Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti mbili za UN zatilia shaka hatua za nchi za kupunguza joto duniani ifikapo 2030

Vijana wanaharakati wakiwa wameketi kwenye mitaa ya Bangladesh wakitaka hatua kwa tabianchi
© UNICEF/Jannatul Mawa
Vijana wanaharakati wakiwa wameketi kwenye mitaa ya Bangladesh wakitaka hatua kwa tabianchi

Ripoti mbili za UN zatilia shaka hatua za nchi za kupunguza joto duniani ifikapo 2030

Tabianchi na mazingira

Ingawa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimechukua hatua kupunguza utoaji wa hewa chafuzi, bado hatua hizo hazitoshelezi kuhakikisha kiwango cha joto duniani hakizidi nyuzi 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo.

Ikitolewa jijini New York, Marekani na Sekretarieti ya Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC, ripoti inasema viwango vyote vya sasa vya nchi 193 vya kupunguza utoaji hewa chafuzi vinaweza kurejesha kwenye  mwelekeo wa nyuzi joto 2.5 katika kipimo cha selsiyasi ifikapo mwishoni mwa karne hii ya 21.

Kasi ni ndogo sana hebu nchi zitekeleze hatua za kijasiri

Katibu Mtendaji wa UNFCCC Simon Stiell anasema, “mwelekeo wa kupunguza utoaji hewa chafuzi unaotarajiwa ifikapo mwaka 2030 unaonesha kuwa mwaka huu nchi zimepata maendeleo makubwa. Lakini sayansi iko dhahiri na vivyo hivyo malengo yetu ya tabianchi kwa mujibu wa Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi. Bado hatujakaribia kokote kwenye punguza la hewa chafuzi linalotakiwa ili kutovuka nyuzi joto 1.5.”

Amesema ili lengo hilo liendelee kuwa hai, serikali zinahitaji kuimarisha mipango yao ya hatua kwa tabianchi na kuitekeleza katika kipindi cha miaka minane ijayo.

Nishati  ya kisukuku ni moja ya visababishi vya hewa chafuzi zinazoongeza joto duniani
UN
Nishati ya kisukuku ni moja ya visababishi vya hewa chafuzi zinazoongeza joto duniani

Ripoti ya leo inaonesha ahadi za sasa za serikali zinaweza kuongeza utoaji hewa chafuzi kwa asilimia 10.3 ifikapo mwaka 2030 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2010.

“Hii inatia moyo ikilinganishwa na tathmini ya mwaka jana ambayo ilibaini kuwa viwango vilivyokuweko vingaliendelea kama vilivyo, basi ongezeko la utoaji hewa chafuzi lingalikuwa  asilimia 13.7 mwaka 2030 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2010.

Ripoti ya jopo la wataalamu wa kiserikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyotolewa mwaka 2018 ilionesha kuwa viwango vya hewa chafuzi ya ukaa vinapaswa kupunguzwa kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030, ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2010.

Nini kifanyike COP27 Sharm el Sheikh?

Wakati mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa UNFCCC ukikaribia, Bwana Stiell anatoa wito kwa serikali kuangalia upya mipango yao ya hatua kwa tabianchi na kuchukua hatua za kijasiri zaidi ili kuziba pengo la mwelekeo wa utoaji hewa chafuzi na kile ambacho sayansi inasema kinapswa kufanyika muongo huu.

 “COP 27 ni fursa ambako viongozi watapata tena kasi ya mabadiliko ya tabianchi na kuchukua hatua sahihi kutoka mashauriano kwenda kwenye utekelezaji na kufanya marekebisho makubwa kwenye sekta mbalimbali za kijamii ili kushughulikia dharura ya tabianchi,” amesema Katibu Mtendaji huyo wa Sekretarieti ya UNFCCC.

Viwango vya Methani na hewa ya Ukaa vyaongezeka- WMO

Katika hatua nyingine, shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa, WMO, hii leo nalo limetoa ripoti yake kuelekea COP27 ambapo imesema imerekodi viwango vya juu zaidi ya hewa aina ya Methani, moja ya aina tatu ya hewa chafuzi duniani. Hewa nyingine ni hewa ya ukaa au Carbon Dioxide na Nitrious Oxide.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo New York, Marekani na Geneva, Uswisi, WMO imesema  tangu kuanza kuanza kurekodi viwango vya Methane miaka 40 iliyopita, mwaka 2021 umekuwa na viwango vya juu zaidi na kwamba sababu mahsusi ya ongezeko hilo haiko dhahiri, lakini yaonekana ni matokeo ya michakato ya kibailojia na kibinadamu.

Takwimu zinaonesha ongezeko la hewa ya ukaa mwaka 2021 kuwa ni asilimia 149, Methani asilimia 262 na nitrious Oxide asilimia 124.

Mwanasiasa nchini Tuvalu Simon Kofe akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Tuvalu kwenye ujumbe wake aliorekodi kwa ajili ya COP26
Wizara ya Sheria Tuvalu
Mwanasiasa nchini Tuvalu Simon Kofe akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Tuvalu kwenye ujumbe wake aliorekodi kwa ajili ya COP26

Katibu Mkuu wa WMO Profesa Petteri Taalas anasema, “jarida la hewa chafuzi la WMO linadokeza tena kuwa changamoto kubwa na udharura wa kuchukua hatua kupunguza hewa chafuzi na kuzuia ongezeko la joto duniani siku zijazo.”

Amesema kuendelea kuwepo kwa hewa zinazodaka joto, ikiwemo viwango vya juu vya Methani “kunaonesha kuwa mwelekeo wetu si mzuri.”

Hatua za kuchukua

Kuna mikakati ya gharama nafuu ya kukabili utoaji wa hewa ya Methane hasa kwenye sekta ya mafuta kisukuku, amesema Profesa Taalas akifafanua “tunapaswa kutekeleza hii mapema. Hata hivyo Methani athari zake hudumu muda mfupi, kama miaka 10 na hivyo athari zake kwa tabianchi zinarekebishika. Kipaumbele kikubwa sasa ni kukata utoaji wa hewa ya ukaa ambayo ndio kichochezi kikubwa cha hali za hewa zilizopitiliza na ambayo itaathiri tabianchi kwa maelfu ya miaka; kupotea kwa theluji, joto kwenye maji ya bahari na ongezeko la viwango vya maji ya bahari.”

Ametaka kubadilishwa kwa mifumo ya viwanda,nishati, mifumo ya usafirishaji na  mienendo ya maisha. Mabadiliko yanayohitajika yanawezekana kiuchumi na kiufundi. Wakati unasonga kwa kasi,” amesema Profesa Taalas.