Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Ufadhili kifedha COP27: Kifaa kipya cha kubaini nani anatoa hewa chafuzi na nishati ya mafuta kisukuku vyamulikwa

Maandamano kupinga nishati ya mafuta kisukuku huko Sharm el-Sheikh nchini Misri wakati wa COP27
UN News/Laura Quinones
Maandamano kupinga nishati ya mafuta kisukuku huko Sharm el-Sheikh nchini Misri wakati wa COP27

Siku ya Ufadhili kifedha COP27: Kifaa kipya cha kubaini nani anatoa hewa chafuzi na nishati ya mafuta kisukuku vyamulikwa

Tabianchi na mazingira

Siku ya tano ya mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP27 huko Sharm el-Sheikh nchini Misri imeendelea kwa maudhui yaliyolenga ufadhili na uchangishaji fedha kwa ajili ya miradi ya hatua kwa tabianchi.

Lengo ni kuhakikisha kuna msukumo wa kimataifa wa kuelekeza upya mamia ya mabilioni ya dola zinazowekezwa kila mwaka katika nishati ya mafuta kisukuku sasa ziende kusaidia kufadhili mipango inayoongozwa na jamii ya nishati mbadala.

Zaidi ya wanaharakati 50 wa kila rika na asili walilizingira 'Eneo la Bluu' ambalo ni eneo kuu la kituo cha mikutano huko Sharm el-Shaik nchini Misri linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa huku wakaiimba “Komesha ufadhili wa nishati ya mafuta kisukuku! Acha kufadhili kifo!”.

Susan Huang, anayewakilisha shirika lisilo la kiserikali la Oil Change International alikuwa miongoni mwa washiriki wanaolenga kuangazia ukweli kwamba nchi tajiri, kama ilivyobainishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antoni Guterres mapema wiki hii, bado zinatoa fedha kwenye nishati ya mafuta ya kisukuku wakati ambapo dunia inahitaji kuwa na mpito tena kwa haraka kuelekea kwenye nishati mbadala.

“Katika mkutano wa viongozi wa kundi la nchi saba tajiri duniani, G7 mwaka jana wa 2021, kulikuwa na makubaliano ya kukomesha fedha za umma kutumika kwenye nishati ya kisukuku kufikia mwisho wa mwaka huu. Lakini Wakala wa Kimataifa wa Nishati umejitokeza na kusema kwamba kwa kweli mabadiliko yanayofanyika kwa polepole kwenda kwenye matumizi ya nishati mbadala ndiyo yanazidisha mzozo wa mabadiliko ya tabianchi na shida ya nishati. Kwa hivyo, tunawahimiza viongozi wa dunia kutimiza ahadi zao na kuacha kutumia fedha za umma kwa ajili ya nishati ya mafuta ya kisukuku, "aliambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Maji katika ziwa Albert nchini Uganda yanazidi kuongezeka na kusababisha nyumba hasa katika wilaya ya Buliisa kutwama.
UN/John Kibego
Maji katika ziwa Albert nchini Uganda yanazidi kuongezeka na kusababisha nyumba hasa katika wilaya ya Buliisa kutwama.

Huang alisema kuwa uwekezaji huu pia unasababisha uharibifu wa ajabu, unaharibu viumbe hai na kuharibu maisha duniani kote.

Hakuwa peke yake: Dipti Bhatnagar, kutoka shirika la  Friends of the Earth International nchini Msumbiji, alitoa hotuba ya kusisimua ambayo iliwafanya watu wengi kutikisa vichwa na huku kukiwa na minong’ono ya kukubaliana waziwazi kati ya wale wote waliokuwa wakiingia kwenye uwanja mkuu wa mkutano huo kukubaliana na alichokuwa akisema, “nchi tajiri ziko tayari kunyakua hifadhi kubwa ya gesi, na watu wananyang'anywa ardhi yao. Watu milioni moja kati ya milioni 23 [ya wakazi wa Msumbiji] wanaishi katika kambi za wakimbizi kwa sababu ya gesi. Tunasema hapana kwa fedha zaidi za gesi. Hatutaacha Afrika iungue,” alifoka.

