Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Hatutaki ukoloni kupitia mafuta ya Kisukuku" Wanaharakati kutoka Afrika:

Wanaharakati vijana katika COP27 huko Sharm El-Sheikh wakitaka mataifa yaliyoendelea 'kulipia' hasara na uharibifu kutokana na mabadiliko ya tabianchi..
Johann Olivier
Wanaharakati vijana katika COP27 huko Sharm El-Sheikh wakitaka mataifa yaliyoendelea 'kulipia' hasara na uharibifu kutokana na mabadiliko ya tabianchi..

"Hatutaki ukoloni kupitia mafuta ya Kisukuku" Wanaharakati kutoka Afrika:

Tabianchi na mazingira

Wakulima wadogo kutoka nchi zinazoendelea wanazalisha thuluthi moja ya chakula duniani, lakini wanapokea asilimia 1.7 tu ya fedha za tabianchi hata kama wanalazimika kukabiliana na ukame, mafuriko, vimbunga na majanga mengine.

Hisia hii imedhihirika katika mabanda kadhaa na vyumba vya mikutano huko Sharm el-Sheikh siku ya Jumamosi wakati COP27 ilipoelekeza maudhui yake kwenye suala muhimu la kukabiliana na ukame, kilimo na mifumo ya chakula katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Sabrina Dhowre Elba, Balozi mwema Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), alisema "Tunahitaji kusaidia wakazi wa vijijini kujenga uwezo wao wa kukabiliana na hali mbaya ya hewa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. La sivyo, tunakuwa tunatoka kwenye shida moja hadi nyingine. Wakulima wadogo wanafanya kazi kwa bidii kulima chakula kwa ajili yetu katika mazingira magumu,”

Kama mwanamke wa Kisomali, Bi. Dhowre Elba alisema suala hili lilikuwa la kibinafsi: wakati COP27 ikiendelea nchi yake ina misimu minne bila ya mvua mfululizo, tukio la hali ya hewa ambalo halijaonekana kwa miaka 40.

"Siwezi kusimama bila kufanya kitu wakati akina mama, familia na wakulima wanateseka. Katika Pembe ya Afrika kunakabiliwa na ukame mkubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni," alielezea, akizitaka nchi zilizoendelea kuhamasisha utashi wa kisiasa na uwekezaji.

"Matrilioni ya dola yalipatikana ili kukabiliana na janga la coronavirus">COVID-19 na athari zake za kiuchumi. Vile vile vinahitajika kwa mabadiliko ya tabianchi. Vile vile zinahitajika kwa msaada endelevu wa kilimo. Ni muhimu kwa ustawi na uhakika wa chakula kwetu sote,” aliongeza.

Wakulima katika magharibi mwa Nepal wanajifunza jinsi ya kukabiliana na jotokali na mifumo tofauti ya mvua.
© CIAT/Neil Palmer

Fedha za kurekebisha lazima ziwasilishwe

Dina Saleh, Mkurugenzi wa Kanda wa IFAD, alielezea kuwa kushindwa kuwasaidia wakazi wa vijijini kukabiliana na hali hii mbaya kunaweza kuwa na matokeo ya hatari, na kusababisha umaskini mrefu, watu kuyakimbia makazi yao na migogoro.

"Hii ndiyo sababu leo ​​tunatoa wito kwa viongozi wa dunia kutoka mataifa yaliyoendelea kuheshimu ahadi yao ya kutoa dola bilioni 100 kwa mwaka katika ufadhili wa tabianchi kwa mataifa yanayoendelea na kuelekeza nusu ya hicho kiasi kwenda kukabiliana na tabianchi," alisisitiza.

Miaka kumi na tatu iliyopita, katika COP15 Copenhagen, mataifa yaliyoendelea yalitoa ahadi muhimu. Waliahidi kuelekeza dola bilioni 100 kwa mwaka kwa mataifa yanayoendelea ifikapo 2020, ili kuwasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza ongezeko zaidi la joto. Ahadi hiyo, hata hivyo, haikutekelezwa.

Bi. Saleh alionya kwamba kuna "dirisha nyembamba" la kusaidia watu maskini wa vijijini kuishi na kulinda jamii zao, na kwamba mavuno ya mazao yanaweza kupungua kwa asilimia 50 kufikia mwisho wa karne.

