Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi yawafanya vijana Afrika kutafakari upya kuwa na watoto: UNICEF   

Kundi la vijana maripoti wa U-Reporter nchini Cote D'Ivoire. U- Report ni jukwaa la kijamii la vijana lililoundwa na UNICEF na linapatikana Facebook, Twitter na SMS na linawapatia vijana fursa ya kutoa maoni yao kwa lengo la kuleta mabadiliko.
© UNICEF/Frank Dejongh
Kundi la vijana maripoti wa U-Reporter nchini Cote D'Ivoire. U- Report ni jukwaa la kijamii la vijana lililoundwa na UNICEF na linapatikana Facebook, Twitter na SMS na linawapatia vijana fursa ya kutoa maoni yao kwa lengo la kuleta mabadiliko.

Mabadiliko ya tabianchi yawafanya vijana Afrika kutafakari upya kuwa na watoto: UNICEF   

Tabianchi na mazingira

Takriban nusu ya vijana barani Afrika wamesema wanafikiria upya suala la kupata watoto ama la kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kwa mujibu wa ripoti mpya ya matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF bakwa kuwahoji watu 243,512 duniani kote. 

Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa leo kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP27 unaondelea huko Sharm el-Sheikh Misri, duniani kote vijana 2 kati ya 5 wamesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimewafanya kufikiria upya hamu yao ya kuanzisha familia.  

“Wasiwasi huu umekuwa mkubwa zaidi katika kanda za Afrika, huku asilimia 44 ambayo ni kubwa ya vijana walioripoti kwamba wanafikiria upya kupata watoto wanapatikana Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini na asilimia 43 kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.” 

Kura hiyo ya maoni ya UNICEF imedhihirisha kuwa vijana katika kanda hizo nbili wameripoti kukumbwa na mshtuko na atharin za mabadiliko ya tabianchi, zaidi ya vijana wengine ulimwenguni, wakisema majanga haya yameathiri upatikanaji wao wa chakula na maji, pamoja na mapato ya familia zao. 

Paloma Escudero mkuu wa ujumbe wa UNICEF kwenye mkutano wa COP27 amesema "Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatukabili sasa, lakini ni nyingi zaidi kuliko mafuriko, ukame na ongezeko la joto. Zimeenda mbali zaidi hadi kwenye hisia zetu za matumaini, hasa barani Afrika, vijana wanashuhudia athari za changamoto hizi kwao wenyewe na wale wanaowapenda na inabadilisha mipango yao ya siku zijazo. Lakini si lazima kufanya hivyo, katika mkutano huu wa COP27, viongozi wa dunia lazima wasikilize hofu hizi kutoka kwa vijana na kuchukua hatua mara moja ili kuwalinda.” 

 Mwaka jana, uchunguzi uliochapishwa na jarida la afya la Uingereza The Lancet uligundua kuwa asilimia 39% ya watu 10,000 waliohojiwa duniani walionyesha kusita kupata Watoto ambacho ni kiwango sawa na kura ya maoni ya UNICEF ya kuhusu vijana.  

Wakati mfumo wa UNICEF ni wa kutumia sampuli ya uwakilishi, jukwaa la U-Ripoti, pamoja na mtandao wake mpana wa vijana barani Afrika, linaaminika kuwa la kwanza kuonyesha kusambaa kwa mtazamo huu barani Afrika. 

Matokeo mengine ya kura hiyo ya maoni yameonyesha kuwa "duniani kote zaidi ya nusu ya vijana walioshiriki kura hiyo wamesema wameathiriwa kwa kiasi Fulani na ama ukame au joto la kupindukia." 

Mtu 1 kati ya 4 pia ameathirika na uchagfuzi wa hewa huku idadi kama hiyo pia wameathirika na mafuriko wakati mtu 1 kati ya 6 wamekumbwa na vimbunga na wengine 1 kati ya 10 wameshapitia athari za moto wa nyika.