Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili zaidi unahitajika kwa ajili ya kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:UNEP 

Msichana akiwa amebeba mtoto akielekea katika kituo cha afya cha kuhamahama baada ya kijiji chao kuathirika na mafuriko nchini Paskistan
© UNICEF/Shehzad Noorani
Msichana akiwa amebeba mtoto akielekea katika kituo cha afya cha kuhamahama baada ya kijiji chao kuathirika na mafuriko nchini Paskistan

Ufadhili zaidi unahitajika kwa ajili ya kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:UNEP 

Tabianchi na mazingira

Nchi lazima zichukue hatua haraka ili kukabiliana na athari za sasa na zijazo za mabadiliko ya tabianchi, kwani juhudi za sasa ni ndogo sana nana zinafanyika  polepole mno, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP) katika ripoti yake iliyochapishwa leo.

Ripoti hiyo “Pengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi 2022” imetolewa kabla ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa COP27, utakaofunguliwa rasmi mwishoni mwa juma hili huko Sharm El-Sheikh, nchini Misri. 

Ripoti inatoa wito wa kuongezeka kwa ufadhili na utekelezaji wa hatua zinazolenga kusaidia wakati huu hatari zikiongezeka. 

Makadirio ya mahitaji ya kila mwaka ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kati ya dola bilioni 160 hadi had idola bilioni 340 kufikia mwisho wa muongo huu, na had idola bilioni 565 kufikia mwaka 2050. 

Hatua za haraka zahitajika sasa 

Inger Andersen, mkurugenzi mtendaji wa UNEP amesema. "Mabadiliko ya tabianchi ni pigo kubwa baada ya pigo kubwa kwa wanadamu, kama tulivyoshuhudia katika mwaka 2022 zaidi katika mafuriko ambayo yaliweka sehemu kubwa ya Pakistan chini ya maji. Dunia lazima ipunguze kwa haraka utoaji wa gesi chafuzi ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini lazima pia tuongeze juhudi kwa haraka kukabiliana na athari ambazo tayari ziko hapa na zile zijazo.” 

Ripoti hiyo inasisitiza kwamba kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kukabiliana na hali hiyo, lazima kuwa msitari wa mbele na katika hatua za kimataifa za kupambana na mzozo wa mabadiliko ya tabianchi. 

Watoto wakichota maji ya kunywa katika bomba lililofunikwa na maji ya mafuriko kwenye jimbo la Sindh nchini Paskistan
© UNICEF/Asad Zaidi
Watoto wakichota maji ya kunywa katika bomba lililofunikwa na maji ya mafuriko kwenye jimbo la Sindh nchini Paskistan

Athari zitaongezeka 

Chini ya Mkataba wa kihistoria wa Paris wa 2015 kuhusu mabadiliko ya tabianchi, nchi ziliahidi kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto 1.5°C juu ya kiwango cha joto cha kabla ya kuanza kwa maendeleo ya viwanda lakini lengo hilo bado liko mbali sana. 

Ripoti imeendelea kusema kwamba mafuriko ya Pakistani na athari nyingine za sasa, kama vile ukame wa kihistoria katika Pembe ya Afrika, vinatokea wakati ongezeko la joto duniani ni nyuzi joto 1.1°Celsius tu juu ya viwango vya kabla ya maendeleo ya viwanda. 

Katika ripoti nyingine iliyotolewa mapema wiki hii, UNEP ilisema michango iliyodhamiriwa ya kitaifa (NDCs) ambayo ni mipango ya kitaifa ya serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inaelekeza kwenye ongezeko la joto la hadi nyuzi joto 2.6 ° C ifikapo mwisho wa karne hii. 

Zaidi ya hayo, utafiti kutoka kwa jopo la serikali mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabianchi (IPCC) unaonyesha kuwa hatari za mabadiliko ya tabianchi zitaongezeka kila sehemu ya kumi ya nyuzi joto. 

Barafu ya mlima ambayo inapungua kwa sababu ya halijoto inayoongezeka na theluji kidogo katika Wilaya ya Kargil, India.
© UNICEF/Srikanth Kolari
Barafu ya mlima ambayo inapungua kwa sababu ya halijoto inayoongezeka na theluji kidogo katika Wilaya ya Kargil, India.

Dunia inashindwa kulinda watu wake 

Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, ripoti hiyo inaweka wazi kuwa dunia inashindwa kuwalinda watu kutokana na kile alichokiita "athari za hapa na pale za mabadiliko ya tabianchi” 

Ameonya kwamba "Mahitaji ya kukabiliana na hali hiyo katika ulimwengu unaoendelea yanatarajiwa kuongezeka hadi kufikia dola bilioni 340 kwa mwaka ifikapo 2030. Hata hivyo msaada wa kukabiliana na hali hiyo leo unasimama chini ya moja ya kumi ya kiasi hicho. Jamii na watu walio katika mazingira magumu zaidi wanalipa gharama kubwa na hili halikubaliki.” 

Ripoti imegundua kuwa maendeleo ya kukabiliana na hali hiyo yamekuwa "ya polepole na yasiyo na tija kubwa". 

Ripoti pia imebainisha kuwa asilimia 80 ya nchi zina angalau chombo kimoja cha kitaifa cha kupanga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wakati theluthi moja ya serikali 197 ambazo ni sehemu ya mkataba wa mfumo wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC) zimejumuisha malengo yanayokadiriwa na ya muda maalum ya kukabiliana na hali hiyo. 

Mabadiliko ya tabianchi yameongeza hatari ya hali ya hewa kavu, ya joto ambao inachangia kuchochea moto wa nyika
Unsplash/Mikhail Serdyukov
Mabadiliko ya tabianchi yameongeza hatari ya hali ya hewa kavu, ya joto ambao inachangia kuchochea moto wa nyika

Ufadhili katika suala hilo 

Ripoti inasema zaidi ya hayo, karibu asilimia 90 ya zana za upangaji zilichunguzwa zinaonyesha uzingatiaji wa jinsia na makundi yaliyotengwa, kama vile watu wa kiasili. 

Hata hivyo, ufadhili wa mipango hii ya kukabiliana na  mabadiliko ya tabianchi unabakia kuwa jambo la msingi.  

Kwa mujibu wa ripoti makadirio ya gharama za kukabiliana na hali hiyo ni mara tano hadi 10 zaidi ya mtiririko wa fedha wa kukabiliana na hali ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea, ambao ulifikia dola bilioni 29 mwaka 2020, ikiwa ni ongezeko la asilimia nne zaidi ya mwaka uliopita. 

Mwaka 2020, mtiririko wa pamoja wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza mtiririko wa fedha ulipungua kwa angalau dola bilioni 17 pungufu ya dola bilioni 100 zilizoahidiwa kila mwaka kwa nchi zinazoendelea. 

UNEP inasema ongezeko kubwa linahitajika ili kufikia lengo la kuongeza mtiririko wa fedha wa 2019 ifikapo mwaka 2025, kama ilivyosisitizwa katika matokeo ya mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa COP26, uliofanyika mwaka jana huko Glasgow, Scotland. 

"Mataifa yanahitaji kuunga mkono maneno makali katika mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Glasgow kwa hatua kali ili kuongeza uwekezaji na matokeo ya kukabiliana na hali hiyo, kuanzia COP27," amesema Bi Andersen. 

Wakati huo huo, amesema ingawa utekelezaji wa hatua za kukabiliana na hali hiyo hasa katika kilimo, maji, mifumo ikolojia na sekta zingine mtambuka unaongezeka, hauendani na athari za mabadiliko ya tabianchi na unaweza kuzidiwa nguvu na kasi ya hatari za hali ya hewa.