Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame huu nchini Kenya, haujawahi kutokea na sio janga la asili, tuwasaidie

Mchungaji akikagua mfigo yake (mbuzi) kwenye kisima cha maji nchini Kenya.
©FAO/Patrick Meinhardt
Mchungaji akikagua mfigo yake (mbuzi) kwenye kisima cha maji nchini Kenya.

Ukame huu nchini Kenya, haujawahi kutokea na sio janga la asili, tuwasaidie

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa na wadau wake wa masuala ya kibinadamu nchini Kenya wameomba dola milioni 472.6 kusaidia watu milioni 4.3 walioathiriwa na ukame mwaka wa 2023, ili kuunga mkono mwitikio unaoongozwa na Serikali, huku janga hilo likitarajiwa kuwa mbaya zaidi. 

Hali katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo katika Pembe ya Afrika, ni mbaya. Mfano mmoja ni katika Kaunti ya Garissa. Video ambayo imeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Mazingira, UNEP, inaonesha hali ya wananchi kuwa maisha yako hatarini. 

Katika Kliniki inayohudumia eneo hili la Maalimin, Katika Kaunti ya Garissa moja ya maeneo yaliyokumbwa na ukame mkali nchini Kenya, watoto wanaonekana wakifanyiwa uchunguzi wa utapiamlo. Wanapimwa uzito ukilinganishwa na umri wao, mzingo wa mkono na hata ukuaji wao wa mwili.  

Mara baada ya uchunguzi wa kitabibu kufanyika, Abbiralimau Hussein Ibrahim, mtoto mwenye umri wa miaka mitatu amekutwa ana tatizo la lishe duni na ukuaji duni.  

Mama yake ni Samey Ahmed Abdi, ana umri wa miaka 30 na ni mama wa watoto 7. Kwa kutumia lugha ya Kisomali anasema, "wanyama tuliotegemea kama chanzo cha mapato wote wamepukutika. Sasa hatuna kazi. Watoto hawana chakula cha kutosha cha lishe. Ukame umeenea, na watu wanateseka sana. Tunataka serikali iingilie kati na kutusaidia.” 

Naam, tunataka serikali iingile kati. Rigathi Gachagua, Naibu Rais wa Kenya, juzi tarehe 21 mwezi huu wa Novemba akiambata na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya, Dkt. Stephen Jackson, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira, UNEP, Inger Andersen, ndipo walitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza mshikamano wao na jamii zinazokabiliwa na matokeo mabaya ya ukame wa muda mrefu na mbaya zaidi katika historia ya hivi karibuni ya Kenya. 

Naibu Rais wa Kenya, Bwana Rigathi Gachagua anasema, “Serikali imeanza mchakato wa kufadhili Mfuko wa Taifa wa Dharura. Vyanzo haviwezi kutosha kushughulikia changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi sasa na katika siku zijazo. Kwa hivyo, serikali inaomba usaidizi wa kushughulikia pengo la rasilimali katika kutekeleza afua za ukame ili kupunguza hasara, viwango vya janga la njaa. Tuna mzigo mzito lakini wa haraka, ambao hatuwezi kuubeba peke yetu kama serikali." 

 

Stephen Jackson, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya naye anaunga mkono kwamba kwa hali ilivyo, itabidi hatua za haraka zifanyike, “ukame huu nchini Kenya, haujawahi kutokea. Na sio janga la asili. Limetengenezwa na mwanadamu. Katika kipindi cha mwaka 2023, tutakuwa na takribani watu milioni 6 wanaohitaji msaada wa kuokoa maisha. Kwa hivyo ili kukabiliana na hilo, tumezindua ombi kwa ajili ajili ya mwaka 2023. Ni dola milioni 472 ndizo tunazotafuta kutoka kwa wadau wa kimataifa ili kutoa usaidizi wa kuokoa maisha kwa Wakenya wanaokabiliwa na janga hili ambalo hawakusababisha. Tunahitaji juhudi za kimataifa pamoja, katika hali ya dharura na katika ahueni ya muda mrefu.” 

Naye Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji huyu wa UNEP anapigilia msumali katika maneno hayo akisema, "huu sio ukame uliojiibua tu. Hii ni kawaida mpya. Tunaishi katika janga la tabianchi. Hili halisababishwi na yeyote kati ya watu wanaonizunguka. Ikiwa nchi ishirini zenye uchumi mkubwa duniani, G20 zitachukua hatua na kupunguza uzalishaji wao wa hewa chafuzi, kusema ukweli, hatutakuwa na tatizo hili. Sasa, tumetoka kwenye COP 27 na tulichoona ni kwamba hatimaye tuna makubaliano juu ya hasara na uharibifu, njia ya kusonga mbele. Ni sawa. Sasa tunahitaji kuona rasilimali kwenye meza kwa sababu hatuwezi kuwa na watu hapa wanaohama kutoka kwenye janga hadi kwenye janga. Tunahitaji kuleta utulivu huu kupitia uwekezaji katika usimamizi wa rasilimali za maji, katika kilimo endelevu, na mfumo mbadala wa maisha. Hivi ndivyo Umoja wa Mataifa utatafuta kufanya chini ya kazi ya Mwakilishi mkazi.” 

Msikilizaji, ili kuona kwa macho namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kusababisha madhara makubwa, haya yote uliyoyasikia unaweza kuyaona katika video iliyoandaliwa na UNEP na iko katika wavuti wa unnews na pia katika Twitter tafuta @HabarizaUN. Mathalani utaona, Mfugaji Hassan Taqal Adhan, anajaribu kupata angalau matone mawili matatu ya juu juu katika chupa iliyobeba maji ambayo kwa kuyaangalia tu, yamejaa tope. Lakini atafanyaje? Mjukuu wake afe kwa kiu?  Thelma Mwadzaya, UN News, Kenya.