Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Choo: UN yaangazia athari za janga la usafi kwenye maji ya chini ya ardhi 

Wasichana wakitumia huduma ya choo katika shule Jimbo la Benue, Nigeria.
© UNICEF/Adzape
Wasichana wakitumia huduma ya choo katika shule Jimbo la Benue, Nigeria.

Siku ya Choo: UN yaangazia athari za janga la usafi kwenye maji ya chini ya ardhi 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika Siku ya Choo Duniani, iliyoadhimishwa Jumamosi hii, Umoja wa Mataifa unasisitiza haja ya kuboresha usafi wa mazingira ili kulinda maji ya ardhini dhidi ya uchafuzi unaotokana nataka.

"Katika Siku hii ya Choo Duniani, zingatia madhara ya mifumo duni ya usafi kwenye maji ya ardhini: yanamwaga kinyesi cha binadamu kwenye mito, maziwa na ardhi, na kuchafua vyanzo vya maji vilivyo chini ya miguu yetu." Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema katika ujumbe wake. 

Kampeni ya Siku ya Choo Duniani 2022, iliyopewa jina la "Fanya visivyoonekana vionekane" inazingatia athari za janga la usafi wa mazingira kwenye maji ya chini ya ardhi. Maji ya chini ya ardhi ndio chanzo cha maji safi zaidi ulimwenguni. Wanasaidia usambazaji wa maji ya kunywa, mifumo ya usafi wa mazingira, kilimo, viwanda na mifumo ya ikolojia. Mabadiliko ya hali ya tabianchi yanapozidi kuwa mbaya na idadi ya watu kuongezeka, maji ya chini ya ardhi ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu. 

Jukumu muhimu la vyoo salama 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Guterres, suala hili limefichwa kwa muda mrefu, kwa sababu linafanyika chini ya ardhi, kati ya jamii maskini zaidi. 

“Leo, tuangazie jukumu muhimu la vyoo hivyo salama katika nyanja zote za maendeleo endelevu, zinazoonekana au zisizoonekana. Hebu tuchukue hatua kwa uthabiti, bila kuchelewa, kufikia haki ya msingi ya maji na usafi wa mazingira duniani kote.” Ameongeza Guterres. 

Katibu Mkuu amebainisha  kuwa kuboresha usafi wa mazingira ni "njia ya gharama nafuu ya kubadilisha maisha ya watu. Faida zinakwenda mbali zaidi ya afya ya umma. Usafi wa mazingira na vyoo salama vinaboresha lishe na usimamizi wa rasilimali adimu ya maji na kukuza mahudhurio ya shule na fursa za kazi hasa kwa wanawake na wasichana.” alisema. 

Bwana Guterres amekumbushia kuwa kila dola inayowekeza kwenye vyoo na usafi wa mazingira inapunguza gharama za afya mara tano na kuongeza tija, elimu na ajira mara tano. 

UNICEF kusaidia 

Kupitia Mpango wa Kufanikisha Usafi wa Mazingira Unaosimamiwa kwa Usalama mwaka 2022-2030, UNICEF itasaidia watu bilioni 1 kupata huduma za usafi wa mazingira zinazofaa, kupitia usaidizi wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja, na kwa ushirikiano na washirika tofauti. 

Katika makadirio ya mwaka 2020, watu bilioni 3.6 walikosa huduma za kujisafi, na kusababisha wengi wao kujisaidia katika maeneo ya wazi, hali inayoleta hatari kwa afya, ustawi na usalama wa wote. 

Tags: Siku za UN, Siku ya Choo Duniani, Antonio Guterres, UNICEF