Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi hewa na ulaghai wa kampuni kuhusu hatua kwa tabianchi vikome – Katibu Mkuu UN

Sayari badala ya Faida! Ndio kauli mbiu inayotumiwa na waandamanaji wakiwa wanataka viongozi waweke sayari mbele badala ya faida.
© Unsplash/Markus Spiske
Sayari badala ya Faida! Ndio kauli mbiu inayotumiwa na waandamanaji wakiwa wanataka viongozi waweke sayari mbele badala ya faida.

Ahadi hewa na ulaghai wa kampuni kuhusu hatua kwa tabianchi vikome – Katibu Mkuu UN

Tabianchi na mazingira

Ingawa serikali nyingi na kampuni zinatoa ahadi za kudhibiti utoaji wa hewa chafuzi sambamba na mikakati ya kufyonza ile inayozalishwa, vigezo vya kuzingatia ahadi hizo vina upenyo mkubwa na mpana wa kuwezesha ahadi hizo kutotekelezwa, amelalama hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati huu ambapo jopo maalum alilounda kuhusu tabianchi likichapisha ripoti iliyofuatilia ahadi hewa za kudhibiti utoaji hewa chafuzi. 

Ripoti hiyo inaponda tabia za baadhi ya kampuni, viwanda, miji, taasisi za kifedha na kanda kujitangaza kuwa zinatekeleza hatua za kukabili na kuhimili mabadiliko ya tabianchi ilihali ukweli halisi si hivyo na badala yake ni kulaghai umma.  

Kwa mujibu wa wataalamu hao, watendaji hawawezi kujinasibu kuwa hewa chafuzi wanayozalisha inafyonzwa ili kuhakikisha hakuna hewa chafuzi angani, wakati watendaji hao hao wanaendelea kujenga au kuwekeza kwenye nishati kisukuku au shughuli zingine zozote zinazoharibu mazingira. 

“Hawawezi pia kushiriki wao wenyewe au wadau wao kushiriki kwenye harakati dhidi ya mabadiliko ya tabianchi au kutoa ripoti ya shughuli zao za kulinda tabianchi huku zinafisha ripoti zingine,” wamesema wataalamu hao. 

“Lazima tukemee na tusivumilie kabisa ulaghai huu kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Jopo la wataalamu leo linaripoti na kutoa mwongozo wa jinsi ya kuhakikisha ahadi zinakuwa za uhakika, wajibishi na zinalenga kuhakikisha kuwa hewa chafuzi inayozalishwa inafyonzwa,” amesema Katibu Mkuu Guterres wakati akizindua ripoti hiyo leo huko Sharm el-Sheikh, nchini Misri wakati wa mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mabadiliko ya tabianchi, COP27. 

Miongozo na ufafanuzi kwa taasisi zisizo za kiserikali 

Mwaka jana wakati wa COP26, huko Glasgow, Uingereza, Katibu Mkuu Guterres alitangaza kuwa anaunda Jopo la Wataalam kushughulikia mkanganyiko wa ziada na pengo la uhalali kuhusu malengo ya taasisi zisizo za kiserikali ya kuhakikisha hewa chafuzi inayozalishwa, inafyonzwa. 

Ripoti ya leo ya jopo hilo inatokana na kazi nzito ya zaidi ya miezi sab ana inaonesha ushauri bora kutoka kwa wataalamu hao wabobevu 17 waliochaguliwa na Katibu Mkuu Guterres. 

Kupitia mapendekezo 10, ripoti hiyo inatoa ufafanuzi wa maeneo makuu manne ambayo Katibu Mkuu Guterres ameyaainisha kama: Maadili ya kimazingira, Uaminifu, Uwajibikaji na Majukumu ya serikali. 

Ni kwa mtazamo huo Katibu Mkuu Guterres anafafanua: 

Mosi: Ahadi haziwezi kuwa jalada la kuziba uchafu 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ahadi za kuondoa hewa chafuzi zinazozalishwa lazima ziendane na mapendekezo ya ripoti ya jopo la wataalamu wa kiserikali kuhusu mabadiliko  ya tabianchi, (IPCC) ya kwamba kiwango cha joto kisizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi. 
 
