Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yachochea ongezeko la wagonjwa wa TB duniani- WHO

Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya
UNOCHA/Giles Clarke
Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya

COVID-19 yachochea ongezeko la wagonjwa wa TB duniani- WHO

Afya

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani WHO inakadiria kuwa watu milioni 10.6 waliugua kifua kikuu (TB) mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.5 kutoka mwaka 2020, na watu milioni 1.6 walikufa kutokana na TB kati yao watu 187,000 wakiwa na Virusi Vya UKIMWI.

Taarifa ya shirika hilo kutoka Geneva Uswisi imesema ripoti hiyo ya mwaka 2022 ya Kifua Kikuu imeonesha kuwa hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi kuwa na ongezeko wa wagonjwa wa kifua kikuu na wengine asilimia 3 wamepata usugu wa dawa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametaja janga la COVID-19 kuwa kichocheo cha watu wengi kukosa dawa za kujitibu kifua kikuu.

“Kama kuna kitu tumejifunza kutokana na janga la CORONA ni kwamba kwa mshikamano, kufanya maamuzi, uvumbuzi na utumiaji sawa wa zana, tunaweza kushinda vitisho vikali vya kiafya. Hebu tutumie masomo hayo kwenye eneo la kifua kikuu. Ni wakati wa kumkomesha muuaji huyu wa muda mrefu. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kukomesha TB.”

Kifua Kikuu ni muuaji wa pili

Ugonjwa wa Kifua kikuu ni muuaji wa pili wa magonjwa ya kuambukiza duniani, baada ya COVID-19.

Ugonjwa huu husababishwa na bakteria ambao mara nyingi huathiri mapafu, lakini unaweza kuzuilika na kutibika.

Huduma za afya kwa ujumla ziliathiriwa sana wakati wa janga la COVID-19, lakini athari zake kwa wagonjwa wa TB imekuwa mbaya sana, hali ambayo imekuwa mbaya zaidi kutokana na migogoro inayoendelea huko Ulaya, Afrika pamoja na Mashariki ya Kati.

Kuendelea kwa changamoto za kutoa na kupata huduma muhimu za TB kumesababisha watu wengi waliokuwa na ugonjwa huo kutogunduliwa na kutibiwa.

Wanawake wawili ambao wanapata matibabu ya kifua kikuu mjini Addis Ababa , Ethiopia.
The Global Fund/John Rae
Wanawake wawili ambao wanapata matibabu ya kifua kikuu mjini Addis Ababa , Ethiopia.

Utambuzi na matibabu wapungua

Idadi ya watu waliogunduliwa hivi karibuni ilipungua kutoka milioni 7.1 mwaka 2019 hadi milioni 5.8 mwaka 2020, kulingana na ripoti ya hivi punde ya Global TB. Ingawa kulikuwa na ahueni ya kiasi hadi milioni 6.4 mwaka 2021, hata hivyo utambuzi huo bado ulikuwa chini ya viwango vya kabla ya janga.

Kupungua huku kunaonesha kuwa idadi ya watu wenye TB ambayo haijagunduliwa au ambayo haijatibiwa imeongezeka, WHO imesema, na kusababisha Mosi, kuongezeka kwa vifo na maambukizi zaidi ya jamii, na hatimaye watu wengi zaidi wanaougua ugonjwa huo.

Idadi ya watu wanaopokea matibabu ya RR-TB na TB sugu ya dawa nyingi (MDR-TB) pia ilipungua kati ya 2019 na 2020. Takriban watu 161,746 walianza matibabu ya RR-TB mwaka 2021, saw ana takriban theluthi moja tu ya wale waliohitaji.

Matumizi ya kimataifa katika huduma muhimu za TB pia yalipungua, kutoka dola bilioni 6 mwaka 2019 hadi dola bilioni 5.4 mwaka 2021, ikiwa ni chini ya nusu ya lengo la kimataifa la dola bilioni 13 kila mwaka ifikapo mwaka huu.

India inaendelea kubeba mzigo mkubwa zaidi wa wagonjwa wa kifua kikuu Duniani
ILO Photo/Vijay Kutty
India inaendelea kubeba mzigo mkubwa zaidi wa wagonjwa wa kifua kikuu Duniani

Hatua za haraka zinahitajika

Kumekuwa na habari njema, ulimwenguni kote, watu milioni 26.3 walitibiwa TB kati ya 2018 na 2021, ingawa tena, bado ni pungufu ya lengo la milioni 40 lililowekwa miaka minne iliyopita.

Matibabu ya kuzuia TB kwa watu wanaoishi na VVU pia ilivuka lengo la kimataifa la milioni sita, na kufikia zaidi ya milioni 10 katika kipindi hicho.

Ripoti hiyo inasisitiza haja ya nchi kutekeleza hatua za haraka kurejesha upatikanaji wa huduma muhimu za TB.

Pia inataka uwekezaji uongezeke, na hatua zichukuliwe, kushughulikia kwa upana wake viambukizi vinavyosababisha milipuko ya TB na athari zake za kijamii na kiuchumi pamoja na hitaji la uchunguzi mpya, dawa na chanjo.

WHO itaitisha mkutano wa ngazi ya juu mapema mwaka 2023 ili kuimarisha maendeleo ya chanjo, kwa kuzingatia walichojifunza kutoka kwa janga hili.