Wenye ukoma wasubiri muda mrefu kutambuliwa kuwa wana ulemavu

Mfanyabiashara aliyeathiriwa na ukoma akisubiri wateja mjini Addis Ababa, Ethiopia.
ILO/Fiorente A.
Mfanyabiashara aliyeathiriwa na ukoma akisubiri wateja mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Wenye ukoma wasubiri muda mrefu kutambuliwa kuwa wana ulemavu

Haki za binadamu

Watu wenye ukoma na familia zao wamesubiri muda mrefu sana ili haki zao za kuwa na ulemavu ziweze kutambuliwa kitaifa na kimataifa, amesema mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa hii leo kwa ripoti yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Alice Cruz, ambaye ni mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ukoma amesema watu walioathiriwa kwa ukoma wanapaswa kutambuliwa kikamilifu kuwa wana ulemavu, kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu, CRPD kwa misingi kwamba ulemavu wao wa viungo umesbabishwa na ukoma, na zaidi ya yote unyanyapaa wanaokabiiliwa nao umetokana na fikra potofu za ukoma wenyewe.

 

Ameongeza kuwa wanafamilia wenyewe wa mtu ambaye ana ukoma, nao pia hujitambulisha kuwa ni watu wenye athari za  ulemavu wa kisaikolojia kutokana na unyanyapaa na ubaguzi kwa msingi wa ukoma.

Bi. Cruz amesema “licha ya changamoto hizo, wenye ukoma na wafamilia zao wamekuwa kwa kiasi kikubwa wakitengwa kwenye mjadala wa kimataifa kuhusu ubaguzi.”

Mtaalamu huyo amesema pamoja na kutambua hatua katika ngazi ya kitaifa ya kuweka usawa kwa watu wenye  ukoma na wale wenye ulemavu, bado anataka hatua zaidi zichukuliwe ili kutekekeleza kwa kina vipengele vilivyomo kwenye mkataba wa watu wenye ulemavu.

Mathalani ametaja suala la haki za ulemavu kwenye suala la hifadhi ya jamii ambapo kuna utata ni nani ana haki ya kujumuishwa na kwamba anasema suala hilo linaachiwa madaktari na kutopatiwa kipaumbele kwenye utungaji wa sera.

Kwa mantiki hiyo ametaka serikali ziongeze maradufu harakati zao za kulinda na kusongesha haki za watu walioathirika kwa ukoma na familia zao kwa kutambua haki zao na washiriki kwenye  utungaji wa sera.

Serikali zipitie upya vigeza vya masharti ya kunufaika na hifadhi ya jamii ili watu wenye ulemavu usioonekana na watu wenye ulemevu na wanaoishi kwenye umaskini waweze kujumuishwa pia.

Amesihi mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali kushirikiana na kutumia ukoma kama mfano wa ushahidi wa kuonesha uhusiano kati ya ulemavu na umaskini ili suala la ukoma liweze kujumuishwa wakati wa uchambuzi wa masuala ya haki.