Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya wanawake ni uhalifu na dharura ya kiafya ya umma: Guterres

Wanawake kutoka Amerika Kusini na Caribbean wakiandamana katika mitaa ya Bogota, Colombia, wakidai kukomeshwa kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana.
UN Women
Wanawake kutoka Amerika Kusini na Caribbean wakiandamana katika mitaa ya Bogota, Colombia, wakidai kukomeshwa kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana.

Ukatili dhidi ya wanawake ni uhalifu na dharura ya kiafya ya umma: Guterres

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ukatili dhidi ya wanawake na wasichana unaendeklea kuwa moja ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea kuiathiri dunia hivi sasa. 

Katika ujumbe wake kwa ajili ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana inayoadhimishwa kila mwaka 25 Novemba, Antonio Guterres amesema “ Ukatili huo ni uhalifu wa kuchukiza na ni dharura ya afya ya umma, yenye madhara makubwa kwa mamilioni ya wanawake na wasichana katika kila kona ya dunia.” 

Takwimu za hivi karibuni kutoka kwa shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women zinathibitisha kwamba wakati wa janga la COVID-19, viwango vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana vimeongezeka. 

Katika nchi 13, karibu nusu ya wanawake wote waliripoti kwamba wao au mwanamke wanayemjua alianza kukabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia wakati wa janga la COVID-19. 

Ujumbe huo wa Katibu mkuu umeendelea kusema kwamba takriban robo ya wanawake waliripoti kuwa migogoro majumbani imekuwa ya mara kwa mara na hivyo kuhisi usalama mdogo majumbani. 

“Vurugu katika sehemu yoyote ya jamii hutuathiri sisi sote. Kuanzia makovu kwenye kizazi kijacho hadi kudhoofika kwa mfumo mzima wa kijamii.” Amesisitiza Guterres na kuongeza kwamba “Tunaweza kuchora mstari wa moja kwa moja kati ya unyanyasaji dhidi ya wanawake, ukandamizaji wa kiraia na migogoro ya vurugu. Kuanzia ubakaji na utumwa wa kingono unaotumika kama zana za vita, hadi uzi wa chuki dhidi ya wanawake unaopitia misimamo mikali yenye jeuri. Lakini ukatili dhidi ya wanawake si suala lisiloweza kuepukika, kwani sera muafaka na mipango mizuri vibnaweza kuzaa matunda.” 

Kukabiliana na chimbuko la ukatili  

Kwa mujibu wa bwana Guterres hiyo ina maana ya mikakati ya kina, ya muda mrefu ambayo inakabiliana na vyanzo vikuu vya unyanyasaji, kulinda haki za wanawake na wasichana, na kuchagiza vuguvugu imara la kupigania haki za wanawake. 

“Huu ndio mfano ambao Umoja wa Mataifa umejenga kupitia ushirikiano wake na Muungano wa Ulaya, mpango wa Spotlight.”  

Ameongeza kuwa “Mwaka jana, katika nchi washirika, tuliona ongezeko la asilimia 22 la mashtaka ya wahalifu. Sheria na sera 88 zilipitishwa au kuimarishwa. Na zaidi ya wanawake na wasichana 650,000 waliweza kupata huduma za kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, licha ya vikwazo vinavyohusiana na janga hilo.” 

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa “Mabadiliko yanawezekana. Sasa ni wakati wa kuongeza juhudi zetu ili kwa pamoja tuweze kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ifikapo 2030.”