa asilimia 28%.  

Katika muongo uliopita, maendeleo katika malengo yote matatu yamepungua, hasa kwa vifo vya uzazi.  

Wakati Afrika imepiga hatua katika upangaji uzazi, huku asilimia 56.3% ya wanawake walio katika umri wa kujifungua wa miaka kati ya 15-49 wakiridhika na mahitaji yao ya uzazi wa mpango kwa njia za kisasa za uzazi wa mpango mwaka 2020, kanda hiyo bado iko chini sana ya wastani wa kimataifa wa asilimia 77% na wenye matokeo mabaya zaidi. 

Kupungua huko kwa kasi kumechochewa na athari za usumbufu wa janga la COVID-19.  

Huduma muhimu za afya kama vile huduma baada ya kujifungua kwa wanawake na watoto wachanga, vitengo vya utunzaji mkubwa wa watoto wachanga, na huduma za matunzo wakati wa ujauzito, na huduma za chanjo vilitatizwa wakati wa janga hilo.  

Ripoti inadsema tangu 2021, Afrika pia imekabiliwa na kuibuka tena kwa milipuko ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo mathalani visa vya surua viliongezeka kwa asilimia 400% kati ya Januari na Machi 2022 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Mama Bendu akipokea mwanae waliyezaliwa kutoka kwa mkunga kituo cha Sinje nchini Liberia.
UNFPA/Elena Heatherwick
Mama Bendu akipokea mwanae waliyezaliwa kutoka kwa mkunga kituo cha Sinje nchini Liberia.

Ufadhili ni changamoto kubwa  

Ripoti imeendelea kusema kuwa uwekezaji duni katika afya na ufadhili wa programu za afya ni baadhi ya vikwazo vikubwa vya kufikia lengo la SDG kuhusu afya.  

Kwa mfano, utafiti wa WHO wa mwaka 2022 katika nchi 47 za Afrika uligundua kuwa kanda hiyo ina uwiano wa wahudumu wa afya 1.55 yaani madaktari, wauguzi na wakunga kwa kila watu 1000, ikiwa ni chini ya kiwango cha WHO cha wahudumu wa afya 4.45 kwa kila watu 1000 wanaohitajika kutoa huduma ya afya na kufikia bima ya afya kwa wote. 

Katika kanda ya Afrika, ripoti inasema asilimia 65 ya watoto wanaozaliwa huhudhuriwa na wahudumu wa afya wenye ujuzi ikiwa ni kiwango cha chini zaidi duniani na kikiwa mbali zaidi na lengo la ajenda yam waka 2030 ya asilimia 90%, kulingana na ripoti hiyo ya takwimu za afya Afrika kwa mwaka 2022.  

Pia imeongeza kuwa wakunga wenye ujuzi ni muhimu kwa ustawi wa wanawake na watoto wachanga.  

Kwani vifo vya watoto wachanga vinachangia karibu nusu ya vifo vyote vya Watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.  

Hivyo ripoti imesisitiza kuwa kuharakisha ajenda ili kufikia lengo lake itakuwa hatua kubwa kuelekea kupunguza kiwango cha vifo vya Watoto wa chini ya umri wa miaka 5 hadi vifo chini ya 25 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa hai.