Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kulinda bayoanuwai inamaanisha kulinda mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris: COP27

DRC
© FAO/Thomas Nicolon
DRC

Kulinda bayoanuwai inamaanisha kulinda mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris: COP27

Tabianchi na mazingira

Wakati kwa miaka mingi mzozo wa hmabadiliko ya tabianchi na mzozo wa bioanuwai umechukuliwa kama maswala tofauti, ukweli kama ulivyoangaziwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa COP27 leo ni kwamba hakuna njia ya kuhakikisha kiwango cha joto duniani kinasalia nyuzi joto 1.5 ° C bila kuchukua hatua haraka kulinda maliasili. 

"Mambo hayo mawili yanapaswa kuonekana yako sanjari kwenye njia moja na sio moja kuwa juu kuliko lingine," amesema Elizabeth Mrema, katibu mtendaji wa sekretariati ya mkataba wa kimataifa wa kulinda bayoanuai CBD, akizungumza na UN News.  

CDB ni chombo cha kisheria cha kimataifa cha ulinzi wa bayoanuwai kilichoidhinishwa na mataifa 196. 

Bi. Mrema ameendelea kusema kwamba siku ya Bioanuwa katika mkutano wa COP27 huko Sharm El-Sheikh inakuja wiki mbili tu kabla ya mkutano wa ngazi ya juu wa nchi wanachama wa CBD huko Montreal ambao unaolenga kubadili mwenendo wa upotevu wa bayoanuwai. 

Kasuku
Unsplash/Alan Godfrey
Kasuku

Wasanifu wanne kati ya wataalamu waliounda mkataba wa Paris wa mwaka 2015, akiwemo mkuu wa zamani wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya mabadiliko ya tabianchi, Christiana Figueres, wamewataka rasmi viongozi wa dunia kupendekeza makubaliano ya kimataifa ambayo ni makubwa na yenye kuleta mabadiliko ya bayoanuwai katika mkutano ujao wa COP15 wa kuhusu bioanuwai. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira UNEP "Ajenda za mabadiliko ya tabianchi na asili vinaingiliana. Ni kwa kuchukua hatua za haraka kukomesha na kubadili upotevu wa maliasili muongo huu, huku tukiendelea kuongeza juhudi za kupunguza kasi ya uchumi wetu, ili tuweze kutumaini kutimiza ahadi ya mkataba wa Paris.” 

UNEP imeendelea kusema kuwa , upotevu wa bayoanuwai tayari una athari kubwa kwa mabadiliko ya tabianchi kwa kikanda na kimataifa. 

Wakati mifumo ya ikolojia ya asili ina jukumu muhimu katika kudhibiti hali ya hewa na inaweza kusaidia kutunza na kuhifadhi hewa ukaa, upotevu wa misitu, kukauka kwa ardhioevu na uharibifu mwingine wa mazingira ulimwenguni kote umechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi. 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasema, juhudi za kupunguza ukataji miti na uharibifu wa misitu na kurejesha mifumo ya ikolojia, kwa mfano, zinaweza kusaidia kupunguza utoaji wa gesi chafuzi kila mwaka. 

Kwa upande wake Inger Andersen, mkurugenzi mtendaji wa UNEP, ameiambia UN News kwamba “Tukiwekeza katika asili na miundombinu ya asili, misitu, miamba ya matumbawe, mikoko, misitu ya pwani, vinatukinga na dhoruba kali. Hii hutoa makazi kwaaina mbalimbali za viumbe, lakini pia huhifadhi hewa ukaa. Kwa hivyo ina mielekeo yote miwili wa kukabiliana na kujenga mnepo.” 

Samaki wakiwa kwenye eneo lenye matumbawe  kwenye bahari ya Pasifiki
Ocean Image Bank/Jayne Jenkins
Samaki wakiwa kwenye eneo lenye matumbawe kwenye bahari ya Pasifiki

Miamba ya matumbawe 

Shirika hilo la mazingira limeendelea kusema kwamba wakati huo huo, viumbe hai huathiriwa na matukio ya hali ya hewa na joto kali, na hasa katika nchi zinazoendelea, kutokana na rasilimali chache za kuzilinda.  

“Hii inatia wasiwasi, kwa kuwa nchi 15 kati ya 17 zenye bayoanuwai kubwa ziko Kusini mwa dunia. Madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa bayoanuwai tayari yanaonekana, hasa wakati aina nyingi za wanyama tayari zikilazimika kubadilisha mwelekeo wao wa uhamaji, mimea inayojitahidi kukabiliana na mabadiliko ya joto na bila shaka, dubu wa polar walio hatarini sana. Pia njaa katika ncha ya Kaskazini kutokana na ukosefu wa barafu ya bahari katika ulimwengu huu wa joto kali.” 

Katika bahari hiyo, wanabiolojia wanashuhudia mkasa mwingine kwani miamba ya matumbawe, ambayo hutoa chakula na makazi kwa zaidi ya viumbe wengine 7,000, yanakufa kutokana na ongezeko la joto na tindikali baharini. 

Kastika mkutano huo wa COP27, balozi mwema wa UNEP Ellie Goulding amezindua mpango mpya wa kulinda miamba hii ya matumbawe.  

Wiki iliyopita, aliongoza msafara katika bahari shamu, karibu na Sharm El-Sheikh. 

"Kuna uzuri wa kuona unapopita huku umevaa kinyago chako na kushuhudia aina hii nzuri ya maisha ya baharini, unahisi kama maisha yote yanaogelea mbele ya macho yako. Na ilinikumbusha kuwa matumbawe hufunika tu asilimia ndogo ya eneo la bahari, lakini ni nyumbani kwa robo ya viumbe vyote vya baharini vinavyojulikana”. 

Bi. Goulding amewakumbusha washiriki kwamba hata kukiwa na ongezeko la joto la nyuzi joto 1.5°C, asilimia 70-90% ya miamba ya matumbawe yote itapotea; idadi hiyo itaongezeka hadi asilimia 99% ikiwa sayari yetu itaendelea kuchemka hadi nyuzi joto 2.0. 

Balozi huo ambaye ni wimbaji na mtunzi wa nyimbo amesema "Ni dhihaka kwamba chini ya asilimia 0.01% ya ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi ndio hutumiwa kulinda miamba ya matumbawe. Ninatoa wito kwa jumuiya ya uongozi wa kimataifa kutambua kwamba miamba ya matumbawe ni mojawapo ya mali yetu kuu ya pamoja na kuwa na nia ya dhati na ya ushindani katika ufadhili, urejeshaji na ulinzi wake.”