Wanaharakati hao walisema wazi kwamba njia bora ya kuongeza upatikanaji wa nishati duniani kote na kukidhi mahitaji ya walio hatarini zaidi, ni kwa kuwekeza katika mipango ya nishati mbadala inayoungwa mkono na jumuiya.

“Mipango ya nishati inayoweza kudhibitiwa na kuendeshwa na watu katika jamii,” Bi. Huang alieleza.

Chombo kipya cha akili bandia kinachoweza kuwawajibisha wachafuzi

Kutoka kwenye eneo la Buluu mabanda mawili pembeni yake kulikuwa na banda jingine na huko Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alishiriki na alitoa wito kwa serikali na sekta ya fedha zinazoendelea kuwekeza katika nishati ya mafuta.

António Guterres alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa ubunifu mpya huru unaoangalia uzalishaji wa gesi chafuzi, ubunifu huo umeundwa na Muungano wa kufuatilia mabadiliko ya tabianchi CLIMATE TRACE COALITION na unaongozwa na Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Al Gore.

Al Gore akiwa COP27 Sharm el-Sheikh wakati akizindua kifaa au mbinu ya kufuatilia watoaji hewa chafuzi .
UNIC Tokyo/Momoko Sato
Al Gore akiwa COP27 Sharm el-Sheikh wakati akizindua kifaa au mbinu ya kufuatilia watoaji hewa chafuzi .

Ubunifu huu unachanganya taarifa zilizopatikana kwenye satelaiti na akili bandia ili kuonyesha kiwango cha utoaji wa hewa chafuzi na utaangalia zaidi ya maeneo 70,000 duniani kote, ikiwa ni pamoja na makampuni nchini China, Marekani na India. Hii itawawezesha viongozi kujua eneo na upeo wa utoaji wa hewa chafu unaotolewa.

Guterres alieleza kuwa takwimu zilizotolewa na mpango huo zinaonyesha kuwa kwa sababu ya kutoripoti uvujaji wa hewa chafuzi ina ya methane, kuwaka moto, na shughuli nyingine zinazohusiana na uzalishaji wa mafuta kisukuku na gesi, uzalishaji wa gesi hizo mara nyingi ni zaidi ya ilivyoripotiwa hapo awali.

"Hii inapaswa kuwa wito wa kuamsha serikali na sekta ya fedha, hasa zile zinazoendelea kuwekeza na kudhibiti uzalishaji wa mafuta," aliwaambia wahudhuriaji wa COP27.

Gharama kubwa za majanga

Uwasilishaji wa orodha wasilianifu isiyo na kifani, ambayo sasa iko mtandaoni, ilimfanya Al Gore kukimbia huku na huko na kuendelea kubofya  taarifa yake aliyokuwa akiwasilisha inayoonesha kila ukurasa uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kote ulimwenguni.

Bwana Gore ambaye ni mwandishi mashuhuri wa Ukweli usiopingika na ambaye anajulikana tangu mapema kabisa kuwa ni mmoja wa watetezi wa mapema wa hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, alicheza video ya bomu la atomiki likilipuka kwenye runinga kubwa ya inchi 360 karibu na kikao. Sauti hiyo iliwaacha wahudumu wakiwa na wasiwasi, lakini wakitaka kujua nini kinaoneshwa.

Alitaka kuangazia ukweli alioshiriki hapo awali katika ufunguzi wa Mkutano wa Viongozi wa Dunia wa COP27: uchafuzi wa gesi chafuzi unaokusanywa katika angahewa yetu hunasa joto la ziada kama vile mabomu 600,000 ya atomiki yanayolipuka kila siku.

