Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saudi Arabia kuanza kunyonga tena kwa makosa ya mihadarati inasikitisha: OHCHR

Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia
Unsplash/Ekrem Osmanoglu
Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia

Saudi Arabia kuanza kunyonga tena kwa makosa ya mihadarati inasikitisha: OHCHR

Haki za binadamu

Saudi Arabia lazima ipitishe sheria ya kusitishwa kwa hukumu ya kifo kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, imesema ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, baada ya taifa hilo la Mashariki ya Kati kuanza tena adhabu ya kifo kwa uhalifu huo unaohusiana na daa za kulevya. 

Msemaji  wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Liz Throssell amesema mauaji yamekuwa yakifanyika karibu kila siku katika wiki mbili zilizopita, kufuatia kumalizika rasmi kwa muda wa kwa kusitishwa unyongaji wa miezi 21. 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Bi Throssell amesema "Kurejeshwa kwa hukumu ya kifo kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya nchini Saudi Arabia ni hatua ya kusikitisha sana, zaidi yah apo inakuja siku chache tu baada ya mataifa mengi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa kwa hukumu ya kifo duniani kote,"  

Watu 17 wamenyongwa hadi sasa 

Tangu tarehe 10 Novemba, Saudi Arabia imewanyonga wanaume 17 kwa kile kinachoitwa makosa ya dawa za kulevya na magendo, huku watatu wakitarajiwa kunyongwa Jumatatu. 

Walionyongwa hadi sasa ni Wasyria wanne, Wapakistani watatu, Wajordani watatu na Wasaudi saba. 

Kwa vile unyongaji unathibitishwa tu baada ya kutokea, ofisi ya OHCHR haina taarifa kuhusu idadi ya watu wanaosubiri kunyongwa nchini humo. 

Saudia sitisheni unyongaji mara moja 

Hata hivyo, Bi Throssell amesema wamepokea ripoti kwamba mwanamume kutoka Jordan, Hussein abo al-Kheir, anaweza kuwa hatarini. 

Kikosi Kazi cha Umoja wa Mataifa cha kuzuia maauji ya kiholela hapo awali kilishughulikia kesi yake na kubaini kuwa kushikiliwa kwake kizuizini hakuna msingi wa kisheria na kulikuwa kwa kiholela.  

Wataalamu hao wa haki za binadamu pia wameelezea wasiwasi mkubwa kuhusiana na haki ya kesi yake kusikilizwa kwa haki. 

"Tunaiomba Serikali ya Saudia isitishe taarifa ya kunyongwa kwa al-Kheir na kufuata maoni ya kikosi kazi kwa kufuta hukumu yake ya kifo, kumwachilia mara moja bila masharti, na kwa kuhakikisha kwamba anapata matibabu, fidia na mafao mengine.” 

Kinyume na kanuni za kimataifa 

Bi. Throssell amesisitiza kuwa kutoa hukumu ya kifo kwa makosa ya dawa za kulevya hakukubaliani na kanuni na viwango vya kimataifa. 

Ameongeza kuwa “Tunatoa wito kwa mamlaka za Saudia kupitisha usitishaji rasmi wa hukumu ya kunyongwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, kubatilisha hukumu za kifo kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, na kuhakikisha haki ya kusikilizwa kwa kesi kwa washtakiwa wote, ikiwa ni pamoja na wale wanaoshtakiwa kwa makosa hayo, kulingana na majukumu yake ya kimataifa.”