Salima Mukansanga - Kama mimi nimefika Kombe la Dunia, hakuna ambako huwezi kufika

Bi. Salma Mukansanga, Mchechemuzi wa UNICEF kwa kipindi cha miezi 12 ili kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Uchechemuzi chini ya UNICEF Rwanda.
©UNICEF/Steve Nzaramba
Bi. Salma Mukansanga, Mchechemuzi wa UNICEF kwa kipindi cha miezi 12 ili kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Uchechemuzi chini ya UNICEF Rwanda.

Salima Mukansanga - Kama mimi nimefika Kombe la Dunia, hakuna ambako huwezi kufika

Wanawake

Michuano ya fainali za Kombe la Dunia kwa mchezo wa soka kwa wanaume inaendelea nchini Qatar huko Mashariki ya Kati. Mmoja wa watu wanaong’ara katika michuano hii ni Mchechemuzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Rwanda, Salima Mukansanga, ambaye ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuwa mwamuzi au refarii katika Kombe la Dunia. Aliingiaje katika tasnia hii ya mpira wa miguu? UNICEF Rwanda ilizungumza naye kabla hajasafiri kwenda Qatar na hapa Anold Kayanda anaeleza kwa lugha ya Kiswahili kilichozungumzwa. 

“Nilikuwa nyumbani wakati wa likizo nikiwa kidato cha tano nikielekea kidato cha sita katika elimu ya sekondari,” ni Salima Mukansanga, msichana raia wa Rwanda mwenye umri wa miaka 35 mmoja wa waamuzi katika kombe la dunia akieleza kwa kifupi safari yake kwamba alikuwa nyumbani wakati wa likizo wakati huo akiwa kidato cha tano akisubiri kuingia kidato cha sita, aliposikia wakitangaza tangazo kuwa kulikuwa na uandikishaji wa refarii au waamuzi wanawake na wasichana kwa ajili ya mpira wa miguu.  

Anasema, “wakati huo  nikafikiria nyakati zote ambapo kwa udadisi wangu nilikuwa najiuliza hawa waamuzi wa mpira huwa wanafanya nini? Haraka nilituma maombi na nikapata bahati nikakubaliwa. Kwenye mafunzo nikafanya vizuri sana. Nilikuwa katika 5 bora na nikawa mwamuzi au refarii.”  

Salima ambaye kabla ya kuvunja rekodi ya sasa ya kuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuwa mwamuzi katika miaka 92 ya uwepo wa Kombe la dunia, alianza na Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2019 ambapo alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa mwamuzi katika michuano hiyo na kabla ya hapo  mwanzoni mwa mwaka huu alivunja rekodi nyingine kwa kuwa Mwamuzi mwanamke wa kwanza katika Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON kwani kabla ya hapo wanawake walikuwa hawajawahi kuwa waamuzi wa kati, ana wito gani kwa wasichana wengine?  Salima Mukansanga anasema, “Ili kukifikia kile tunachokitaka, tunahitajika kuwa wavumilivu. Kuwa msichana hakutuzuii katika ulimwengu wa sasa. Hapana, hakuna ambacho huwezi kufanya. Kifanye kikatae, kesho utarudi ujaribu tena na ujifunze kutoka kwenye makosa yako kwa sababu utakuwa umepata uzoefu. Usipojaribu tena, unapoteza njia yako wakati ulikuwa kwenye njia sahihi. Ulichohitaji ni kujaribu zaidi. Kwa hiyo kama mimi Salima kutoka Cyangugu eneo lisilofahamika sana nje ya mji nimeweza kufanikisha hili katika hatua hii ya maisha yangu, iwe kokote kule unakotokea, hakuna ambako huwezi kufika.”