"Chaguo ni kati ya kuzoea au kufa njaa," alionya, akihimiza COP27 iwe juu ya hatua, uaminifu na haki kwa asiyeonekana na kimya.

 

Mpango mpya

Ili kushughulikia maswala haya, Urais wa COP27 wa Misri ulizindua Ijumaa (10 Novemba 2022) mpango mpya wa Chakula na Kilimo kwa Mabadiliko Endelevu au FAST, ili kuboresha idadi na ubora wa michango ya tabianchi ili kubadilisha kilimo na mifumo ya chakula ifikapo 2030.

Mpango wa ushirikiano utakuwa na mambo madhubuti yanayoweza kutolewa kwa ajili ya kusaidia nchi kupata fedha na uwekezaji kuhusu tabianchi, kuongeza maarifa, na kutoa usaidizi wa kisera na mazungumzo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, watakuwa wawezeshaji wa mpango huu, ambao kwa mujibu wa Zitouni Ould-Dada, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa na Mazingira wa shirika hilo, anaweka kilimo katika msingi wa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

"Ujumbe kwa kweli ni kutambua kwamba kilimo lazima kiwe sehemu muhimu ya suluhisho la mzozo wa tabianchi," aliiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Mboga zikiandaliwa wakati wa mafunzo kwa wakulima huko Taita nchini Kenya
© FAO/Fredrik Lerneryd
Mboga zikiandaliwa wakati wa mafunzo kwa wakulima huko Taita nchini Kenya

Umuhimu wa kuwekeza katika uvumbuzi

Wakati huo huo, wakati sekta ya kilimo na chakula inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi, pia inachangia karibu theluthi moja ya uzalishaji wa hewa chafu duniani, kutoka kwa uzalishaji hadi matumizi, Ould-Dada anaelezea, akisema kwamba lazima kuwe na mabadiliko ya mifumo ya kilimo chakula.

"Hatuwezi kuendelea na mtindo wa sasa wa kuzalisha chakula na kisha kuharibu udongo, kupungua kwa viumbe hai, kuathiri mazingira. Hapana. Ni lazima kiwe endelevu,” anabainisha.

Mtaalam huyo anaangazia kwamba ikiwa uchaguzi sahihi utafanywa, kilimo kinaweza kuwa sehemu muhimu ya suluhu la kukabiliana na mzozo wa tabianchi kwa kunyakua kaboni kwenye udongo na mimea na kukuza kukabiliana na hali hiyo na ustahimilivu.

"Hatuwezi kuzalisha chakula cha kulisha na kulisha idadi ya watu inayoongezeka kwa mtindo wa sasa, na tishio la mabadiliko ya tabianchi. Hatuwezi.”

Jambo la kwanza ambalo ulimwengu unapaswa kukabiliana nalo, anasema, ni kushughulikia upotevu wa chakula, ambao unawajibika kwa asilimia 8 ya utoaji wa gesi duniani.

"Tuna karibu watu milioni 828 ambao wana njaa kila siku. Na bado, tunatupa theluthi moja ya chakula tunachozalisha kwa matumizi ya binadamu. Tunahitaji kubadilisha mawazo yetu, mtindo wetu wa uzalishaji, ili tusipoteze na kupoteza chakula, "anasisitiza.

Anaongeza kuwa katika suala la suluhisho, kutumia nguvu ya uvumbuzi ni muhimu ili kupunguza uzalishaji, kusaidia kukabiliana na kilimo na hali ya hewa inayobadilika, na kuifanya iwe sugu zaidi dhidi ya shida, sio tu inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, lakini pia na milipuko au vita, kama hali ya sasa ya Ukraine.

"Uvumbuzi kwa maana pana kama kilimo cha usahihi ambapo una umwagiliaji wa matone pamoja na nishati mbadala ili uwe na ufanisi. Lakini pia, uvumbuzi unaotumia ujuzi wa jadi wa wakulima wadogo pia ni muhimu, kwa sababu unafanyika kila wakati,” Ould-Dada alisisitiza.

