Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres akaribisha muafaka wa kuendelea na mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi

Meli ya kwanza ya kibiashara ikiwa na nafaka kupitia mpango wa usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi
© UNOCHA/Levent Kulu
Meli ya kwanza ya kibiashara ikiwa na nafaka kupitia mpango wa usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi

Guterres akaribisha muafaka wa kuendelea na mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amekaribisha makubaliano yaliyofikiwa na pande zote ya kuendelea na mpango wa usafirishaji nafaka wa bahari Nyeusi bila bugudha ili kuwezesha kusafirisha nafaka, vyakula vingine na mbolea kutoka Ukraine.  

Katika taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York Marekani Guterres amesema Umoja wa Mataifa umedhamiria kuendelea kuunga mkono kituo cha uratibu wa pamoja na mpango ili kuhakikisha usafirishaji huo unaendelea bila changamoto yoyote. 

Pia mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema Umoj huo umedhamiria kuondoa vikwazo vyote vilivyosalia vya kusafirisha chakula na mbolea kutoka shirikisho la Urusi akisisitiza kuwa makubaliano yote yaliyotiwa saini Istanbul Uturuki miezi mitatu iliyopita ni muhimu katika kushusha bei ya chakula na mbolea na kuepuka mgogoro wa kimataifa wa chakula.  

Katibu Mkuu ameongeza kuwa mpango wa usafirishaji nafaka wa Bahari Nyeusi unaendelea kuonyesha umuhimu wa diplomasia linapokuja suala la kutafuta suluhu za pamoja za kimataifa kwa changamoto za kimataifa zinazoathiri watu wote.