Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majeraha na machafuko hukatili maisha ya watu 12,000 kila siku: WHO

Kila mwaka maisha ya watu takriban milioni 1.35 hukatizwa kutokana na ajali ya barabarani.
WHO/T. Pietrasik
Kila mwaka maisha ya watu takriban milioni 1.35 hukatizwa kutokana na ajali ya barabarani.

Majeraha na machafuko hukatili maisha ya watu 12,000 kila siku: WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO leo limesema majeraha na machafuko vinasababisha vifo vya watu 12,000 kila siku kote duniani ambavyo ni sawa na kifo 1 kati ya vifo 12.

Kupitia ripoti yake mpya “Mtazamo wa kuzuia majeraha na machafuko” iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis WHO inasema sababu kuu tatu kati ya tano zinazosababisha vifo vywa watu wa umri wa kati ya miaka 5 hadi 29 ni majeraha, athari za ajali za barabarani , mauaji na kujiua. 

Mbali ya sababu hizo ripoti inasema, vifo vingine vinavyohusiana na majeraha ni pamoja na kuzama majini, kuanguka, kuungua na sumu. 

Kwa mujibu wa ripoti kati ya vifo milioni 4.4 vinavyohusiana na majeraha kila mwaka, takriban kifo 1 kati ya vifo 3 kati ya hivi vinatokana na ajali za barabarani, wakati kifo1 kati ya 6 ni vya kujiua, kifo 1 kati ya 9 ni mauaji na kifo 1 kati ya 61 vinatokana na vita na migogoro. 

Sekta ya afya ina jukumu muhimu 

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema “Sekta ya afya ina jukumu kubwa katika kushughulikia hali hiyo na kuzuia majeraha na machafuko kupitia ukusanyaji wa takwimu, kuunda será, kutoa huduma na programu za kuzuia na huduma, kujenga uwezo na kuchagiza kuhusu jamii ambazo hazipati huduma zinazostahili.” 

Ameongeza kuwa “Watu wanaoishi katika umasikini ndio walio na nafasi kubwa zaidi ya kupata majeraha kuliko matajiri.” 

Ripoti imeendelea kusema kuwa hatua nyingi za ufanisi na za gharama nafuu zinapatikana.  

Kwa mfano, nchini Uhispania, wameweka kikomo cha kasi ya kuendesha magari kuwa ni kilometa  kilomita 30 kwa saa  mijini  nah ii inasaidia kuboresha usalama barabarani,  nchini Viet Nam wanatoa mafunzo ya kuogelea ili kusaidia kuzuia watu kuzama na nchini Ufilipino wameweka sheria ya kuongeza umri wa ridhaa ya kujamiiana kutoka miaka 12 hadi 16, kwa nia ya kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia, vyote hivi vinaleta mabadiliko chanya.  

Hata hiyo ripoti imesema, katika nchi nyingi, utashi wa kisiasa na uwekezaji haupo kwani hatua hazipo katika viwango vya kutosha. 

Hatu za haraka zinahitajika 

"Hatua za haraka zinahitajika ili kuepuka mateso haya yasiyo ya lazima kwa mamilioni ya familia kila mwaka," amesema Dkt. Etienne Krug, mkurugenzi wa idara ya masuala ya kijamii ya afya, wa WHO.  

Ameongeza kuwa "Tunajua nini kinapaswa kufanywa, na hatua hizi madhubuti lazima zielekezwe katika nchi na jamii ili kuokoa maisha." 

Ripoti ya WHO inatolewa wakati wa mkutano wa 14 wa dunia wa kuzuia majeraha na ukuzaji wa usalama, unaofanyika hivi sasa Adelaide, nchini Australia.  

Tukio hili linatoa fursa kwa watafiti na watendaji wakuu duniani wa kuzuia majeraha na ukatili kuendelea kutetea hatua zinazozingatia ushahidi ili kuzuia majeraha na vurugu. 

Ripoti hii pia imeainisha njia za kuzuia na muongozo wa kiufundi uliopo wa WHO ambao unaweza kusaidia kufanya maamuzi ya kusonghesha juhudi za kuzuia majeraha na machafuko.