Wanaharakati wafanya maandamano makubwa katika COP27 huko Sharm El-Sheikh wakiwataka viongozi kufanya zaidi kushughulikia masuala muhimu yanayohusu kilimo, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kustahimili hali ya hewa.
Laura Quinones
Wanaharakati wafanya maandamano makubwa katika COP27 huko Sharm El-Sheikh wakiwataka viongozi kufanya zaidi kushughulikia masuala muhimu yanayohusu kilimo, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kustahimili hali ya hewa.

‘COP huyu amepotea na kuharibiwa’

Wakati huo huo, mwanaharakati mashuhuri wa Nigeria Nnimmo Basse alisema kuwa COP27 "ilipotea na kuharibiwa" kwa kuruhusu wachafuzi wa mazingira wakubwa kushiriki.

"Afrika inashambuliwa hivi sasa. Makampuni ya uchimbaji madini na mafuta na gesi yanazamisha mashine zao chafu katika bara zima na kuharibu, kuua, kuiba. Huu ndio aina ya ukoloni ambao hauwezi kuvumiliwa”, alisema, muda mfupi kabla ya kuhamasisha wimbo wa "Hatutaki ukoloni kupitia mafuta ya kisukuku" miongoni mwa washiriki.

Basse alisema ikiwa nchi zinaweza kutumia dola trilioni mbili kwa mwaka kwa vita, kuharibu na kuua, zinaweza kuzitumia katika kulipia ustahimilivu.

"Hatuombi mdola bilioni 100 moja. Hatuulizi dola bilioni 200. Tunaomba deni ambalo tunalodai lazima lilipwe. Lipa deni la tabianchi,” aliwaambia viongozi wa dunia.

 

Mashirika ya kiraia yanataka fedha, mabadiliko ya uchumi

Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa hawakuwa pekee waliosisitiza haja ya nchi kuwekeza katika mabadiliko na kutoa ahadi zao za ufadhili wa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Maandamano makubwa yaliyoongozwa na muungano wa mashirika ya mazingira, wanawake, wazawa, vijana na vyama vya wafanyakazi yalitapakaa kwenye barabara na njia kati ya mabanda kwenye COP27.

“Haki ya maeneo, haki za rasilimali, haki za binadamu, haki za watu wa kiasili, hasara na uharibifu lazima ziwe katika maandishi yote ya mazungumzo…. 1.5 haiwezi kujadiliwa ndivyo tuko hapa,” alisema Hindou Oumarou Ibrahim, mwanamazingira kutoka nchini Chad na mtetezi wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDG.

Mwanaharakati huyo alisema kuwa watu wake wanakufa kwa sababu ya mafuriko, ukame, huku baadhi ya jamii za kiasili katika Pasifiki zikipoteza makaazi yao.

“Tunataka tuwe na haki. Haki kwa watu wetu, kwa uchumi wetu kwa hasara na uharibifu. Tunapoteza tamaduni zetu, utambulisho wetu, maisha yetu, na haya hayalipwi, lakini ufadhili wa athari za mabadiliko ya tabianchi unahitaji kutolewa," alifoka huku kukiwa na mamia ya waandamanaji.

 

Marekani inasema iko tayari kusaidia hasara na uharibifu

Baadaye siku ya Jumamosi, John Kerry, Mjumbe Maalumu wa Marekani wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, aliuambia mkutano na waandishi wa habari kwamba nchi yake "inaunga mkono kikamilifu" msukumo wa kushughulikia hasara na uharibifu, suala lenye mwiba hadi sasa katika mazungumzo ya COP27.

"Tumeshirikiana na marafiki zetu kufanyia kazi mapendekezo hayo," aliongeza, akisisitiza kwamba Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye mashirika yasiyo ya kiserikali yalimtaja Ijumaa kwa kutotaja hasara na uharibifu katika hotuba yake katika COP27, pia anaunga mkono hatua hiyo.

Kikundi cha mazungumzo cha 77 na China, ambacho kimsingi kinajumuisha nchi zote zinazoendelea, kiliweza kwa mara ya kwanza kuweka suala hilo kwenye ajenda ya COP mwaka huu.

Wazo ni kuunda wa kituo cha kifedha cha hasara na uharibifu ambacho kinaweza kutoa fidia ya fedha kwa mataifa yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi, lakini kwa uwajibikaji mdogo wa uzalishaji wa hewa chafuzi.