Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtama waenda kuoteshwa anga za juu kwa majaribio

Zao la mtama
FAO/Sandro Cespoli
Zao la mtama

Mtama waenda kuoteshwa anga za juu kwa majaribio

Tabianchi na mazingira

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la nishati ya atomiki, IAEA na la chakula na kilimo, FAO yamepeleka mbegu za mazao huko kwenye kituo cha kimataifa cha anga za juu ikiwa ni sehemu ya juhudi zao za kupata mbegu mpya zinazoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa iliyotolewa leo katika miji ya Virginia, MArekani, Roma, Italia na Vienna Austria imesema mbegu zilizopelekwa ni za mtama na nyingine iitwayo Arabidopsis  ambayo ni ya jamii ya kabichi na haradali na ambayo hutumika zaidi kwenye majaribio ya kijenetiki.

Hatua hiyo imefanyika leo wakati viongozi wanakutana huko Sharm el-Sheikh nchini Misri kwenye mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC, COP27 kujadili changamoto kubwa za kimazingira, ikiwemo madhara ya janga la tabianchi kwenye mifumo ya uzalishaji chakula duniani.

Mtama anga za juu

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi amesema ni sayansi ya nyuklia kwa mara nyingine tena inaonesha uwezo wake wa kipekee wa kukabili mabadiliko ya tabianchi.

“Ni matumaini yangu kuwa jaribio hili litaleta uvumbuzi: matokeo ambayo tutayasambaza bure kwa wanasayansi na mazao mapya ambayo yatasaidia wakulima kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji wa chakula,” amesema Bwana Grossi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu amesema, “mamilioni ya wakulima wadogo duniani wanahitaji mbegu zenye mnepo na za ubora wa hali ya juu ili waweze kukabiliana na changamoto zinazoongezeka za mazingira ya kilimo. Sayansi bunifu kama vile kuboresha aina ya mbegu anga za juu kunaweza kuleta mazao yaliyoboreshwa na kufungua njia angavu na yenye nuru zaidi kwa uzalishaji bora siku za usoni, lishe bora, mazingira bora na maisha bora.”

Mbegu bora za kuhimili tabianchi

Mbegu aina ya Arabidopsis, ni ya mmea unaotumika zaidi kwenye majaribio ya kijenetiki kutokana na sifa zake za kipekee, ilhali mtama, ni nafaka yenye virutubisho lukuki kwa ajili ya binadamu na chakula cha wanyama, halikadhalika Ethanol.

Mbegu hizo zitawekwa ndani na nje ya kituo cha kimataifa cha anga za juu kwa takribani miezi mitatu na kupata mazingira tofauti tofauti ikiwemo viwango vya chini vya joto.

Kwa mujbu wa ripoti ya jopo la kiserikali, upatikanaji wa chakula duniain utapungua siku za usoni kutokana na mabadiliko ya tabianchi na hivyo aina mpya za mazao zikipatikana zitasaidia wakulima na watunga sera ambao wanahitaji mabadiliko makubwa katika uwekezaji ili kukabili mabadiliko ya tabianchi na kuwa na uendelevu kwenye uzalishaji wa chakula.

Hili ni jaribio la kwanza la IAEA na FAO kupeleka mbegu za mazao anga za juu.