“Miezi miwili iliyopita mnamo Septemba 2020, kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu alituambia kuhusu mawimbi ya joto barani Ulaya, mafuriko nchini Pakistani, ukame mkubwa ... na aliunganisha yote kwa usahihi kama bei ya uraibu wa binadamu wa mafuta,” aliwakumbusha wajumbe.

Gore alisema kuwa majanga haya kwa sasa yanagharimu uchumi wa dunia dola trilioni mbili na nusu kila mwaka.

Hata hivyo, alisema, dunia iko katika hatua ya mwisho ya mabadiliko kwa sababu masuluhisho yapo yakusaidia kugeuza hali hii (ya athari za mabadiiko ya tabianchi) na kuongeza uwekezaji katika bidhaa jadidifu.

Ufuatiliaji wa tabianchi
© Climate Trace
Ufuatiliaji wa tabianchi

Umuhimu wa chombo kipya

Bwana Gore aliendelea kubainisha kuwa wakati ufadhili na ruzuku kwa nishati ya mafuta ni "wendawazimu", uwezekano wa ufadhili wa nishati mbadala barani Afrika unapuuzwa na hakuna ufikiaji wowote wa ufadhili kwa bara hilo.

"Uwezo wa upepo na jua ni mara 400 zaidi ya hifadhi ya jumla ya mafuta ya Afrika na inakuja bila uchafuzi wa mazingira na kuzalisha ajira zaidi, lakini kuna pengo la kifedha…Ndiyo maana katika COP hii kuna umakini mkubwa katika kubadilisha  mfumo wa ufadhili mkuu wa kimataifa,” alisisitiza.

Kisha akaeleza kwamba hesabu ya Climate TRACE, ambayo inachanganya takwimu za kuaminika na zilizothibitishwa kutoka kwenye taasisi zaidi ya 100 na vitambuzi 30,000, inaweza kusaidia Serikali kuweka malengo kwenye vitendo wanavyofanya.

"Inafanya kutowezekana kwa watoa hewa chafuzi kudanganya," alielezea na kufichua kwamba kwa sasa, vyanzo 14 vya juu vya uzalishaji wa hewa chafu duniani ni maeneo ya mafuta na gesi.

"Mojawapo ya utambuzi wa mapema zaidi kutoka kwa kazi hii ni kiwango cha uzalishaji wa mafuta na gesi  haswa zile ambazo hazijaripotiwa hapo awali," Bwana Guterres alisema, akiita takwimu hiyo "chanzo muhimu" cha juhudi za habari kushughulikia dharura ya mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa chombo hicho kipya kitakuwa muhimu kwa viongozi wa makampuni ya biashara wanaofanya kazi ya kuondoa minyororo ya kaboni wanapofanya ugavi, kwa serikali zinazofanya kazi kuoanisha utungaji sera na mipango yao ya mabadiliko ya tabianchi, na kwa wawekezaji wanaofanya kazi kufuatilia maendeleo ya sekta binafsi hadi kufikia sifuri halisi.

"Tatizo ni kubwa zaidi kuliko vile tulivyoaminishwa na hiyo inamaanisha ni lazima tufanye kazi kwa bidii zaidi ili kuharakisha uondoaji wa nishati zote za mafuta", alionya.

Taarifa zaidi za kifedha kwenye COP27

Siku hii maalum ya kujadili masuala ya ufadhili katika COP27 ilionesha kwamba uwekezaji wa thamani wa matrilioni ya dola unahitajika kila mwaka ili kufikia mabadiliko ya haraka na makubwa yanayohitajika kushughulikia athari za mzozo wa mabadiliko ya tabianchi, na kutimiza malengo ya Mkataba wa Paris.

Katika vyumba mbalimbali vya mikutano, mabanda na 'vituo vya vitendo', na katika mazungumzo ya faragha, wajumbe, wanaharakati, mabenki ya uwekezaji, na wadau wengine walijadili umuhimu wa kuziba pengo la sasa la fedha katika maeneo muhimu ya hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, pamoja na marekebisho na hasara na uharibifu ambao umeshatokea.

