Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaharakati huko COP27 wasema hakuna hatua kwa tabianchi bila kujali haki za binadamu

Ina Maria Shikongo, mwanaharakati wa watu wa jamii ya asili kutoka Namibia akiwa kwenye maandamano huko COP27 Sharm-el-Sheikh nchini Misri.
UN News/Laura Quinones
Ina Maria Shikongo, mwanaharakati wa watu wa jamii ya asili kutoka Namibia akiwa kwenye maandamano huko COP27 Sharm-el-Sheikh nchini Misri.

Wanaharakati huko COP27 wasema hakuna hatua kwa tabianchi bila kujali haki za binadamu

Tabianchi na mazingira

Huko Sharm-el-Sheikh nchini Misri, kwenye mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP27, tarehe 17 mwezi huu wa Novemba yalishuhudiwa maandamano ya maelfu ya wawakilishi wa watu wa jamii ya asili, wanawake, wanarahakati wa masuala ya jinsia, vijana, mazingira na haki kwa tabianchi kutoka pande mbalimbali za dunia.

Soundcloud

Wao waliandamana kwa niaba ya maelfu ya mashirika na mamilioni ya watu  na kupitisho azimio lao la umma kuhusu haki kwa tabianchi. Wanapaza sauti je ni sauti zipi? Wanataka nini?

Tunapigania haki! Na kwa  ukombozi!! Kila tunapoenda!!! Watu wanataka kufahamu! Kwa hiyo tunawaambia!!

Kwenye barabara za Sharm-el-Sheikh nchini Misri, eneo la mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP27, wanaharakati, wanawake kwa wanaume wakiandanmana wakipaza hizo sauti wakiwa na mabango mbalimbali.

Mfano bango moja limeandikwa kutokomeza ukoloni wa kiuchumi na wa kijamii!!! Lingine Fidia kwa uharibifu utokanao na madhara ya mabadiliko ya tabianchi!! Lingine tokomeza nishati kisukuku.

Anayeonekana kiongozi wa maandamano haya yaliyoitwa ya Watu, akiwa na kipaza sauti ni Gina Cortes Valderrama, mwanaharakati huyu kutoka Colombia na anasema “tunatambua kuwa hakuwezi kuweko na haki ya tabianchi bila haki za binadamu na haki za watu wa jamii ya asili. Tunazitaka serikali zikomeshe tabia ya kubinya fursa za raia kuzungumza, ziheshimu haki na utu wa watu wa jamii ya asili, wafanyakazi, wanaharakati wa tabianchi, haki za binadamu na watetezi wa mazingira.”

Wanaomsikiliza wanaonekana kuguswa na ujumbe na mikono yao wamenyanyua juu wakikunja konde kuonesha kumuunga mkono. Gina anaendelea akisema, “ujumbe wetu leo ni kutetea haki za binadamu, haki za binadamu ambazo zinapaswa kuwa msingi wa mashauriano, lakini suala hilo limekuwa likisiginwa na maslahi ya faida binafsi, halikadhalika masoko. Tuko hapa kubadili mwelekeo huu na kuelekea mwelekeo wa marekebisho.”

Gina akachukua tena kipaza sauti na kuanza kuongoza wenzake akisema wanachotaka kwenye mkutano!!! tunataka nini! Haki  ya tabianchi!! Lini tunataka! Hivi sasa!! Tusipopata! Funga kabisa!!

Kutoka Namibia, mwanaharakati wa tabianchi Ina Maria Shikongo anafunguka ya kwamba, “sisi ndio tunapaswa kuwa kwenye meza ya mazungumzo. Tunapaswa kuwa sisi kama mataifa yenye jamii za asili na jamii zilizoathirika. Tunapaswa kuwa pale. Tuna majawabu. Watu wa jamii ya asili wana majawabu.”

Sasa wameketi chini na mabango yao moja likiwa limeandikwa Hakuna haki ya tabianchi bila haki ya kijinsia.

Dominika Lasota mwanaharakati kutoka Poland akasimama na kutoa dukuduku lake kuhusu mafuta ya kisukuku akisema, “hatimaye tunapaswa kutambua kuwa hakuna mustakabali wowote na nishati kisukuku, na tunahitaji kuweka fedha zote zinazohitajika, nguvu zote na utashi wa kisiasa katika jawabu la kupanua wigo wa nishati jadidifu, mpito ulio haki kuelekea nishati hiyo na kuondokana na mafuta ya kisukuku.”