Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatambua tamaduni 19 kuwa turathi za dunia zisizoshikika, miongoni ni mlo wa dhifa Jordan

Mlo aina ya Mansaf kutoka Jordan umeingia katika orodha ya turathi za dunia zisizoshikika au kugusika.
Majdolene Hasan
Mlo aina ya Mansaf kutoka Jordan umeingia katika orodha ya turathi za dunia zisizoshikika au kugusika.

UN yatambua tamaduni 19 kuwa turathi za dunia zisizoshikika, miongoni ni mlo wa dhifa Jordan

Utamaduni na Elimu

Hii leo Umoja wa Mataifa umejumuisha tamaduni 19 kwenye orodha ya turathi za dunia za tamaduni zisizoshikika au kugusika, (Intangibile Cutural Heritage) ambapo tamaduni hizo zinahusisha ufahamu na stadi muhimu kwa ajili ya usanii wa kijadi au vitendo vya kitamaduni vinayohamishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Taarifa iliyochapishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO inasema uamuzi huo umefikiwa leo jijini Rabat nchini Morocco ambako kunafanyika kikao cha Kamati ya Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Turathi za kitamaduni zisizogusika duniani.

Kamati hiyo inaundwa na wawakilishi 24 kutoka nchi 180 wanachama wa mkataba huo.

Tamaduni zilizojumuishwa kwenye orodha ya turathi za dunia

Kwa mujibu wa wavuti huo, jumla ya maombi 46 yaliwasilishwa na kati yao hayo 19 yamejumuishwa kwenye orodha.

Al-Mansaf mlo wa dhima nchini Jordan

Nchini Jordan mlo wa Al-Mansaf ni mlo maarufu wakati wa dhifa na sherehe za kijamii na kitamaduni kwenye eneo la kati la taifa hilo la kiarabu. Ni ishara muhimu inayoibua hisia ya utambulisho na utangamano wa kijamii, na unahusishwa na mtindo wa maisha ya wakulima na wafugaji ambako nyama na maziwa ni vitu vinavyopatikana kwa urahisi.

Mapande makubwa ya nyama ya ngombe au kondoo huchemshwa na kuwekwa viungo na maziwa ya mgando na huliwa kwa pamoja na wali au bulga juu ya kipande chembamba cha mkate. “Maandalizi yake pekee ni ni tukio la kijami huku mapishi yakijumuisha mazungumzo ya changamoto za pamoja, simulizi za hadithi na kuimba.”

 

Aina ya mkate kutoka Ufaransa  Baguette, ambao nao umeingia kwenye orodha ya dunia ya  turathi za tamaduni zisizogusika
Unsplash/Sergio Arze
Aina ya mkate kutoka Ufaransa Baguette, ambao nao umeingia kwenye orodha ya dunia ya turathi za tamaduni zisizogusika

Sherehe zihusianazo na safariya familia takatifu nchin Misri

Tukio hili ni la kukumbuka safari ya Familia Takatifu kutoka Bethlehemu kwenda Misri kukimbia ukandamizaji kutoka kwa Mfalme Herode. Kila mwaka tukio hili hujumuisha sherehe mbili ambamo kwazo wamisri, wakiwemo waislamu na wakritu wa madhehebu ya Koptiki wa umri na jinsia zote wanashiriki kwa kiasi kikubwa. Sherehe ya kwanza ni Ujio wa Familia Takatifu Misri kuanzia mwezi Juni na ya pili ni Kuzaliwa kwa bikira, ni kati ya Mei na Agosti. Washiriki huimba, hucheza michezo ya kijadi, wanapaka rangi miili yao, hurejelea safari hiyo ya maelfu ya miaka iliyopita na huleta utangamano na muungano wa kijamii.

Mbinu za kijadi za usindikaji wa chai nchini China

Nchini China mbinu za kijadi za usindikaji wa chai ukiambatana na tamaduni vinahusisha ufahamu, stadi na vitendo vinavyozingira usimamizi wa mashamba ya chai na uchumaji wa majani ya chai, usindikaji wa majani hayo kwa kutumia mikono, unywaji na upeanaji wa chai hiyo miongoni mwa jamii. Kwa kuzingatia mazigira ya kiasili na mila za eneo husika, wazalishaji au wakulima wa chai wameibuka na aina sita za chai ikiwemo ya kijani, manjano, nyeupe, oolong na nyeusi.

Wachumaji wa majai ya chai kwenye shamba la chai nchini China. Mchakato mzima wa kilimo cha chai hadi unywaji wake umeingia kwenye orodha ya dunia ya turathi za tamaduni zisizoshikika au kugusika.
Wizara ya Utamaduni China 2021 / ZHANG Xiaoxi
Wachumaji wa majai ya chai kwenye shamba la chai nchini China. Mchakato mzima wa kilimo cha chai hadi unywaji wake umeingia kwenye orodha ya dunia ya turathi za tamaduni zisizoshikika au kugusika.

Tamaduni nyingine zilizojumuishwa hii leo kwenye orodha hiyo ni pamoja na uokaji wa mikate nchini Ufaransa utumiao unga, maji, hamira na chumvi pekee bila viambato vingine.

Nyingine ni dansi ya kisasa ya nchini Ujerumani, uchezaji wa ngoma za maigizo ya kiasili huku vinyago vikiwa vimevaliwa huko Korea Kusini.

Korea Kaskazini nayo imeingia kwenye orodha kupitia mlo wake wa tambi baridi zinazotengenezwa kwa ngano na kuchanganywa na nyama na kabichi iliyowekewa siki au Kimchi kwa kikorea.

Wiki takatifu nchini Guatemala ni tukio la maandamano likirejelea mateso ya Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita ambapo maeneo ya mbele ya nyumba na majengo hupambwa na tukio hilo huhamishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kupitia ushiriki wa watu wa rika na jinsia mbalimbali.

Kwa kina orodha yote unaweza kuipata hapa.