Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yapatia mafunzo wafanyabiashara Sudan Kusini ili wafanye biashara kwa ufanisi

Soko nchini Sudan Kusini
© UNICEF/Sebastian Rich
Soko nchini Sudan Kusini

UNMISS yapatia mafunzo wafanyabiashara Sudan Kusini ili wafanye biashara kwa ufanisi

Ukuaji wa Kiuchumi

Ushirikiano na ukuaji kiuchumi ni miongoni mwa masuala muhimu katika kuhakikisha nchi yoyote ina amani na wananchi wake wanapata Maendeleo. Na ili kuhakikisha wananchi wa Sudan Kusini wana amani na maendeleo, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda Amani nchini humo UNMISS umeandaa warsha ya biashara lengo likiwa ni kuwatia moyo wafanyabiashara wa ndani na kuwawezesha kiuchumi ili nao waweze kuimarisha biashara zao lakini pia waweze kufanya biashara na Umoja wa Mataifa .

Nchi ya Sudan Kusini ambayo sasa inapona makovu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na janga la COVID-19, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS unawasaidia wananchi kujenga upya amani na ustawi bora wa Maisha yao.

Namna moja wapo ya kuwasaidia wananchi hawa ni kuwajengea uwezo wafanyabiashara ili waweze namna ya kufanya biashara na Umoja wa Mataifa kama alivyoeleza Kessiah Mwamungu, Kaimu Mkuu wa Manunuzi wa UNMISS.

Tweet URL

“Ni muhimu sana kufanya warsha hii kuwajengea uwezo makampuni ya Sudan Kusini ili nao waweze kufanya biashara na Umoja wa Mataifa na pia watumie fursa hii ya uwepo wa Umoja wa Mataifa, lakini hili ni moja tu jingine ni kuwajengea uwezo kiuchumi na kuwafanya sekta binafsi waweze kukuwa kitu ambacho kina mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa kiuchumi wa viwango vya taifa nyingine lolote.”

Mjasiriamali Jacob Bengamin ni mmoja kati ya wanaopatiwa mafunzo na anasema aliwahi kukosa mafunzo hayo na sasa ameamua kuchangamkia fursa hiyo anasema “Hii ni warsha ya kuvutia sana, nilikosa kuhudhuria kwenye warsha ya awali lakini hii nimefanikiwa kuhudhuria hii na naweza kusema imenifungua macho jinsi Umoja wa Mataifa unavyofanya kazi na pia nimejua kuwa Umoja wa Mataifa kumbe unatoa fursa za biashara hapa nchini kwetu Sudan Kusini.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Womens Block, Amer Deng anasema amekuwa katika biashara kwa muda mrefu na ameona kuwa wanawake wengi wa Sudan Kusini wanakose elimu ya kuwajengea uwezo kwenye biashara.

“Na biashara inahitaji ufanye majaribio sana na kupata elimu kwakiashi kukubwa ili uweze kufanikiwa, kwa mfano hii leo tumepata maarifa mengi na taarifa kutoka kwa wawasilishaji wa UNMISS na tuna furaha na kuona fahari na tuko na uhakika kwamba tutafanya kazi pamoja.”

Mgeni rasmi katika Warsha hiyo ni Sara Beysolow Nyanti ambaye ni Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa shirika la kuratibu misaada ya dharura OCHA nchini Sudan Kusini anasema baada ya mafunzo ya kwanza kutolewa mwaka 2021 kwa wafanyabiashara 52, walifanya uchunguzi na matokeo yalikuwa yakuridhisha.

“Kutoka kwenye uchunguzi tuliofanya, ni Dhahiri washiriki walinufaika na warsha waliyopatiwa, washiriki waliona thamani kwenye kile tulichowafundisha, na inatupa moyo sisi UNMISS hapa nchini Sudan Kusini kuona kwamba wajasiriamali wa Sudan Kusini na wafanyabiashara wameimarika zaidi na zaidi na wanasaka masoko mpaka nje ya mipaka yao kwenda kufanya biashara na nchi za Afrika Mashariki”.