“Hii ina maana utoaji wa hewa chafuzi duniani lazima upungue kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030, na ikifika mwaka 2050 hewa inayotolewa iwe sawa na hewa inayofyonzwa au kuondolewa. Lazima kuwe na ahadi zenye malengo ya mpito kila baada ya miaka mitano kuanzia mwaka 2025,” amesema Katibu Mkuu. 

Malengo hayo lazima yahusisha hewa zote chafuzi na kwa mawanda yote. Kwa taasisi za fedha, ina maana shughuli zote za kifedha, biashara na kwa miji ina maana uchafuzi wote unaotoka moja kwa moja au si moja kwa moja kwenye shughuli zao za usambazaji. 

“Ujumbe ni wazi kwa wale wote wanaosimamia shughuli za kujitolea pamoja na Watendaji wakuu wa kampuni, mameya, magavana waliotoa ahadi. Zingatieni ahadi zentu na isifikie COP28.” 

Kwa kampuni za nishati kisukuku na wawezeshaji au wafadhili wao ambao wana ahadi zinazoengua shughuli hiyo inayozidi kumwaga sumu duniani, amesihi waangalie upya ahadi zao na kufuata mwongozo wa jopo la wataalamu. 

Pili: Mipango iwe ya kina na thabiti 

Bwana Guterres ametaka ahadi ziambatane na mipango ya utekelezaji ikiwemo kipindi cha mpito. 

“Menejimenti lazima ziwajibike kutoa ahadi hizo. Hii ina maana kuchechemua wazi kwa umma kuhusu hatua kwa tabianchi na kuweka dhahiri au wazi shughuli za uhamasishaji,” amesema Guterres akiongeza kuwa ukosefu wa viwango, kanuni na uwazi katika biashara ya hewa ya ukaa inatoa hofu. 

Halikadhalika, ahadi hizo ziweke bayana ni kwa vipi kipindi cha mpito kinaweza kushughulikia mahitaji ya wafanyakazi wa nishati kisukuku na sekta nyingine wanaweza kuathiriwa wakati wa mpito kuelekea nishati jadidifu. 

Tatu: Ahadi lazima ziwe wajibifu na wazi 

Katibu Mkuu ametoa wito kwa mipango ya udhibiti utoaji hewa chafui uchochee juhudi za kuweka viwango kwa mujibu wa ripoti, kupitia majukwaa ya wazi ya umma ambayo yanaungainishwa moja kwa moja na Jukwaa la kimataifa la tabianchi la Umoja wa Mataifa. 

“Lazima tufanye kazi pamoja kuziba pengo la ukosefu wa mamlaka ya tatu inayotambulika kidunia na lazima tuimarishe mifumo iliyoko ya uthibitisho na uwajibikaji,” amesema Guterres. 

Nne: Mipango ya kujitolea iwe mwelekeo mpya sasa

Hatimaye Katibu Mkuu ametaka serikali zihakikishe kuwa mikakati ya kujitolea inakuwa ndio mwelekeo wa sasa. 

 “Nasishi viongozi wote wa serikali wapatie vyombo visivyo vya kiserikali kuwa na fursa sawa ya kuwa na eneo saw ana mustakabali wa kutoa na kufyonza hewa chafuzi. Kutatua janga la tabianchi kunahitaji uongozi thabiti wa kisiasa,” amesisitiza Katibu Mkuu akitoa wito kwa nchi Tajiri kuchagiza harakati za kudhibiti hewa ya ukaa kwa kuonesha uongozi. 

Sauti ya wataalamu

Ripoti hii inakuja kwenye mwaka ambao dunia imekumbwa na janga la nishati likichochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine pamoja na majanga yasiyokoma ya mafuriko na ukame. 

Kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya heaw chafuzi zinadhibitiwa na ahadi za kufyonza hewa hizo kutoka angani. 

“Kwa sasa, sayari dunia haiwezi kusubiri, kukubali sababu au ahadi za uongo,” amesema Catherine McKenna, Mwenyekiti wa jopo hilo na Waziri kutoka Canada. 

Ameeleza kuwa katika wakati muhimu kama huu, ahadi za kudhibiti hewa chafuzi inamaanisha kupunguza utoaji hewa chafuzi na si kupindisha maneno.