Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa kibinadamu pekee hauwezi kukabili changamoto ya wakimbizi wa ndani: UNDP

Wakimbizi wa ndani katika eneo la Bozoum baada ya kukimbia ghasia kutoka vikundi vilivyojihami nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
© UNICEF/Tchameni Zigoto Tchay
Wakimbizi wa ndani katika eneo la Bozoum baada ya kukimbia ghasia kutoka vikundi vilivyojihami nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Msaada wa kibinadamu pekee hauwezi kukabili changamoto ya wakimbizi wa ndani: UNDP

Wahamiaji na Wakimbizi

Juhudi za maendeleo za muda mrefu zinahitajika ili kubadili viwango vilivyovunja rekodi vya wakimbizi wa ndani duniani kote, inasema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa marendeleo, UNDP iliyotolewa leo. 

Ripoti inasema mwaka 2022, zaidi ya watu milioni 100 walilazimishwa kufungasha virago na kuacha nyumba zao.  

Wengi wa wale waliofurushwa kutokana na migogoro, ghasia au maafa wamekwama na kuwa wakimbizi ndani ya nchi zao, na mara nyingi kwa miaka au miongo.  

Ripoti imeongeza kuwa na ni mara chache sana masaibu yao yanagongha vichwa vya habari.  

Mgogoro huu wa wakimbizi wa ndani usioonekana kulingana na ripoti hiyo ya UNDP unatokana na mapungufu katika usaidizi wa maendeleo. 

Juhudi za kubadilisha mambo zinahitajika zaidi kwani mamilioni ya watu wako katika hatari ya kung'olewa makwao kutokana na mabadiliko ya tabianchi katika siku zijazo, inasisitiza ripoti hii yenye kichwa "Kurudisha nyuma mwelekeo wa wakimbizi wa ndani: mtazamo wa maendeleo kuelekea suluhu”. 

Mwanamke akinyunyizia maji mboga katika bustani ya soko iliyoanzishwa kwenye ardhi iliyoharibiwa zamani huko Ouallam, Niger. Bustani hiyo inashirikiwa na wakimbizi, watu waliokimbia makazi yao na wenyeji.
© UNHCR/Colin Delfosse
Mwanamke akinyunyizia maji mboga katika bustani ya soko iliyoanzishwa kwenye ardhi iliyoharibiwa zamani huko Ouallam, Niger. Bustani hiyo inashirikiwa na wakimbizi, watu waliokimbia makazi yao na wenyeji.

Athari za mabadiliko ya tabianchi 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kufikia mwaka 2050, mabadiliko ya htabianchi yanaweza kulazimisha zaidi ya watu milioni 216 kuhama makazi yao, na kuacha maisha yao ya zamani na riziki, na kwenda kuhamia kwenye maeneo salama. 

Mwishoni mwa mwaka 2021, ripoti inasema kulikuwa na wakimbizi wa ndani milioni 59.1 ulimwenguni kote.  

Wakimbizi hawa wa ndani wanahaha kukidhi mahitaji yao ya msingi, kupata kazi zenye staha, kuwa na chanzo thabiti cha mapato, kudumisha afya njema na kupeleka watoto wao shule.  

Wanawake, watoto na makundi mengine yaliyotengwa huteseka zaidi. Kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anavyoonyesha katika Ajenda yake ya 2022 ya utekelezaji wa uhamiaji wa ndani, hali ya sasa haiwezi kutekelezeka. 

Mkuu wwa UNDP Achim Steiner amesema. "Juhudi za ziada zinahitajika ili kukomesha utengwaji wa watu waliolazimika kuhama makwao ambao lazima waweze kutumia kikamilifu haki zao kama raia, ikiwa ni pamoja na kupata huduma muhimu kama vile huduma za afya, elimu, ulinzi wa kijamii na fursa za ajira. Kando na usaidizi wa kibinadamu ambao unasalia kuwa muhimu, mbinu dhabiti inayolenga maendeleo ni muhimu sana katika kuunda mazingira ya amani ya kudumu, utulivu na kujikwamua upya." 

Uchambuzi wa sampuli za takwimu zilizotolewa na kituo cha ufuatiliaji wa ukimbizi wa ndani (IDMC) zinazojumuisha nchi za Colombia, Ethiopia, Indonesia, Nepal, Nigeria, Papua New Guinea, Somalia na Vanuatu unaonyesha kuwa kati ya wakimbizi wa ndani waliojibu tafiti mbalimbali, theluthi moja walisema hawakuwa wamepata ajira, asilimia 68% walionyesha kuwa hawakuwa na pesa za kutosha kukidhi mahitaji ya msingi ya kaya zao na theluthi nyingine walisema afya yao ilidhoofika baada ya kukimbia makazi yao.

Familia ikiwa kwenye makazi yao huko jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia shambulio kubwa kwenye kambi ya wakambizi mwezi Februari mwaka huu wa 2022.
© UNHCR/Hélène Caux
Familia ikiwa kwenye makazi yao huko jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia shambulio kubwa kwenye kambi ya wakambizi mwezi Februari mwaka huu wa 2022.

Malengo ya maendeleo endelevu 

Ritoti hiyo ya UNDP inasema kuzingatia haki na mahitaji ya watu waliohamishwa makwao na serikali zinazohusika ni sharti la kuafikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu SDGs, kama ilivyokubaliwa na viongozi wa dunia mwaka 2015 na ambayo muda wake wa mwisho unakaribia haraka. 

Ripoti hiyo inasisitiza kwamba “ili kushughulikia suala la wakimbizi wa ndani, ni muhimu kwamba serikali zitekeleze suluhisho muhimu za maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji sawa wa haki na huduma za msingi, kukuza ushirikiano wa kijamii na kiuchumi, kwa kurejesha usalama na kuimarisha mshikamano wa kijamii.” 

Imeongeza kuwa ni muhimu kuweka mgogoro huu usioonekana kwenye ajenda ya jumuiya ya kimataifa.  

Ripoti hii inatoa wito wa kuboreshwa kwa utafiti na ukusanyaji wa takwimu katika eneo hili.  

UNDP imejitolea kushughulikia mapengo yaliyotambuliwa kwa kutoa kielezo cha suluhu za wakimbizi wa ndani ili kufuatilia maendeleo na kusaidia serikali kuondokana na hatua za msaada wa kibinadamu na kuingia kwenye mkakati unaozingatia maendeleo.