Wataalamu walikubali kwamba msukumo wa kifedha lazima utoke kwa sekta zote, za umma au za kibinafsi, deni au usawa, za kibiashara au za uhisani.

"Fedha ndio suluhu kubwa zaidi linaloweza kuchochea hatua kila mahali", Anjali Viswamohanan, mkurugenzi wa sera katika Kundi la Wawekezaji la Asia, aliiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Moja ya wito mkubwa ulikuwa kufunga "pengo la kukabiliana na athari". 

Kwa mujibu wa Sekretarieti ya Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi , (UNFCCC), waendelezaji wa mradi na wawekezaji lazima wazingatie kuandaa na kuwekeza katika miradi inayojenga ustahimilivu na kulinda walio hatarini kutokana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi; kuendesha mabadiliko ya kimfumo na uvumbuzi kwa ajili ya mabadiliko ya kaboni, mabadiliko yanayostahimili hali ya hewa katika muktadha wa mpito tu; na kulinda na kurejesha hali ilivyokuwa hapo awali kabla ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Rasilimali fedha na uwekezaji bora ni muhimu ili kufanikisha hatua sahihi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
© Unsplash/Micheile
Rasilimali fedha na uwekezaji bora ni muhimu ili kufanikisha hatua sahihi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Ahadi na mipango zaidi

Mpaka kufikia hii leo jumatano , ahadi zilizotolewa zimefika jumla ya dola milioni 20, New Zealand iliongezeka kwenye orodha, pamoja na Scotland, Norway, Ujerumani, Austria, na Ubelgiji, ya wale ambao wameahidi fedha kwa ajili ya masuala la hasara na uharibifu (malipo kwa ajili ya kuendeleza nchi zinazotoa kaboni kidogo lakini zimeathiriwa na kuna maafa kutokana na mabadiliko ya tabianchi).

Wakati huo huo, Uingereza ilisema kuwa itaruhusu kuahirishwa kwa malipo kwa nchi zilizokumbwa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.

Kituo cha Hatari ya Hali ya Hewa barani Afrika, mpango wa Azimio la Nairobi kuhusu Bima Endelevu, pia ulizinduliwa, na watia saini wakijitolea kutoa dhamana ya dola bilioni 14 kwa hatari za mabadiliko ya tabianchi ifikapo 2030.

Mjumbe wa Maalum wa Marekani kuhusu mabadiliko ya tabianchi John Kerry, pia alifanya tukio katika COP27 akitangaza mipango ya makampuni "kununua mikopo ya hewa ya kaboni" na kusaidia nchi zinazoondokana na makaa ya mawe.

Chini ya mpango uliopendekezwa, unaoitwa Kichochezi cha Mpito wa Nishati, mashirika ya serikali yanaweza kupata mikopo ya kaboni kwa kupunguza utoaji wao ikiwa watapunguza matumizi yao ya nishati ya mafuta na kuongeza matumizi ya nishati mbadala.

Vijana hawataki ahadi hewa

Kwa kuzingatia hilo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa UNICEF, mwanaharakati kijana wa Ujerumani Luisa Neubauer alituma ujumbe mzito kwa viongozi wa dunia wanaotoa ahadi katika COP27:

"Usije hapa na kuzungumza juu ya hatua za mabadiliko ya tabianchi kwakuwa ni mradi tu unashiriki katika miundombinu yoyote mpya ya mafuta ulimwenguni kote. Usije hapa na kuzungumza juu ya haki ya hali ya hewa kwani ufadhili wa mafuta ya visukuku unalipuka. Usije hapa kujaribu kutueleza kuwa fedha zinaweza kuwa kidogo kwa marekebisho na hasara na uharibifu wakati uwekezaji wa mafuta ya kisukuku kote ulimwenguni unaongezeka, siku baada ya siku ".