Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata kulazimu WFP kusitisha misaada kwa wakazi milioni 1 Cabo Delgado

Huko Cabo Delgado nchini Msumbiji kuna wanufaika wapato 10,000 ambao wanapata misaada kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo WFP, UNICEF na IOM
Lucio Melandri /UNICEF Mozambique
Huko Cabo Delgado nchini Msumbiji kuna wanufaika wapato 10,000 ambao wanapata misaada kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo WFP, UNICEF na IOM

Ukata kulazimu WFP kusitisha misaada kwa wakazi milioni 1 Cabo Delgado

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP linasema iwapo halitapokea fedha za nyongeza, litalazimika kusitisha msaada muhimu wa kibinadamu kwa wakazi milioni moja wa jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji ifikapo kilele cha msimu wa njaa mwezi Februari mwakani kutokana na ukata unaokabili.

Antonella D’Aprile ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Msumbiji amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo ya kwamba Cabo Delgado ni jimbo la Msumbiji lisilo na uhakika wa chakula na uhakika wa chakula unadorora kila uchao, huku takribani watu milioni 1.15 jimboni humo wakiwa kwenye janga au udharura wa njaa, huku takwimu mpya zaidi zikionesha hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Ghasia zimeshamiri miezi ya karibuni, mashambulizi karibu na Pemba, mji mkuu wa Cabo Delgado pamoja na jimbo Jirani la Nampula, yamelazimu watu wengi zaidi kukimbia vijiji vyao, idadi ya wakimbizi wa ndani imeongezeka mara nne na kufikia milioni moja katika miaka miwili iliyopita.

Licha ya ghasia hizo, Bi. D’Aprile amesema WFP imeendelea kusambaza misaada ya dharura, vyakula vyenye lishe kwa wajawazito na watoto, pamoja na miradi ya kujengea mnepo jamii zilizo hatarini, wakiwemo watu 44,000 kupata ardhi yao huko Cabo Delgado

Halikadhalika WFP inaendesha shirika la huduma za ndege la Umoja wa Matiafa, UNHAS ambalo ndilo pekee linalosafirisha wahudumu wa kibinadamu kuelekea maeneo yasiyofikika kwa barabara.

Mkuu huyo wa WFP nchini Msumbiji amesema katika maeneo ya ndani kabisa, UNHAS ndio huduma pekee ya anga kwa wahudumu wa misaada na kwamba “mwezi Desemba mwaka 2020, kufuatia kushamiri kwa mapigano na janga la coronavirus">COVID-19, WFP ilifungua njia ya anga ya kuunganisha maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji yasiyofikika. Huduma hii ya anga imesafirisha zaidi ya watumishi wa kibinadamu 10,000, na kilo 70,000 za misaada ya kibinadamu sambamba na huduma 330 za kiusalama.”

Amesema kutokana na ukata huduma zote hizo zinaweza kusitishwa iwapo hawatopata dola milioni 51.

Amesisitiza kuwa wakati wanatoa ombi la usaidizi huo, wataendelea kujitahidi kusambaza huduma kwa makundi yaliyo hatarini zaidi kama wenye utapiamlo uliokithiri, wajawazito na wanawake wanaonyonyesha watoto, lakini kuna baadhi ambao itabidi washindwe kuwahudumua labda kupatikane fedha za ziada.