Mradi wa UNICEF Malawi wanusuru kaya zilizokuwa zimekata tamaa
Mradi wa UNICEF Malawi wanusuru kaya zilizokuwa zimekata tamaa
Nchini Malawi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF kwa msaada kutoka kwa wadau wake wa maendeleo linatekeleza mradi wa kupatia fedha jamii au MSCTP kwa ajili ya kupunguza umaskini, kukabili utapiamlo halikadhalika kuondokana na utoro shuleni utokanao na wazazi kushindwa kulipa karo.
Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF inaanza kwa kuonesha wanawake kwa wanaume wakiwa wamepanga foleni huku wameshikilia nyaraka tayari kupokea mgao wa fedha kwa mwezi kupitia mradi huo wa mgao wa fedha taslim kunusuru kaya maskini.
Mradi umeniwezesha kupeleka watoto shule
Mary Wale mnufaika kutoka wilaya ya Balaka mkoa wa Kusini wa Malawi anasema, “niko hapa kunufaika na mradi wa mgao wa fedha za kijamii. Nilikuwa maskini sana, sikuwa na chakula, sikuweza kupeleka watoto wangu shuleni, hata sikuwa na mavazi. Sasa nina furaha sana. Kwa fedha hizo nitatununua mahindi, nitakarabati nyumba yangu kwa kuwa iko kwenye hali mbayá. Nitanunua kuku wa kufuga ili wanisaidie siku za usoni.”
Pamoja na kugawa fedha taslimu, mradi huu ulioanza kutekelezwa nchini Malawi mwaka 2006, umeanzisha vikundi vya kuweka na kukopa ambako wanachama wana uwezo wa kukopa fedha na kurejesha.
Elube Ositini yeye ameanza kunufaika na mradi huu tangu mwaka 2014 na anasema,“ kwa miaka yote hii nimeweza kujenga nyumba, kununua mifugo, kupeleka watoto shuleni. Na katika miaka minne ijayo nataka niongeze ng’ombe wafikie 10, niwapeleka watoto wangu hadi shule ya sekondari. Nina furaha sana kwa sababu nilicho nacho sasa sikutarajia kuwa navyo maishani.”
Sasa naweza kulisha kaya yangu
Kwa Richard Kakoti ambaye naye yuko kwenye foleni kupata mgao, mradi huu ni mkombozi sana kwao kwani njaa iliwapiga na sasa wana ahueni kubwa akisema “Nimepokea Kwacha za kimalawi elfu 36. Hii ni mara yangu ya kwanza kupokea mgao huu wa fedha. Fedha hizi zitanisaidia mimi kama mkuu wa kaya kununua mahindi, maharagwe na mafuta ya kupikia kwa ajili ya familia yangu.”
Kwacha Elfu 36 ni sawa na dola dola 35.
UNICEF inasema mradi huo pamoja na kusaidia kukabili njaa, unasaidia pia kujenga mnepo kwa kaya wakati huu ambao mtikisiko wa kiuchumi unaleta changamoto kwenye jamii.
IMF yapatia Malawi mkopo wa kujikwamua na uhaba wa chakula
Katika hatua nyingine, shirika la fedha duniani, IMF nalo hii leo limetangaza kuidhinisha dola milioni 88.32 kwa ajili ya Malawi kupitia mfumo wa utoaji kasi mikopo kuhimili mtetemeo wau haba wa chakula unaokumba dunia hivi sasa.
Malawi inakuwa nchi ya kwanza ya kipato cha chini kutumia mfuko huo tangu upitishwe na Bodi Tendaji ya IMF mwezi uliopita wa Oktoba.