Kupuuzwa kwa afya ya kinywa kunaathiri karibu nusu ya watu duniani:WHO

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil wanaohudumu nchini Haiti wakifundisha watoto jinsi ya kutunza afya ya kinywa. (Picha MAKTABA)
UN /Marco Dormino
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil wanaohudumu nchini Haiti wakifundisha watoto jinsi ya kutunza afya ya kinywa. (Picha MAKTABA)

Kupuuzwa kwa afya ya kinywa kunaathiri karibu nusu ya watu duniani:WHO

Afya

Ripoti mpya ya hali ya afya ya kinywa duniani iliyochapishwa leo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO inatoa picha kamili ya kwanza kabisa ya mzigo wa magonjwa ya kinywa na takwimu kwa nchi 194, ikitoa ufahamu wa kipekee katika maeneo muhimu na masuala ya afya ya kinywa ambayo ni muhimu kwa wafanya maamuzi kuyatilia maanani. 

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inasema ripoti hiyo inaonyesha kuwa karibu nusu ya watu duniani saw ana asilimia 45 au watu bilioni 3.5 wanaugua magonjwa ya kinywa, huku watu 3 kati ya 4 walioathirika wakiishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati.  

WHO inasema visa vya kimataifa vya magonjwa ya kinywa vimeongezeka kwa bilioni 1 katika kipindi cha miaka 30 iliyopita ikiwa ni dalili ya wazi kwamba watu wengi hawana njia za kuzuia na matibabu ya magonjwa ya kinywa. 

"Afya ya kinywa kwa muda mrefu imekuwa ikipuuzwa katika afya ya kimataifa, lakini magonjwa mengi ya kinywa yanaweza kuzuiwa na kutibiwa kwa hatua za gharama nafuu zilizoainishwa katika ripoti hii. WHO imejitolea kutoa mwongozo na usaidizi kwa nchi ili watu wote, popote wanapoishi na chochote kipato chao, wawe na maarifa na zana zinazohitajika kutunza meno na midomo yao, na kupata huduma za kinga na matunzo pale wanapohitaji .” amesema mkurugenzi mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus. 

Ongezeko la kasi la magonjwa ya kinywa 

Kwa mujibu wa WHO magonjwa ya kawaida ya kinywa ni kuoza kwa meno, ugonjwa ya fizi, kupoteza meno na saratani ya mdomo.  

Ugonjwa maarufu zaidi duniani wa kinywa ni wa kuoza kwa meno ambao unaathiri takriban watu bilioni 2.5 na wengi hawatibiwi .  

Ugonjwa mbaya wa fizi  ndio sababu kuu ya kupoteza meno na unakadiriwa kuathiri watu bilioni 1 duniani kote.  

Na takriban visa vipya 380,000 vya saratani ya kinywa hugunduliwa kila mwaka. 

Ripoti hiyo ya WHO inasisitiza kwamba “kukosekana kwa usawa dhahiri katika upatikanaji wa huduma za afya ya kinywa, na mzigo mkubwa wa magonjwa ya kinywa ni hali zinazoathiri watu walio hatarini zaidi na wasio na uwezo. Watu wa kipato cha chini, watu wanaoishi na ulemavu, wazee wanaoishi peke yao au katika nyumba za utunzaji wa wazee, wale wanaoishi katika jamii za mbali na vijijini na watu kutoka kwenye vikundi vya wachache hubeba mzigo mkubwa wa magonjwa ya kinywa.” 

WHO inasema mtindo huu wa kukosekana kwa usawa ni sawa na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama vile saratani, magonjwa ya moyo na mishipa, kisukari, na matatizo ya akili.  

Ugonjwa mbaya wa fizi  ndio sababu kuu ya kupoteza meno na unakadiriwa kuathiri watu bilioni 1 duniani kote - WHO  

Sababu za hatari zinazoeneza magonjwa yasiyoambukiza kama vile unywaji wa sukari nyingi, aina zote za utumiaji wa tumbaku, na matumizi mabaya ya pombe yote huchangia tatizo la afya ya kinywa duniani kote. 

Vikwazo vya kutoa huduma za afya ya kinywa 

Ripoti hiyo mpya ya WHO inasema ni asilimia ndogo tu ya watu duniani wanahudumiwa na huduma muhimu za afya ya kinywa, na wale walio na uhitaji mkubwa mara nyingi wanapata huduma chache zaidi.  

Vikwazo vikubwa vya kufikisha huduma za afya ya kinywa kwa wote ni pamoja na: 

  • Huduma ya afya ya kinywa zinahitaji gharama kubwa nje ya bima. Hii mara nyingi husababisha gharama na mzigo mkubwa wa kifedha kwa familia na jamii. 
  • Utoaji wa huduma za afya ya kinywa kwa kiasi kikubwa hutegemea watoa huduma waliobobea sana wanaotumia vifaa na nyenzo za hali ya juu, na huduma hizi hazijaunganishwa vyema na miundo ya afya ya msingi. 
  • Mifumo duni ya taarifa na ufuatiliaji, ikichanganywa na kipaumbele cha chini kwa utafiti wa afya ya kinywa ya umma ni vikwazo vikubwa vya kuunda mfumo na sera zenye ufanisi zaidi za afya ya kinywa. 

Fursa za kuboresha afya ya kinywa kimataifa 

Ripoti hiyo inaonyesha kuna fursa nyingi za kuboresha hali ya afya ya kinywa duniani ikiwa ni pamoja na: 

  • Kuchukua mtazamo wa afya ya umma kwa kushughulikia mambo ya kawaida ambayo ni hatari kwa kuhimiza lishe bora isiyo na sukari nyingi, kuacha matumizi ya aina zote za tumbaku, kupunguza unywaji wa pombe na kuboresha upatikanaji wa dawa za meno za floridi zenye ufanisi na gharama nafuu. 
  • Kupanga kwa usawa huduma za afya ya kinywa kama sehemu ya mipango ya kitaifa ya afya na kuboresha ujumuishaji wa huduma za afya ya kinywa katika huduma ya afya ya msingi kama sehemu ya huduma ya afya kwa wote.
  • Kufafanua upya miundo ya wafanyakazi wa afya ya kinywa ili kukidhi mahitaji ya idadi ya watu na kupanua uwezo wa wahudumu wa afya wasio wa meno ili kuongeza wigo wa huduma ya afya ya kinywa. 
  • Na kuimarisha mifumo ya taarifa kwa kukusanya na kuunganisha takwimu za afya ya kinywa katika mifumo ya kitaifa ya ufuatiliaji wa afya. 

Dkt. Bente Mikkelsen, Mkurugenzi wa WHO wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza amesema "kuweka watu katika kitovu cha huduma za afya ya kinywa ni muhimu ikiwa tunataka kufikia malengo ya huduma ya afya kwa wote kwa watu binafsi na jamii ifikapo 2030.”  

Ameongeza kuwa "ripoti hii ni sehemu ya kuanzia kwa kutoa taarifa za msingi ili kusaidia nchi kufuatilia maendeleo ya utekelezaji, huku pia ikitoa mrejesho kwa wakati unaofaa kwa watoa maamuzi katika ngazi ya kitaifa. Kwa pamoja, tunaweza kubadilisha hali ya sasa ya kutojali afya ya kinywa.”