Ripoti: Nchi nyingi zinazoendelea hazina sera za kuongoza mipango ya Jiji Mahiri

Mfumo wa barabara kwenye moja ya barabara kuu kwenye mji wa Malindi nchini Kenya. Julai 26, 2022.
UN-Habitat/Julius Mwelu
Mfumo wa barabara kwenye moja ya barabara kuu kwenye mji wa Malindi nchini Kenya. Julai 26, 2022.

Ripoti: Nchi nyingi zinazoendelea hazina sera za kuongoza mipango ya Jiji Mahiri

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Miji inazidi kutumia teknolojia za kidijitali katika utoaji wa huduma za kimsingi kama vile usafiri, nishati, taa za umma, udhibiti wa taka, huduma za afya na nyingine nyingi. Mabadiliko haya ya kidijitali yanayoendelea yanatoa fursa mpya lakini pia huzua changamoto ili kuanzisha kinachojulikana kama Mipango ya Jiji Mahiri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UNHABITAT jijini Nairobi, Kenya na Barcelona Hispania, katika miji mingi hasa yenye kipato cha juu ni jambo la kawaida kuwa na Kitengo cha Jiji Mahiri, mahususi kwa ajili ya uratibu na utekelezaji wa mipango na ufanyaji maamuzi unaotokana na takwimu.

Lakini, utekelezaji na utumiaji wa mifumo ya kisheria na kanuni mahususi kwa mipango mahiri ya jiji ni kazi ngumu kwa manispaa nyingi ulimwenguni. Serikali za mitaa nyingi hazina mawazo yenye mwelekeo wa uvumbuzi na umahiri kwa majiji yao ule unaohitajika ili kudhibiti mageuzi ya kidijitali yenye ufanisi.

Na zaidi ya yote, zaidi ya theluthi mbili ya nchi za kipato cha chini hazina sera za kitaifa ya kuongoza mipango ya miji mahiri.

Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat Maimunah Mohd Sharif amesema “Ninaamini serikali za mitaa zina jukumu muhimu la kutekeleza katika utawala wa miji mahiri na katika kukabiliana na changamoto na hatari za kuongezeka kwa mfumo wa kidijitali katika utoaji wa huduma za umma na athari kama vile mgawanyiko wa kidijitali, ujumuishaji wa kidijitali, na usawa wa kijamii.”

Ripoti mpya ya jiji mahiri

Maelezo hayo yapo kwenye ripoti mpya iliyotolewa leo ambayo imetayarishwa kwa pamoja na UN-Habitat, Benki ya Maendeleo ya Amerika ya Kusini, (CAF), Chuo Kikuu cha Edinburgh Napier, na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tallinn (TalTech).

Ripoti hii ya aina yake iliyopewa jina la Mapitio ya Ulimwenguni kuhusu Mbinu za Utawala Bora wa Jiji ni ripoti ya kwanza kabisa ya kuchunguza jinsi utawala bora wa jiji unavyotafsiriwa na kudhibitiwa katika maeneo yote duniani.

Ripoti hiyo imeleta pamoja uzoefu kutoka kwenye miji 250 ili kutoa mapendekezo muhimu yakimkakati kwa serikali za mitaa wanapopanga, kutekeleza na kudumisha mipango ya jiji bora.

Akizungumzia kilichomo kwenye ripoti hiyo Luca Mora, Profesa wa mijini, Ubunifu na Mkurugenzi wa Maabara ya Sera ya Ubunifu mijini katika Chuo Kikuu cha Edinburgh Napier amesema “Kwenye makutano kati ya teknolojia ya kidijitali na maendeleo ya mijini kuna fursa ya maisha endelevu katika jamii za mijini. Ripoti hii inatoa ushauri wa wazi juu ya jinsi ya kutambua uwezo huu kwa njia inayojumuisha na iliyo endelevu, na mapendekezo ya msingi ya ushahidi ambayo yanaweza kutoa taarifa ya juhudi zozote za kubadilisha teknolojia za jiji kuwa na nguvu ya mustakabali endelevu wa mijini.”

Kwa upande wake Meneja wa Mabadiliko ya Miundombinu na Digital kutoka Benki ya Maendeleo ya Amerika ya Kusini, Antonio Silveira, amesema kuwa “Katika Amerika ya Kusini na Karibiani, eneo lenye miji inayoendelea zaidi duniani, usimamizi mzuri wa jiji ni kipengele muhimu katika kuboresha maisha ya watu. Kwa kazi hii, tunatarajia kuchangia katika mjadala kuhusu masuala ya maendeleo jumuishi ya miji na kueneza mipango bunifu inayolenga kuimarisha usimamizi makini wa miji.”

 

Mengine yaliyotolewa katika ripoti ni pamoja na:

  1. Zaidi ya theluthi mbili ya miji katika nchi zenye kipato cha chini hazina sera za kitaifa za kuongoza mipango ya miji mahiri.
  2. Asilimia 64 ya miji ya Afrika inataja ukosefu wa ujuzi kama sababu kuu inayozuia mipango yao ya miji mahiri ikilinganishwa na miji katika mabara mengine.
  3. Uendelevu wa muda mrefu wa mipango mahiri ya mijini umechukuliwa kama jambo kuu duniani kote, huku kukiwa na matukio mengi zaidi barani Afrika na Amerika Kaskazini.
  4. Kanuni za ununuzi wa umma na udhibiti mkali wa urasimu zimesalia kuwa kikwazo katika ushirikiano wa washirika wa nje katika mipango mahiri ya jiji, hasa Amerika ya Kusini na Amerika Kaskazini.
  5. Ni vigumu kwa serikali za manispaa duniani kote kuhakikisha ushiriki wa wakazi katika mipango mahiri ya jiji. Hii inazua wasiwasi kuhusu juhudi za kuifanya miji mahiri kuwa ya watu zaidi.

 

Ripoti kamili ya :  Global Review of Smart City Governance Practices itazinduliwa kesho (15 Novemba ) kwenye mkutano wa Dunia wa Smart City Expo huko Barcelona.