Baraza la UN la haki za binadamu launda jopo kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Iran

Waandamanaji wakiwa wamekusanyika huko Stockholm nchini Sweden baada ya Mahsa Amini, msichana mwenye umri wa miaka 22  kufa akiwa kituo cha polisi nchini Iran.
Unsplash/Artin Bakhan
Waandamanaji wakiwa wamekusanyika huko Stockholm nchini Sweden baada ya Mahsa Amini, msichana mwenye umri wa miaka 22 kufa akiwa kituo cha polisi nchini Iran.

Baraza la UN la haki za binadamu launda jopo kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Iran

Haki za binadamu

Kufuatia wito wa Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk wa uchunguzi huru kuhusu ghasia mbaya zinazoendelea dhidi ya waandamanaji nchini Iran, Baraza la Haki za Kibinadamu limeunda ujumbe wa kutafuta ukweli, kuhusiana na maandamano yaliyoanza tarehe 16 Septemba 2022. 

Baraza hilo, linalokutana katika kikao maalum kuchukua hatuakufuatia mzozo uliosababishwa na kifo cha mwezi Septemba chini ya mikono ya polisi cha Jina Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22, limemsikia Bwana Türk akikosoa mawazo ya ngome ya wale wanaotumia mamlaka nchini Iran. 

"Matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima na yasiyo na uwiano lazima yakomeshwe,” amesisitiza mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa 

Picha za kutisha 

"Inanitia uchungu kuona kile kinachotokea nchini Iran. Kuona picha za watoto waliouawa. Ya wanawake waliopigwa mitaani ya watu waliohukumiwa kifo." alikiambia chumba kilichojaa wajumbe. 

Kamishna Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameangazia jinsi vikosi vya usalama, haswa jeshi la walinzi wa mapinduzi ya Kiislamu na vikosi vya Basij vinavyotumia risasi za moto, risasi kwa kutumia ndege na vyuma, mabomu ya machozi na virungu dhidi ya vuguvugu la maandamano wakati yameenea katika miji 150 na vyuo vikuu 140 katika majimbo yote ya Iran. 

Kabla ya kuitisha uchunguzi huru kuhusu madai yote ya ukiukaji wa haki za binadamu , Kamishna Mkuu alibainisha kuwa ofisi yake ilipokea mawasiliano mengi kutoka Iran kuhusu kipindi hicho, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa ndani. Juhudi hizi "zimeshindwa kufikia viwango vya kimataifa vya kutopendelea, na kuwa uhuru na uwazi”, Bwana. Türk alisema. 

Iran imekanusha rasmi 

Akijibu maoni ya Kamishna Mkuu, mwakilishi wa Iran, Khadijeh Karimi, naibu wa makamu wa Rais wa masuala ya wanawake na familia, alisisitiza kwamba hatua za lazima zimechukuliwa kutafuta haki na serikali, baada ya kifo cha Bi Amini.  

Hatua hizo ni pamoja na kuundwa kwa tume huru, ya bunge ya uchunguzi pamoja na timu ya matibabu ya mahakama. 

Ameongeza kuwa "Hata hivyo, kabla ya kutangazwa rasmi kwa uchunguzi huo, hatua za upendeleo na za haraka ya baadhi ya mamlaka za Magharibi na uingiliaji kati wao katika masuala ya ndani ya Iran, kuligeuza maandamano ya amani kuwa ghasia na vurugu.” 

Akiongea pia katika kikao hicho maalumu cha Baraza Maalumu cha 35 tangu kilipoanzishwa mwaka 2005 Javaid Rehman, mwakilishi maalum kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran alisisitiza kuwa katika wiki iliyopita, juhudi za kuwanyamazisha waandamanaji zimeongezeka, ikiwa ni pamoja na dhidi ya watoto. 

Watoto ni miongoni mwa waliokufa 

Takriban watu 60 hadi 70 wameuawa, amesema, wakiwemo watoto watano, wengi wao kutoka maeneo ya Wakurdi.  

Pia ameelezea kuwa kuna hali ya kutisha katika miji ya Wakurdi ya Piranshahr, Javanrood na Mahabad. 

"Serikali ya Iran mara kwa mara imekuwa ikiwasilisha ripoti zisizo na uthibitisho na kukariri madai kwamba Jina Mahsa hakufa kutokana na vurugu au vipigo," amesema mwakilishi huyo maalum.  

Ameongeza kuwa "Katika taarifa nyingine, serikali inakanusha mauaji ya watoto yanayofanywa na vyombo vya usalama, ikidai kwamba walijiua, walianguka kutoka ghorofani, walilishwa sumu au kuuawa na maajenti wa maadui wasiojulikana." 

Hawa ni watatu kati ya takriban watu 400 ambao wameuawa kwa sababu walisimama kutetea haki yao ya kuamua kuhusu maisha yao wenyewe. 

Sheria za kuhusu hijabu 

Tangu kifo cha Bi Amini kufuatia kukamatwa kwake na polisi wa maadili wa Iran 13 Septemba kwa kutovaa hijabu yake ipasavyo, zaidi ya watu 300 wameuawa katika maandamano, wakiwemo watoto wasiopungua 40, kulingana na taarifa za hivi karibuni za ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa. 

Takriban watu 15,000 wamekamatwa pia "na serikali ya Iran sasa inatishia waandamanaji kwa hukumu ya kifo," amesema waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ambaye awali alitoa wito wa kikao maalum 

Ameongeza kuwa  "Na kwa nini? Ni kwa sababu tu wanawake hawa, wanaume na watoto wanataka kufurahia haki ambazo sote tunataka kufurahia kuishi kwa heshima na bila ubaguzi.” 

Akirejelea ujumbe huo, balozi wa Haki za Kibinadamu wa Marekani huko Geneva Michèle Taylor ameliambia Baraza hilo kwamba watu wa Iran "wanadai jambo rahisi sana, jambo ambalo wengi wetu hapa tunalichukulia kirahisi, fursa ya kuzungumza na kusikilizwa. Tunapongeza ujasiri wao, haswa wanawake, wasichana na vijana ambao kwa ujasiri wanadai kuheshimiwa kwa haki zao za kibinadamu na uwajibikaji kwa dhuluma.”